Michezo

Mwanariadha chipikuzi ahofia mabadiliko ya KCSE yatamvuruga

April 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Afrika katika mbio za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18, Jacob Krop, amesema kwamba janga la corona litavuruga mipango yake ya kujiandaa kwa mashindano yajayo iwapo ratiba ya mitihani ya kitaifa ya KCSE itabadilishwa mwaka huu.

Krop ni miongoni mwa maelfu ya wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne mwaka huu.

Hofu yake ni kuwa iwapo corona itaathiri kalenda ya sekta ya elimu, basi huenda akakabiliwa na mtihani mgumu wa muda mrefu wa kumakinikia riadha na masomo kwa viwango sawa.

Licha ya umri wake mdogo, Krop ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Chewoyet, Pokot Magharibi, tayari anajivunia umaarufu katika ulingo wa riadha. Anashikilia kwamba kukamilika kwa safari yake ya elimu ya sekondari mwaka huu kutampa jukwaa mwafaka zaidi la kuzamia ulingo wa riadha kikamilifu.

Ni matumaini yake kuwa janga la corona halitaathiri ratiba ya awali ya Wizara ya Elimu na Baraza la Mitihani kuhusu tarehe za kufanywa kwa mitihani ya kitaifa mwaka huu.

Krop aliwakilisha Kenya katika Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar mwaka jana na akaambulia nafasi ya sita kwenye mbio za mita 5,000 alizozikamilisha kwa dakika 13:03.08. Huo ndio ulikuwa muda wake bora zaidi katika historia ya kushiriki mbio hizo.

Awali, alikuwa ameandikisha muda wa dakika 13:14.44 katika mbio za Afrika zilizoandaliwa jijini Abidjan, Ivory Coast mnamo Aprili 2019.

“Corona inatisha! Nilitarajia kukamilisha masomo yangu ya sekondari mwaka huu. Hofu zaidi ni kwamba mabadiliko yoyote katika ratiba ya mitihani huenda ikaathiri maandalizi yangu kwa mashindano kadhaa niliyotazamia kushiriki mwaka ujao baada ya kuahirishwa mwaka huu,” akasema.

Krop ambaye pia ni mshikilizi wa taji la mbio za kilomita 10 za Endebess Road anaamini kwamba ndiye atakayetwalia Kenya nishani ya dhahabu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 17 kwenye Riadha za Dunia kipute hicho kitakapoandaliwa jijini Oregon, Amerika mnamo 2022.

Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo ambayo imekuwa ikitamalakiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah wa Uingereza kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hata kwenye Michezo ya Olimpiki haijawa ya kuridhisha katika miaka 30 iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988.

“Mbio za mita 5,000 ni fani ambayo imekuwa ikiwaumiza vichwa mashabiki, wanariadha na vinara wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kwa kipindi kirefu. Naamini ushindi wangu utatoa suluhu ya kudumu ambayo itashuhudia ufufuo wa Kenya katika fani hii ambayo kwa sasa inatawalia na Waethiopia,” akasema Krop.