Michezo

Mwanariadha maarufu Ben Jipcho azikwa nyumbani kwake Kisawai, Trans-Nzoia

July 31st, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA mara mbili wa Michezo ya Afrika, Ben Jipcho amezikwa leo Ijumaa asubuhi nyumbani kwake katika kijiji cha Kisawai, Kaunti ya Trans-Nzoia katika maziko yaliyohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto miongoni mwa viongozi wengine.

Dkt Ruto amesema serikali imejitolea kuwatambua majagina katika ulingo wa michezo.

“Serikali ina mpango wa kuwatuza wanariadha watakaoibuka mabingwa katika vitengo mbalimbali vya michezo,” amesema Dkt Ruto.

Aidha, amesema watakaoshinda dhahabu watakuwa wakipokea Sh1 milioni huku watakaopata fedha kila mmoja akipokea Sh500,000 nao wa nishani ya shaba wakipokea Sh250,000 kiasi cha tuzo.

Jipcho ambaye pia ni mshindi wa zamani wa nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki za 1968, aliaga dunia mnamo Julai 24, 2020 katika hospitali ya Fountain mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu alikokuwa amelazwa kwa kipindi cha siku tatu. Alikuwa akitatizwa sana na maradhi ya mapafu, figo na ini kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa mwanawe wa kiume David Kwenden, mwili wa Jipcho ulitolewa katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH) mnamo Julai 30, 2020.

Kwenden amesema kwamba babaye ambaye pia ni bingwa mara mbili wa mbio za Jumuiya ya Madola, alikuwa nguzo na mhimili muhimu katika familia na ushauri wake ulitegemewa sana na maelfu ya wanariadha wa humu nchini ambao sasa wanatamba katika fani mbalimbali

“Alikuwa mtu mwenye moyo wa kutoa, baba aliyepanda familia yake na mzalendo kindakindaki. Tulimtegemea sana kwa mengi ila kifo kimemchukuwa wakati ambapo tulikuwa bado tunamhitaji sana,” akaongeza Kwenden katika kauli iliyoshikiliwa na dadaye Ruth Jipcho.

“Wiki moja kabla ya kuaga, baba alipata maradhi ya tumbo na akapelekwa katika Hospitali ya Crystal mjini Kitale alikotibiwa na kushauriwa kutafuta matibabu zaidi mjini Eldoret kabla ya hali yake ya afya kudorora,” akasema Ruth.

Akimwomboleza Jipcho, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock), Paul Tergat, alisema kwamba Jipcho ndiye baba mwanzilishi wa riadha za Kenya ambaye aliwafungulia watimkaji wote wazawa wa humu nchini milango ya heri na hatimaye kutamba katika ulingo wa kimataifa.

“Kifo kimetupiga pute johari adimu na kito cha thamani katika ulingo wa riadha. Tumesikitishwa sana na kifo cha Jipcho ambacho tumepokea kwa mshtuko mkubwa. Mola aifariji familia na wote walioguswa na kuondoka kwake,” akasema Tergat.

Aliyekuwa Mbunge wa Cherangany na bingwa wa Boston Marathon 2012, Wesley Kipchumba Korir alisema kuwa alimjua Jipcho kama mwanariadhaa mkomavu wa enzi zake ambapo aliletea nchi hii sifa tele yakiwemo mataji ya haiba.

“Ni miongoni mwa watimkaji ambao waliwawekea wanariadhaa chipukizi msingi wa kushindana katika majukwaa ya kimataifa, mimi nikiwamo. Familia ya wanariadha imempoteza mtu mashuhuri ambaye atakumbukwa kwa kukuza talanta za wanariadha wengi humu nchini. Alitegemewa sana kwa mawaidha na ni muhali sana kujaza pengo ambalo ameliacha,” akasema.

Jipcho alijitosa rasmi katika ulingo wa riadha katika miaka ya 60 na anakumbukwa kwa kujinyima nafasi ya kutwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 alizomwachia Mkenya mwenzake Kipchoge Keino kwenye Olimpiki za 1972.

Mnamo 1970, Jipcho alijizolea nishani ya fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Edinburgh, Scotland kabla ya kuambulia tena nafasi ya pili katika mbio hizo kwenye Olimpiki za 1972 jijini Munich, Ujerumani.

Mnamo 1973, alizoa medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Michezo ya Bara la Afrika iliyoandaliwa jijini Lagos, Nigeria.

Mnamo 1974, Jipcho alitwaa nishani za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji kisha akaridhika na nishani ya shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Christchurch, New Zealand.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Tawi la Magharibi, Patrick Kipsang, alisema wamempoteza gwiji waliyemtegemea mno katika masuala ya mashindano mbalimbali katika eneo lake.

“Alikuwa mkimbiaji stadi. Ingawa alikuwa akiishi Trans-Nzoia, Jipcho ana usuli wake katika eneo la Mt Elgon, Kaunti ya Bungoma – ngome ya miongoni mwa wanariadha maarufu zaidi kutoka humu nchini,” akasema Kipsang.