Mwanasheria Mkuu kukata rufaa ya BBI katika Mahakama ya Juu

Mwanasheria Mkuu kukata rufaa ya BBI katika Mahakama ya Juu

Na RICHARD MUNGUTI

MWANASHERIA Mkuu Paul Kihara Kariuki atawasilisha rufaa katika Mahakama ya Juu kujaribu kufufua mpango wa kurekebisha katiba BBI uliozamishwa Ijumaa na mahakama ya rufaa.

Punde tu baada ya majaji saba wa Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa zilizowasilishwa na Rais Uhuru Kenyatta , Mwanasheria Mkuu, aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wakili mkuu wa serikali Kennedy Ogeto alisema atakata rufaa.

“Majaji wenyewe walitofautiana kuhusu muundo msingi wa katiba ya Kenya.Pia kuna ubishi ikiwa Rais aliye mamlakani anaweza kushtakiwa au la,” Bw Ogeto aliambia Taifa Leo Ijumaa usiku.

Bw Ogeto alisema mahakama itawapa maamuzi saba ya kila jaji kisha watajua ni masuala yapi ambayo atakayopeleka kuamuliwa na Mahakama ya Juu chini ya uongozi wa Jaji Mkuu Martha Koome.

Katika uamuzi wao majaji hao walisema Rais anaweza kushtakiwa akiwa angali afisini endapo hatatekeleza majukumu yake kwa njia inayofaa.Hata hivyo Jaji Daniel Musinga na wenzake sita walitupilia mbali maagizo Rais Uhuru Kenyatta ashtakiwe kwa kukaidi sheria.

Majaji hao walitofautiana katika masuala mbali mbali iwapo Rais Kenyatta na Raila Odinga waliruhusiwa kisheria kuongoza mpango huo wa kurekebisha katiba.“Rais Kenyatta ndiye aliongoza harakati hizo za kurekebisha katiba kwa kuteua kamati ya BBI na kuchapisha majina yao katika gazeti rasmi la Serikali,” walisema majaji hao.

Mahakama ilisema kisheria Rais Kenyatta hapasi kuongoza zoezi la kurekebisha katiba kwa vile, “yeye sio mwananchi wa kawaida.”Majaji hao walisema ni wananchi wa kawaida wapatao milioni moja ambao wameandikishwa kuwa wapiga kura ambao wangeliongoza zoezi hilo.

“Wote wawili Rais Kenyatta na Bw Odinga waliongoza harakati za kufanyia sheria marekebisho sio –Wanjiku-” Jaji Musinga na wenza walisema.

Kati ya majaji hao saba ni Jaji Fatuma Sichale tu aliyetofautiana na wenza na kufutilia mbali uamuzi wa majaji watano wa mahakama kuu waliozima mpango wa kurekebisha katiba iliyozinduliwa 2010.

Kufurushwa kwa mchakato huo wa kurekebisha katiba ni pigo kubwa kwa Rais Kenyatta na mwenzake wa handisheki Bw Odinga waliozika tofauti zao za kisiasa Machi 2018 na kuamua kusaka amani na kuwaunganisha Wakenya.

“Sheria inasema zoezi hilo lapasa kuongozwa na wananchi wa kawaida na wala sio Rais Kenyatta ambaye sio mwananchi wa kawaida,” ilisema mahakama.Korti iliongeza kusema zoezi hilo lilitiwa dosari au ndoa na Rais Kenyatta ambaye walisema ni kiongozi wa nchi na wala “ÿeye sio Wanjiku.”

Mahakama hiyo ilikubaliana na majaji watano wa mahakama kuu waliozima Rege na kusema Rais Kenyatta anaweza kushtakiwa kwa kukiuka sheria.“Rais Kenyatta anaweza kushtakiwa kwa kutotii sheria,” walisema majaji hao.

Majaji hao walitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Rais Kenyatta kupitia kwa mawakili Waweru Gatonye na Mohammed Nyaoga akiomba korti iruhusu kura ya maoni ifanyike ili katiba irekebishwe.

Majaji saba wa mahakama hii iliyo ya pili kwa ukuu nchini baada ya Mahakama ya Juu ilisema “ijapokuwa katiba ya 2010 imetoa fursa ya kufanyiwa marekebisho kuna utaratibu uliowekwa wa kuzinduliwa na wananchi na wala sio Rais anayeongoza nchi.”

Majaji hao walikubaliana na majaji watano wa mahakama kuu kwamba tume ya uchaguzi huru na mipaka haina makamishna wa kutosha kuendeleza zoezi hilo.“Kifungu nambari 257 kimeeleza mpango wa kubadilishwa kwa Katiba unapasa kuanzishwa na wananchi wa kawaida,” walisema majaji hao.

Majaji hao walisema mpango huo ulizinduliwa wakati Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga Machi 2018.Rais wa Mahakama ya Rufaa Jaji Daniel Musinga aliyetoa utangulizi alisema, “Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 nchi hii ilitumbukia katika hali ya vurugu za kisiasa ndipo wapinzani wakuu katika kinyang’anyiro cha Urais Bw Kenyatta na Bw Odinga wakakutana na kuzika tofauti zao za kisiasa zilizosababisha hii kuzozana.”

Jaji Musinga alisema mpango wa maridhiano BBI ulizinduliwa na hatimaye ikabuniwa kamati iliyoongozwa na marehemu Seneta Yusuf Haji ilizuru maeneo mbali mbali kote nchini wakipokea maoni ya wananchi.

Hatimaye sahihi miliioni nne zilikusanywa na kuwasilishwa kwa IEBC kuzikagua.Jaji Musinga alisema kufuatia kubuniwa kwa kamati ya BBI Mbunge wa Suna mashariki Junet Mohammed na aliyekuwa Mbunge wa Dagoreti kusini Dennis Waweru waliridhi mpango huo na kuwasilisha sahihi milioni nne kwa IEBC chini ya uenyekiti wa Bw Wafula Chebukati.

Kwa sasa IEBC iko na makamishna watatu Bw Chebukati, Boya Molu na Abdi Yakub Guloye.Majaji hao walisema sheria inataka shughuli za IEBC ziendelezwe na makamishna watano.

Majaji walisema IEBC inatakiwa kuwa na makamishna saba ili iwe kamilifu.“Zoezi la kukagua sahihi milioni moja za wapiga kura zilifanywa na makamishna watatu na zoezi hilo halikuwa na mashiko kisheria,” walisema majaji hao.

Jaji Musinga alisema utaratibu huo wa kurekebisha katiba ulipingwa na mwanauchumi David Ndii akisema IEBC haina makamishna wakutosha kuendeleza kura ya maoni.Wakiongozwa na Jaji Musinga, majaji hao walisema sheria haikufuatwa kuzindua mfumo wa kurekebisha katiba.

Majaji hao walitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Rais Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kamati ya BBI na mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki kupinga uamuzi wa majaji watano wa mahakama kuu waliositisha rege.

Kila mmoja wa majaji hao saba Jaji Musinga , Jaji Roselyn Nambuye, Jaji Hannah Okwengu, Jaji Fatuma Sichale , Jaji Kairu Gatembu , Jaji Patrick Kiage  na Jaji William Tuiyot walisema maoni ya wananchi hayakushirikishwa kabla ya mchakato wa kubadilisha Katiba kuanzishwa.

Majaji hao waliikosoa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kwa kuanzisha harakati za kukagua sahihi milioni moja za wapiga kura kabla ya kura ya maoni kupigwa.

Mahakama hiyo iliamua masuala 23 waliowasilishwa wakati wa rufaa hiyo iliyopingwa vikali na mawakili Dkt John Khaminwa , Martha Karua , Elisha Ongoya miongoni mwa wengine waliomba mahakama iamuru Rais Kenyatta ashurutishwe kurudishia umma zaidi ya Sh4bilioni zilizotumika kamati ya BBI ilipozunguka nchini ikipokea maoni.

Uamuzi huo ulipokewa kwa furaha na mawakili Dkt Khaminwa na wengine waliopinga rufaa hiyo wakisema “BBI izamishwe.”Dkt Khaminwa aliipongeza mahakama akisema “imesimama kidete kutetea haki na katiba.”

Mawakili James Orengo , Otiende Amolo, Waweru Gatonye , Mohammed Nyaoga na Paul Mwangi waliowasilisha rufaa hiyo walisema watashauriana  na kufikia uamuzi ikiwa watakata rufaa katika Mahakama ya Juu au la.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Amerika inavyotumia unafiki kuendeleza...

DINI: Hatuna budi kusali wakati wa mabaya na mazuri tusije...