Habari Mseto

Mwanasiasa kutoka Meru anayedai kwa siku huingiza Sh20 milioni  

March 11th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MWANASIASA Mike Mutembei maarufu kama Makarina, kutoka Kaunti ya Meru ameonya wanaomdhalilisha kuwa maskini, akidai kwamba biashara ya uzoaji taka aliyowekeza humuingizia kima cha Sh20 milioni kwa siku.

Bw Makarina amesema kwamba yeye huwa na magari matatu ya kibinafsi ya kifahari na hakuna lililo chini ya thamani ya Sh20 milioni.

Anadai kwamba majengo anayomiliki hayawezi yakahesabika na pia pesa alizokopeshana ni nyingi ajabu.

Isitoshe, anajigamba akisema kwa mwezi mmoja pekee hutoa zaidi ya Sh300, 000 kusaidia wasiojiweza katika jamii yake ya Ameru.

Katika mkanda wa video ambao amepachika mitandaoni, Bw Makarina alisema kwamba “mimi sio maskini na sio mwizi. Huwa ninatuma maombi ya kandarasi na ninapata kutoka kwa serikali”.

Aliongeza kwamba “mimi ni wa upinzani ndio, lakini nina urafiki na serikali ambayo hunipa kandarasi na ninalipa”.

Mwanasiasa huyo alisisitiza kwamba yeye ni mwaminifu, na hulipa ushuru kwa serikali.

Aliteta kwamba licha ya kuwa mlemavu, hela hazijambagua, jambo analojivunia bila maringo.

“Mimi nikiamua kuringia Wameru hamtapata amani. Mimi nina pesa na si kidogo. Siwezi nikaomba pesa mimi. Hela ninazotembea nazo ni nyingi,” akasema huku akihesabu mamilioni ndani ya gari lake.

Alidai kwamba pesa anazobeba hazitoshei kiganja cha mikono, akitaka wanaomdhalilisha kumheshimu.