HabariSiasa

Mwanasiasa mkongwe Charles Rubia afariki

December 23rd, 2019 1 min read

NDUNGU GACHANE na CHARLES WASONGA 

MWANASIASA mkongwe na waziri za zamani Bw Charles Rubia amefariki Jumatatu, mwanawe wa kiume Maurice Rubia amethibitisha.

Alifariki nyumbani kwake mtaani Karen, Nairobi kutokana na kile ambacho familia yake imesema ni uzee.

Mwendazake Bw Rubia, mwenye miaka 96, ambaye alikuwa Meya wa kwanza nchini, amewaacha watoto wanne, wote wanaume.

“Alituacha Jumatatu asubuhi na tunashuku ni kutokana na uzee. Lakini tutasubiri ripoti ya daktari ili kuthibitisha madai yetu,” Bw Maurice Rubia, ambaye ni mwanawe, akaambia Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu.

Alisema kuwa, babake juzi alianza kupata matatizo ya kupumua na kuiambia familia yake kwamba alikuwa akihisi uchovu baada ya kutembea hatua chache

“Amekuwa akilalamika kwamba anapumua kwa shida baada ya kutembea mwendo mfupi,” mwanawe akasema akiongeza kuwa babake hakuwa anaugua.

Marehemu ambaye majina yake kamili ni Charles Wanyoike Rubia, ndiye Mwafrika wa kwanza kushikilia wadhifa wa Meya Nairobi mnamo 1963.

Baadaye mnamo 1969 Rubia aliwania kiti cha ubunge wa Starehe, Nairobi na kushinda. Alihudumu kama mbunge hadi mwaka wa 1988, chini ya utawala wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Rais Mstaafu Daniel Moi.

Mnamo 1990, alishirikiana na Kenneth Matiba kupigania kurejelewa kwa demokrasia ya vyama vingi nchini.