Makala

MWANASIASA NGANGARI: Alibahatika kuwahudumia Mzee Kenyatta na Rais mstaafu Moi

December 29th, 2019 4 min read

Na KEYB

NDIYE mwanamke wa kipekee ambaye aliwahi kuhudumia Rais wa kwanza nchini Hayati Mzee Jomo Kenyatta kama Katibu wake wa Masuala ya Kijamii kwa miaka yote aliyohudumu kama Waziri Mkuu na Rais wa Kenya.

Ajabu ni kwamba Bi Elizabeth Madoka hakutuma maombi ya kazi hiyo iliyotamaniwa na wengi. Kazi yenyewe ndiyo ilimfuata.

Isitoshe, alihudumu katika wadhifa huo huo hata chini ya Rais mstaafu Daniel Moi, aliyemrithi Mzee Kenyatta, hadi mwanamke huyo alipostaafu.

Je, Elizabeth aliwezaje kujulikana na Mzee Kenyatta kiasi cha kuweza kumwajiri kazi ya ukarani.

Kenyatta alipenda kumtembelea babake Elizabeth akiwa njiani akielekea katika Chuo cha Walimu cha Githunguri.

Anaeleza hivi: “Babangu alikuwa akifanya kazi ya kupanda miche ya miti na maua kwa ajili ya kuu. Alikuwa na orodha ndefu ya wateja, wakiwemo walowezi wa Kizungu. Sikumbuki Kenyatta kama mmoja wa wateja hao lakini kama rafiki wa babangu ambaye angemtembelea kila wakati kumjulia hali kabla ya kuelekea Githunguri.”

“Nilizuzuliwa na fimbo ya Kenyatta ambayo alipenda kuacha mlango kabla ya kuingia nyumbani kuchapa gumzo na babangu. Nilicheza na fimbo hiyo huku wakiongea. Lakini wakati huo, Rais mtarajiwa hakuonyesha kuvutiwa na sifa zozote nilizokuwa nazo. Nilisalia tu kuwa mtoto nyumbani kwa rafikiye.”

Lakini hivyo ndivyo Kenyatta aliweza kumjua Elizabeth.

Kufanya kazi benki

Mumbi, kama alivyojulikana nyakati hizo akiwa msichana, alisomea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Alliance, wakati huo ikijulikana kama African Girls High School ambako alisoma pamoja na mpwawe Kenyatta, Beth Mugo.

Baadaye aliajiriwa katika Benki ya Baclays jijini Nairobi.

Ni alipokuwa akifanya kazi katika benki hiyo ambapo nyota yake ilianza kung’aa. Katika usiku wa mkesha uhuru mnamo 1963, gazeti la Daily Nation liliandaa mashindano ya urembo ambapo mshindi angetawazwa kuwa “Miss Uhuru”. Wasichana wa Kiafrika waliruhusiwa kushiriki mashindano hayo.

“Sikufahamu kuwa kuliandaliwa mashindano ya urembo, na hata sikuvutiwa na shughuli kama hiyo” Mumbi anakumbuka kwa kicheko.

“Ni mwenzangu mmoja kazini aliyenijuza kuhusu shindano hilo la urembo. Nikatuma picha yangu. Baadaye “Nation” ilinialika niungane na wasichana wengine katika shindano hilo lililofanyika mnamo Desemba 14, 1963- siku mbili baada ya Kenya kupata uhuru.

“Sherehe hiyo ilifanyika katika katika uwanja wa michezo wa City na kuhudhuriwa na watu wengi. Rais Kenyatta aliwasili akiwa amendamana na Mama Ngina, ambaye wajibu wake ulikuwa ni kumtuza mshindi kama “Miss Uhuru” (Bi Uhuru)” Bi Mumbi akasema.

Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na wanasiasa wengi wakuu nyakati hizo

“Kulikuwa na msisimko mkubwa. Na mwishowe, tukio ambalo halikuweza kuaminika lilitokea. Nilipewa taji la Miss Uhuru! Mama Ngina aliweka taji hilo kichwani mwangu na nikapandwa na furaha isiyo na kifani. Sehemu ya zawadi ya taji hilo ilikuwa ni ziara ghali iliyolipiwa nchini Japan. Na baada ya ziara hiyo nilirejelea kazi yangu katika Benki ya Barclays.

Vile vile, kama sehemu ya sherehe hizo za kuadhimisha uhuru, Gavana aliandaa karamu katika mkahawa wa New Stanley. Mshindi wa taji la Miss Uhuru alikuwa miongoni mwa walioalikwa sio na mwingine ila Gavana McDonald mwenyewe.

Simu

Bi Mumbi alishangaa kwamba karamu hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wakati Mzee Kenyatta na mawaziri. Alipokuwa akitangamana na wageni waalikwa, Mumbi alipatwa na msukumo wa kumfikia Waziri Mkuu, ambaye alitangamana naye mwisho akiwa mtoto katika nyumba ya babake.

Mumbi alitumia nafasi hiyo kuelezea haja yake ya kutaka kufanya kazi katika afisi ya Kenyatta. Siku moja baada ya kurejea kazini mwanamume mmoja alipiga simu katika benki akitaka kuongea na Elizabeth Mumbi. Simu hiyo ilishikwa na meneja wa cheo cha juu katika benki hiyo ambaye alimwambia aliyepiga simu kwamba Mumbi alikuwa na shughuli nyingi na hangejibu simu hiyo.

Mwanamume huyo alipiga simu kwa mara nyingine. Na meneja huyo huyo akamkumbusha tena kuwa Mumbi alikuwa amebanwa na shughuli. Na kabla ya meneja huyo kukata simu, mwanaume huyo alimuuliza hivi: “Unajua ni nani anapiga simu?” Meneja huyo hakujua wala kutaka kujua.

“Huyu ni Waziri Mkuu wa Kenya,” Kenyatta alijitambulisha. “Naweza kuongea naye?” Nusra meneja azirai. Aliomba msamaha na kumpa simu Mumbi na ndipo Kenyatta akamwambia aje amwone afisini mwake katika jumba la Harambee.

Katika jumba la Harambee, Kenyatta alimfanyia mahojiano Bi Mumbi lakini akaanza kwa swali: “Je, unafahamu familia kiasi gani?” Mumbi alirejea yale yote aliyomweleza Kenyatta alipokutana naye katika mkahawa wa New Stanley.

Baada ya dakika chache Kenyatta alimwita Bw Dancan Ndegwa, Mkuu mpya wa Utumishi wa Umma na Katiba wa Baraza la Mawaziri, na kumjulisha kwamba amempata mtu ambaye amekuwa wakimtafuta.

Kenyattaa alimweleza Mumbi kwamba wamekuwa wakimsaka mtu ambaye angeshughulikia masuala yake ya kijamii, katika ngazi ya familia na kibinafsi. Mtu huyo angefanya kazi kwa karibu ka Mama Ngina na kazi yake ingejumuisha kuwatunza watoto wake, akiwemo Rais wa sasa Uhuru Kenyatta.

Baada ya Ndegwa kuridhika na maelezo kuhusu asili ya uhitimu wa Mumbi alimwajiri mara moja kama Katibu wa Masuala ya Kijamii katika afisi ya Waziri Mkuu.

Na mara moja Mumbi alirejea katika Benki ya Barclays na kuomba kujiuzulu, ombi ambalo lilikubaliwa mara moja.

Bi Mumbi aliporipoti kwa mara ya kwanza katika Afisi ya Waziri Mkuu, Kenyatta alimjulisha kwa Bi Trit ambaye alihudumu kama Afisa wa kupokea wageni katika afisi hiyo. Bi Trit alimwelekeza Bi Mumbi kuhusu kazi yake hata baada ya Waziri Mkuu kumpeleka katika Chuo cha Serikali cha Mafunzo ya Masuala ya Usimamizi kusomea kozi ya usimamizi.

Ikulu ya Rais

Desemba 12, 1964, ilipokuwa ikikaribia Kenyatta alimtuma Bi Mumbi katika Ikulu ya Rais ambayo iligeuka kuwa mahala pake pa kazi hadi alipostaafu.

“Nakumbuka kuwa nilishirikiana na maafisa wa Ikulu kuandaa sherehe za kwanza za Jamhuri Dei mnamo 1964. Baada ya hapo Gavana McDonald aliondoka na Waziri Mkuu Kenyatta akawa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya. Alihamisha afisi yake kutoka jumba la Harambee House hadi Ikulu. Lakini afisi pekee, sio makazi.”

Akasema Mumbi: “Kenyatta hakuwahi kulala katika Ikulu ya Nairobi. Alikuwa akisafiri kwenda Gatundu kila jioni kulala huku na kurejea Nairobi asubuhi, isipokuwa akiwa katika ziara nje ya Nairobi.”

Kwa haraka Mumbi aliweza kumwelewa Rais Kenyatta. Kwa mfano, aliweza kufahamu kwamba Mzee Kenyatta alipenda vyakula vya kigeni kwa sababu aliwahi kuishi Uingereza kwa miaka mingi.

Vilevile, Kenyatta hakutaka kusikia dereva wake akilalamika. Kabla ya kuanza kula, ilikuwa ada kwa Rais Kenyatta kuuliza ikiwa dereva wake, kwa jina Njenga, alikwisha kula.

Anasema Mumbi: “Walinzi wa Rais, chini ya Wanyoike Thungu, walihakikisha kuwa Njenga alihudumiwa ipasavyo ili kuhakikisha Kenyatta ameridhika. Lakini sisi sote kama wafanyakazi wake tulihudumiwa kwa usawa.

Mumbi alikutana vipi na mumewe Marsden Madoka?

Mnamo 1966 palitokea nafasi msaidizi (aide de camp) wa Rais Kenyatta. Rais mwenyewe ndiye aliwafanya mahojiano ya watu waliotaka kazi hiyo. Aliwakataa wale wote aliopendekezewa na Jeshi.

“Baadaye mwanamume mmoja kwa jina Marsden Madoka aliwasili. Mzee aliwamfanyia mahojiano akiwa ameandamana na Mkuu wa Sheria Charles Njonjo. Nilikuwa nikisimama nje ya ofisi mahojiano hayo yalipokuwa yakiendelea. Mwishowe mwanamume huyo alitangazwa kuwa mshindi,” anasema Mumbi.

Mumbi na Madoka waliishi nyumba za wafanyakazi ziliko katika Ikulu ya Nairobi.

“Madoka alinifundisha mambo mengi ambayo sikufahamu, kama vile uogeleaji. Vile vile, angenipeleka kuona sinema. Tulishirikiana kwa njia hadi siku moja nikamwendea Mzee na kumwambia ningetaka kuolewa na Bw Madoka,

“Mzee akaniuliza, je, unampenda au unapenda sare zake?” Nilimwambia kuwa nampenda kisha akapongeza uamuzi niliofanya.” akasema Mumbi.

Kenyatta aliwachukulia yeye na Mardoka kama wanawe

Wakati huu Elizabeth Mumbi Madoka hutumia wakati wake mwingi kufanya kazi ya kanisa kaunti za Nairobi na Taita Taveta. Pia amekuwa akifanya kazi ya huduma kwa jamii chini ya Shirika la Kijamii la Tesia Kisanga linalowahudumia mayatima wa wazazi wahanga wa Ukimwi.