Makala

MWANASIASA NGANGARI: John Koech, waziri aliyemshinda Moi akili, akifutwa anateuliwa tena

January 19th, 2020 4 min read

Na KEYB

SIKU moja baada ya hafla ya mahafali katika Chuo Kikuu cha Egerton kilichoko eneo la Njoro, waziri John Koech, alinyemelea msafara wa Rais Daniel arap Moi aliyekuwa akielekea nyumbani kwake kwa ajili ya maakuli ya mchana.

Koech alipofika langoni alikatazwa kuingia.

Waziri huyo alipandwa na ghadhabu na akafululiza hadi katika afisi za shirika la habari la Nation Media Group mjini Nakuru kuandika barua ya kujiuzulu. Barua hiyo ilichapishwa gazetini siku iliyofuatia.

Haijulikani kilichofanyika usiku, lakini ilipofika asubuhi alihutubia wanahabari na kubatilisha ujumbe wa barua aliyokuwa ameandika.

Aliendelea kushikilia wadhifa wake wa uwaziri.

Huo ndio uliokuwa mwanzo wa uhasama baina ya waziri Koech na Rais Moi.

Koech alizaliwa mnamo 1946 kijijini Chepalungu na alisomea katika Shule ya Msingi ya Segemik na baadaye akajiunga na shule ya Upili ya Tenwek.

Baada ya kukamilisha elimu yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda ambapo alisomea Uchumi kiwango cha digrii na kuhitimu mnamo 1972.

Alikuwa mwalimu wa shule ya upili kati ya 1973 na 1975. Baadaye, alipandishwa cheo na kuwa afisa wa elimu kati ya 1976 na 1979.

Awali, alikuwa amejaribu kuwania kiti cha ubunge cha Chepalungu lakini akaibuka wa pili baada ya kubwagwa na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Kimunai arap Soi.

Lakini aliibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika 1979 baada ya Moi kuapishwa kuwa rais kufuatia kifo cha Mzee Jomo Kenyatta.

Kabla ya uchaguzi huo wa 1979, Koech alikuwa amekutana na Rais Moi kwa msaada wa Isaac Salat, ambaye alihudumu kama naibu waziri katika afisi ya rais kwa kipindi kirefu.

Wakati huo Rais Moi alikuwa akitafuta kikosi cha wanasiasa waaminifu ambao angefanya nao kazi kwenye serikali yake.

“Wakati huo, rais alikuwa katika harakati za kuunda serikali yake. Alikuwa akitafuta watu waaminifu ambao wangemsaidia kuendesha serikali. Hapo ndipo alipomwita Koech,” akasema Chepkebit Mibei, mwenyekiti wa Kanu tawi la Kericho kati ya 1988 na 2002.

Mibei alisema Koech ambaye alihudumu kama mbunge wa Chepalungu kati ya 1979 na 1990, aliboresha kiwango cha elimu katika maeneo ya Kericho na Bomet.

Moi alihitaji wanasiasa waaminifu ambao wangemsaidia bungeni kusambaratisha jaribio la kupitisha kura ya kutokuwa na imani naye.

“Alijaza bunge na wandani wake kutoka eneo la Bonde la Ufa kuzima jaribio lolote la kutaka kumng’oa afisini. Wanasiasa kutoka eneo la Kati ndio waliokuwa na njama ya kumwondoa mamlakani Rais Moi,” akasema Mibei.

“Wakati huo ilikuwa lazima kwa wanasiasa wa Bonde la Ufa kupata baraka za Moi kabla ya kuingia bungeni,” akasema.

Mnamo 1983, Moi alitangaza uc haguzi mkuu kwa lengo la kuondoa wabunge waliokuwa wandani wa aliyekuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo. Mibei alisema Koech alichaguliwa bila pingamizi kutokana na uaminifu wake kwa Moi.

“Uaminifu wake kwa Moi ulimfanya kuchaguliwa tena kwa urahisi. Wakati huo mwanasiasa kuchaguliwa kuwa mbunge au diwani alihitaji kuidhinishwa na Moi.”

Baada ya uchaguzi wa 1988, Koech aliteuliwa kuwa waziri wa Ujenzi, wadhifa alioshikilia kwa mwaka mmoja kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Timothy Mibei, mbunge wa Bureti, Kericho mnamo Mei 1989.

Koech alitimuliwa baada ya kutofautiana na Moi na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini kuhusiana na jinsi alivyokuwa akiendesha shughuli katika wizara ya Ujenzi.

“Japo tuliambiwa kwamba alitimuliwa baada ya kutofautiana na rais na uongozi wa chama cha Kanu, wengi walihisi kwamba Koech alipigwa kalamu kwa kukataa kuruhusu baadhi ya watu kutumia wizara yake kwa masilahi ya kibinafsi,” akasema Mibei.

Baada ya kutimuliwa uwaziri, Koech alipoteza hamu ya kuendelea kuunga mkono serikali na chama tawala cha Kanu.

“Alianza kuchukia serikali na kila mahali alipoenda alilalamikia utawala wa Moi. Hatua hiyo ilimghadhabisha Moi na viongozi wa Kanu ambao walimwadhibu,” alisema Mibei.

Uhusiano baina yake na Moi ulizorota na mnamo 1990 alitimuliwa kutoka katika chama cha Kanu ambacho kilikuwa cha pekee wakati huo.

Chama cha Kanu kilidai kuwa Koech alikuwa akiendeleza siasa za mgawanyiko miongoni mwa jamii ya Wakipsigs.

Uchaguzi mdogo ulifanywa na Soi akaibuka mshindi na kuchukua kiti cha Koech.

Mnamo 1992, Koech alisamehewa. Ilipofika Desemba mwaka huo, Koech aliwania tena kiti hicho na kumbwaga Soi.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 1997, Koech aliteuliwa kuwa waziri baada ya Kipkalya Kones kutimuliwa kutoka wadhifa wake wa Waziri katika Afisi ya Rais.

Kones alijuzwa kuhusu kutimuliwa kwake kupitia taarifa ya habari ya saa saba mchana ya redio ya KBC huku akiwa katika shamba la baba mkwe wake katika eneo la Molo.

Dereva wake alimtoroka na kupeleka bendera iliyokuwa katika gari lake katika Kituo cha Polisi cha Molo. Kones alilazimika kutumia matatu hadi Nakuru Mjini.

Koech alipokuwa waziri katika Afisi ya Rais, hakuwa akimtetea Moi ambaye wakati huo alikuwa akikabiliwa na mawimbi makali ya kisiasa kufuatia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.

“Moi alihitaji mwanasiasa machachari ambaye angekabiliana na kusambaa kwa upinzani katika eneo la Bonde la Ufa. Lakini Koech alikuwa mpole na mwanadiplomasia, hivyo hakumfaa Rais Moi,” akaelezea William Kettienya, ambaye alikuwa mwandani wa Koech.

Koech alikuwa kiongozi aliyependa kuendesha mambo yake bila kuingiliwa. Alikuwa akijifanyia maamuzi yake mwenyewe bila kujali ikiwa yangemkera Moi au la.

Upole wake ulimfanya kupendwa na mawaziri wenzake.

Koech alibwagwa na Isaac Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 1997, lakini alidai kuwa kura zake ziliibiwa kutokana na uhasama baina yake na Moi.

Baada ya kupoteza kiti chake, aliteuliwa kuhudumu kama Mwakilishi wa Kenya katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kati ya 1998 na 2000.

Lakini Moi alimtimua kabla ya kukamilisha kipindi chake kutokana na madai kwamba alikuwa mshirika wa karibu wa chama cha Democratic Party (DP) chake Mwai Kibaki.

Moi alimteua Profesa Michael Kipkorir Koech kuchukua wadhifa huo.

Licha ya kuhangaishwa na Moi, Koech anasema kuwa alishauriwa na serikali kabla ya kupeleka mradi wowote katika eneo la Bonde la Ufa.

“Kabla ya serikali kuleta mradi katika ukanda wa Bonde la Ufa, walikuja kutafuta ushauri wangu,” akasema Koech.

Alisikitika kuwa umri wake wa juu ulimkosesha fursa ya kuwa gavana wa kwanza wa Bomet 2013.

Koech alichangia pakubwa katika kuanzishwa kwa Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi Siongiroi.

Katika mahojiano na gazeti moja la humu nchini kabla ya uchaguzi wa 2013, Koech alilalamikia tabia ya wanasiasa kuwahonga wapigakura ili kuwashawishi kuwachagua.

“Jukumu la kiongozi ni kuwezesha watu kujiinua kiuchumi na wala si kuwahonga. Haya mazoea ya kuhonga wapigakura hayafai na hufanya watu kuwa wazembe.