Makala

MWANASIASA NGANGARI: Magugu, mwandani wa Moi aliyeilainisha Wizara ya Afya

January 26th, 2020 4 min read

Na KEYB

ARTHUR Kinyanjui Magugu alipoingia siasa akiwa na umri wa miaka 35, aliwashangaza wengi kwa kumshinda aliyekuwa Mbunge wa Githunguri na mpiganiaji uhuru mashuhuri Waira wa Kamau katika uchaguzi mkuu wa 1969.

Na mnamo 1974 Magugu, ambaye alikuwa mwanawe Chifu Mkuu na mhitimu wa vyuo vikuu vya La Verne na Stockholm, aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Afya katika utawala wa Rais Jomo Kenyatta.

Baadaye alishikilia wadhifa huo katika Waziri ya Fedha mnamo mwaka wa 1976. Huo ndio wakati ambapo baadhi ya viongozi kutoka eneo la Kati mwa Kenya na Ukambani walianzisha kampeni ya kutaka katiba ifanyiwe mabadiliko ili kumzuia Makamu wa Rais, wakati huo, Daniel Arap Moi, achukue urais endapo Kenyatta angefariki.

Hata hivyo, Magugu alijiunga na mrengo wa viongozi waliopinga mipango hiyo wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo. Hii ilimfanya kupendwa zaidi na Moi alipofaulu kuingia mamlakani mnamo 1978 baada ya Mzee Kenyatta kufariki.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 1979 Magugu alimshinda aliyekuwa mwanadiplomasia, na Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Josephat Karanja katika kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Githunguri. Na baada ya uchaguzi huo, Moi akamteua kuwa Waziri wa Afya.

Wakati ambapo Magugu alichukua uongozi wa Wizara ya Afya kulitokea changamoto kubwa iliyosababishwa na kujiuzulu kwa madaktari na wataalamu wengine kutoka huduma ya serikali.

Ziada

Hii ni kutokana na amri ambayo Rais Moi alitoa mnamo Agosti 1979 kwamba madaktari wote wanaohudumia serikali hawakuruhusiwa kufanya kazi za ziada katika katika hospitali za kibinafsi.

Moi alisema kuwa mwenendo wa madaktari katika hospitali za umma kufanya kazi za ziada katika hospitali za kibinafsi ndio ulichangia kushuka kwa viwango vya huduma katika hospitali za umma ambazo mamilioni ya Wakenya hutegemea.

Shughuli za masomo katika kitivo cha mafunzo ya matibabu katika Chuo Kikuu cha Nairobi na vyuo vingine vya mafunzo ya matibabu pia ziliathirika baada ya wakufunzi na wataalamu wengine kugoma.

Mnamo 1980, Magugu aliungama kuwa kufikia wakati huo, jumla ya madaktari 23 walikuwa wamejiondoa kutoka utumishi wa umma. Kujiondoa huko kuliilazimu serikali kuajiri madaktari wanane kutoka India katika jitihada za kujaza pengo la walioondoka.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika hospitali za umma hali iliyowalazimisha Rais Moi na Waziri Magugu kulegeza marufuku walioweka dhidi ya madaktari wa umma kufanya “kazi za kando”. Madaktari waliruhusiwa tu kufanya kazi za kibinafsi nyakati za likizo au mapumziko.

Na mnamo Juni 1980 Magugu alianzisha mpango wa kurekebisha hali katika hospitali za umma kuanzia Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa kutembelea hospitali nyinginezo za umma kote nchini.

Katika KNH alikerwa pale alipopata mirundiko ya dawa ambazo muda wao wa matumizi yameisha. Ndiposa akaahidi kubuni Bodi ya usimamizi kuongoza shughuli za kila siku katika hospitali hiyo. Bodi hiyo pia ingefanya mabadiliko kadha miongoni mwa wasimamizi wa KNH kwa lengo la kuimarisha viwango vya utendakazi.

Magugu alifanya ziara za kushtukia katika taasisi zote za kimatibabu za serikali nchini. Alipigwa na butwa na aliyoyashuhudia katika Ghala Kuu la Dawa na Vifaa vya Kimatibabu ambako alipata tani nyingi za dawa ambazo muda matumizi yameisha.

Alipozuru hospitali ya Mathari, hospitali ya kipekee nchini ya kutibu maradhi ya kiakili, Waziri huyo alikumbana na hali kama hiyo hiyo.

Isitoshe, alikasirika ziadi alipokumbana mirundiko ya mavazi machafu ya wagonjwa kwa sababu ya kile alielezwa kuwa ukosefu wa dizeli katika mtambo wa kuosha nguo.

“Usafi wa mazingira ni muhimu zaidi na inasikitisha kuwa wanaougua maradhi ya kiakili wanachukuliwa kama watu wasio na thamani yoyote,” Magugu akanukuliwa akisema kupitia vyombo vya habari.

Wakati wa ziara hiyo Waziri huyo alitangaza kuwa serikali ilikuwa na mipango ya kuanzisha kitengo cha kutibu maradhi ya kiakili katika hospitali za kimkoa kuzuia msongamano katika hospitali ya Mathari. Msongamano huo ndio ulichangia wagonjwa kuishi katika mazingira machafu.

Kwa kuendeleza ziara zake, za kushtukia, katika taasis za kimatibabu, Magugu alifika katika Hospitali ya Gatundu mnamo Jumatatu Septemba 1980.

Dawa

Na baada ya kushuhudia hali mbayo sawa na ilivyokuwa katika hospitali nyinginezo, aliamuru kwamba taasisi zote za matibabu ya umma zisalimishe dawa zote, zilizoisha muda wa matumizi, kwa Ghala Kuu la Dawa na Vifaa vya Matibabu mwezi huo.

“Siku zijazo hatutarajii kupata dawa zozote ambazo wa matumizi umeisha katika taasisi zetu za matibabu,” Magugu akatangaza.

Katika wiki zilizofuata, Magugu aliendeleza shughuli ya ukaguzi wa taasisi za matibabu huku akiwakaripia Maafisa wa Matibabu katika maeneo ya Loitokitok, Kiambu na Eldoret miongoni mwa sehemu zingine kwa kuhifadhi dawa mbovu. Pia aliwazomea maafisa hao kwa kuzembee kazini hali iliyopelekea baadhi ya wahudumu wa afya kukosa kufika kazini kila mara, kutodumisha usafi, miongoni mwa mienendo mingine

Magugu aliacha kumbukumbu katika Wizara ya Afya alipotoa amri kwa watengenezaji bidhaa za tobacco kuchapisha ilani ya kiafya kwenye paketi za sigara. Vile vile, anakumbukwa kwa kutekeleza marufuku dhidi ya watu kuvuta sigara katika maeneo ya umma.

Magugu aliendelea kuwa mwandani mkubwa wa Rais Moi kiasi kwamba hata baada ya Njonjo, na marafiki zake kukosana na kiongozi huyo wa taifa, alikuwa ni mmoja wa Wakikuyu wachache waliendelea kushikilia nyadhifa zenye ushawishi Serikalini.

Hii ndio maana baada ya uchaguzi mkuu wa mapema wa 1983, Magugu aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, kimsingi, kutokana uaminifu wake kwa Rais Moi.

Alikuwa mfuasi sugu wa Moi kiasi kwamba wakati mmoja aliamuru kutolewa kwa picha za Rais wa kwanza nchini, Mzee Kenyatta, katika afisi za serikali. Hata hivyo, amri hiyo ilibatilishwa baada ya Rais Moi kuingilia kati, japo haikujulikana ni kwani Magugu aliibua wazo hilo.

Baadaye alihudumu kama Waziri wa Uchukuzi. Wizara hiyo ilizongwa na changamoto nyingi kufuatia madai kwamba maafisa wa chama tawala Kanu, na wandani wa Moi, waliitumia kuiba pesa za umma. Magugu vile vile, alimsaidia Moi kuwamaliza kisiasa wanachama wa kundi la Kiambu Mafia, waliokuwa na ushawishi kubwa katika utawala wa Mzee Jomo Kenyatta.