Makala

MWANASIASA NGANGARI: Mpenda amani na mpatanishi wa wanasiasa, viongozi

August 25th, 2019 4 min read

Na THE KENYA YEAR BOOK

MWANASIASA Lawrence George Sagini alitawala siasa za eneo la Gusii kama simba anavyowala wanyama wa mwituni kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Marehemu Sagini aliwania kiti cha uwakilishi eneobunge lililojulikana kama Kisii mnamo 1961 kwa tiketi ya chama cha Kenye African Democratic Union (Kadu).

Mnamo 1962, alikuwa miongoni mwa ujumbe wa wapiganiaji uhuru wa Kenya waliosafiri hadi London Uingereza kuhudhuria Kongamano la kihistoria katika Kituo cha Lancaster.

Kenya ilipata uhuru wa kujitawala mnamo 1963, Sagini akichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Magharibi na kuteuliwa Waziri wa Mali Asili.

Na mnamo 1964, Kenya ilipotawazwa kuwa Jamhuri, mwanasiasa huyo aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Wilaya katika serikali mpya iliyoundwa na Hayati Mzee Jomo Kenyatta kama Rais.

Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka wa 1969 alipopoteza kiti chake cha ubunge kabla ya kuwania tena kiti hicho katika chaguzi zilizofuata.

Sagini anakumbukwa kama mwanasiasa aliyependa kushughulikia masuala ya kitaifa kwa njia ya mazungumzo. Kila mara angeitisha mkutano wa viongozi katika Ukumbi Baraza la Mji wa Kisii kusaka muafaka kuhusu masuala ya kitaifa.

Sagini alitumia mbinu hii hii kushughulikia migawanyiko ya kisiasa iliyoibuka katika ngazi ya kitaifa hali iliyomwezesha kuwaunganisha wananchi nyuma ya serikali ya Kenyatta.

Mwanasiasa huyu alizaliwa mnamo Januari 1, 1926, akiwa mtoto wa kwanza wa Bw Ndemo Kibagendi na Bi Esther Nyanganyi. Babake alikuwa rais wa Mahakama ya Kiafrika ya Kisii (African Tribunal Courts).

Sagini alitoka katika ukoo unaojulikana kama Mwabogonko ulio na mizizi yake kwa kiongozi wa zamani wa kijamii, Nyakundi.

Kiongozi huyo (Nyakundi) pia alikuwa mpiganaji jasiri aliyekabiliana na wanajeshi wa Uingereza waliofika katika eneo la Kisii kuandaa mahala pa kujengwa afisi za utawala wa kikoloni.

Babake alithamini elimu hali iliyomwezesha Sagini kuanza masomo yake ya msingi mnamo 1934 katika shule iliyojulikana kama, Isecha Sector School.

Mnamo 1937, alijiunga na shule ya Kisii Government African School kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Mang’u iliyoko Thika; wakati huo ikijuliakana kama Kabaa Mangu Holy Ghost College.

Shule hiyo ilikuwa ikidhaminiwa na Kanisa Katoliki.

Ni katika shule hiyo ambapo Sagini alibatizwa.

Miongoni mwa wanafunzi aliosoma nao katika shule hiyo ni aliyekuwa Mbunge Andrew Omanga, aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori, Rais mstaafu Mwai Kibaki, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kikatiba Tom Mboya, Lawrence Oguda na Chrisantus Ogari.

Baada ya Mangu, Sagini alijiunga na Chuo cha Mafunzo cha Ualimu (TTC) cha Kagumo, Nyeri.

Na alipohitimu, aliajiriwa kuwa mwalimu kabla ya kupandishwa cheo kuwa mwalimu mkuu na kisha afisa wa elimu aliyehudumu katika maeneo ya Kati na Kusini mwa Nyanza.

Mnamo 1957, aliachana na kazi ya ualimu ili kwenda kusomea shahada ya digrii katika Soshiolojia na Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Allegheny College katika jimbo la Pennsylvania, Amerika. Alihitimu mnamo 1957.

Aliporejea nchini Kenya, Sagini alijiunga tena na taaluma ya ualimu ambapo alihudumu kama Mhadhiri katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Asumbi.

Mnamo 1960, serikali ya mkoloni ilimteua tena kuwa naibu wa afisa wa elimu, cheo alichokishilia hadi 1961. Vilevile, aliwahi kuwa mwanachama wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki katika uliokuwa Mkoa wa Nyanza.

Pamoja na mkewe Mary Nyaboke waliyeoana mnamo 1950, walijaaliwa watoto sita. Waliwasomesha hadi kiwango cha Chuo Kikuu. Isitoshe, Sagini aliwasomesha kaka zake; Paul Mong’are, Francis Mayieka, Salim Ndemo, Prof Francis Abuga, Job Kibagendi na Dkt Bitange Ndemo aliyewahi kuhudumu kama Katibu wa Wizara ya Habari na Mawasiliano katika utawala wa Kibaki.

Kwa sababu alikuwa Mkristo muumini wa Kanisa Katoliki, Sagini alisaidia kujenga Kanisa la Katoliki la Ria ‘Sagini lilipewa jina hilo kwa heshima yake. Vilevile, alisaidia makanisa mengine na miradi ya kijamii hali iliyomfaidi pakubwa katika ulingo wa siasa.

Alama ya Sagini katika siasa ilikuwa ni twiga, kushabihiana na umbo la mwili wake na urefu. Vilevile, alikuwa na ufasaha mkubwa katika lugha za Kiingereza na Ekegusii, sifa iliyomsadia pakubwa katika siasa.

Nyakati za kampeni, alama yake ya sanamu ya twiga iliwekwa kwenye paa la gari lake aina ya Volkswagen. Alama hiyo ilivutia zaidi kiasi cha kupelekea wafuasi wake kumpa jina la “twiga” yaani “Sagini Esirori”.

Alipokabiliwa na umati wa watu waliopinga sera zake wakati wa kampeni akasita na kusema: “Mpigie kura yule ambaye mnamwona kuwa kiongozi bora kati yetu, lakini mnikumbuke pia. Mimi pia ni ndugu yenu Mkisii.”

Na angekutana na umati wa watu wanaompinga kwa kumzomea, angesifu mgombeaji ambaye watu hao wanamtaka. Lakini kabla ya kuondoka jukwaani, Sagini angesema hivi: “Kwa kuwa mimi ni mrefu kwa kimo, mtanashati na mwana wa Kisii, naamini kuwa mtatenga kura zingine ambazo mtanipa. Je, mwataka kumchagua mgombeaji mnayemtaka na kuniacha mimi, rafiki yake bila kura yoyote?” Umati ungejibu kwa sauti: “Hapana!”

Sagini alijiepusha na siasa za makabiliano na alikuwa mfuasi sugu wa Kanu na mwandani wa karibu wa Rais Mzee Jomo Kenyatta. Faraghani alimrejelea Kenyatta kama “Mfalme.” Lakini katika mikutano ya hadhara alimrejelea Rais Kenyatta kama “Otwori.” Na hili ndilo lilikuwa jina la utani la Rais huyu miongoni mwa Wakisii.

Hii ni kwa sababu katika historia ya jamii hiyo Otwori O’Nyangena Ime alikuwa ni kiongozi aliyeanziwa na mpiganiaji shupavu aliyewalemea maadui wa jamii ya Wakisii.

Kwa hivyo, urafiki kati ya Sagini na Rais Kenyatta ulimwezesha kuwasaidia wanasiasa, haswa waliovutiwa na chama cha Jaramogi Oginga Odinga cha Kenyatta na wale waliomchukia Rais huyo kufuatia kuuawa kwa wanasiasa kama Tom Mboya na JM Kariuki.

Sagini alikuwa akimhakikishia Kenyatta kila alipopata nafasi kwamba angewashauri wanasiasa waliojihusisha katika “vitendo vya uasi” kuwa waaminifu kwa serikali yake. Sifa kama hii ilimfurahisha Rais huyo na akaendelea kumwamini Sagini hata zaidi.

Lakini kichinichini, Sagini alikuwa ni mtu wa kudumisha marafiki wake. Wakati mmoja Mboya (waliyesoma naye shuleni Mangu) alipotuhumiwa kupanga kupindua serikali, Sagini aliamua kusalia kuwa rafiki yake, licha ya kushurutishwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Bruce McKenzie kukatiza uhusiano wake na Mboya.

Isitoshe, Sagini hakuwa upande wowote katika vita vilivyoshamiri ndani ya chama cha Kanu na serikalini.

Lakini mnamo 1966, chama hicho kilipopunguza mamlaka ya aliyekuwa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga kwa kuteua manaibu wenyeweviti wa mikoa yote minane, Sagini aliwania kiti cha Nyanza na akashinda.

Hata hivyo, aliendelea kudumisha uhusiano kati yake na Mboya pamoja na Odinga, hata wakati viongozi hao wawili kutoka Nyanza walikuwa mahasidi kisiasa.

Na baada ya Sagini kupoteza kiti chake cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa 1969, Kenyatta hakutana kumwacha kwenye “baridi”. Alitumia mamlaka yake na kuwezesha Sagini kuteuliwa kama Meneja wa kampuni ya kutengeneza magurudumu, Firestone.

Na baada ya miaka miwili Rais alimteuwa Sagini kuwa Mbunge Maalum. Ni wakati alipokuwa akihudumu katika wadhifa huo ambapo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Kusambaza Umeme, Kenya Power and Lighting Company. Lakini alikataa wadhifa huo akisema “siwezi kupokea mshahara bunge na tena kupokea marupurupu kama mwenyekiti wa bodi ya KPLC.”

Hata hivyo, baadaye Sagini aliwahi kushikilia nyadhifa mbalimbali katika mashirika ya serikali haswa alipoondoka katika ulingo wa siasa. Kwa mfano, aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Shirika la Ustawi wa Kilimo (ADC), kampuni ya kutayarisha Mbegu, Kenya Seed Company, Mamlaka wa Ustawi wa Mito ya Tana na Athi (TANRDA) na kampuni ya East Africa Industries.

Hatimaye alifariki kutokana na majeraha aliyopata alipohusika katika ajali ya barabarani mnamo Agosti 1, 1995. Ajali ilitokea pale gari lake lilipogongana na gari jingine kutoka nyuma karibu na soko la Chepseon katika barabara ya Nakuru kwenda Kericho.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke