Makala

MWANASIASA NGANGARI: Msomi aliyeteuliwa na Mzee Kenyatta kutuliza jamii ya Waluo wakati Mboya aliuawa

November 3rd, 2019 3 min read

Na KYEB

DKT Joseph Gordon Odero-Jowi anakumbukwa kwa kutochangia lolote katika ulingo wa siasa.

Alihudumu kama mbunge wa eneo la Ndhiwa kati ya 1969 na 1974 kwa tiketi ya chama cha Kanu.

Wakati huo, eneo la Nyanza lilikuwa kwenye upinzani chini ya chama cha Kenya People’s Union (KPU) kilichoongozwa na Bw Jaramogi Oginga Odinga.

Licha ya kuteuliwa kama waziri na Mzee Jomo Kenyatta, hilo halikumsaidia kujiimarisha kisiasa. Mzee Kenyatta alimteua kama njia ya kuituliza jamii ya Waluo kufuatia mauaji ya kikatili ya mwanasiasa Tom Mboya, aliyehudumu kama Waziri wa Mipango na Masuala ya Maendeleo.

Awali, Dkt Jowi alikuwa amehudumu kama Naibu Waziri wa Fedha na alikuwa akiitetea vikali serikali kila wakati ilipokosolewa na Upinzani.

Kwenye mchango wake kuhusu hoja ya kuiahirisha Bunge mnamo Desemba 22, 1967, alisema: “Nchi imepiga hatua katika nyanja zote na lazima tuushukuru uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta kwa kuleta uthabiti wa kisiasa nchini. Hilo ndilo limeiwezesha serikali yake kuleta maendeleo ya ajabu.”

Hasa, aliisifu serikali kwa kuimarisha utoaji huduma muhimu kama afya, akisema kuwa, isingekuwa ni mchango wa Mzee Kenyatta, Kenya ingechukua mamia ya miaka kufikia hatua hizo.

“Nadhani ni lazima tuipongeze serikali panapofaa kwa kuwapa wananchi matumaini katika nchi yao. Uongozi wake umeifaa nchi pakubwa,” akasema.

Kuhusu Upinzani, alisema: Udanganyifu na propaganda zinazoendelezwa na Upinzani zimeisha!”

Alipoulizwa na mbunge wa Butere Martin Shikuku kuhusu alivyomaanisha, mbunge huyo aliunga mkono kauli yake, akisema kuwa Upinzani ulikuwa ukitumia propaganda kuwapotosha wananchi kuhusu utendakazi wa serikali. Aliwaomba viongozi wa Upinzani kukomesha njama za “kuwagawanya wananchi.”

Hakukuwa na tashwishi yoyote kwamba mwanasiasa huyo alikuwa mwenye uaminifu mkubwa kwa Mzee Jomo Kenyatta.

“Watu kadhaa wamekabiliwa na serikali kwa kuipinga, lakini nasisitiza kuwa Upinzani nchini hauna nafasi yoyote. Ni vigumu kwa chama cha upinzani kupiga hatua yoyote ikiwa watu hawamwamini Rais wao,” alisema,

Bw Jowi aliandikisha historia kama mwanasiasa wa kwanza kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wenye ushindani mkali mnamo 1974 na baadaye kuwaacha wapigakura kwenda kukaa ughaibuni.

Inaelezwa alikasirishwa vikali na hatua ya Mzee Kenyatta kutomteua kama waziri.

Alikuwa katika njia panda: Awafurahishe wapigakura walioegemea upande wa Upinzani ama aiunge mkono serikali iliyolaumiwa kwa mauaji ya Bw Mboya?

Serikali ya Mzee Kenyatta pia ililaumiwa pakubwa kwa kumhangaisha Jaramogi, kupiga marufuku chama chake cha KPU na kuwazuilia wabunge wake kwa tuhuma za kuwa tishio kwa usalama wa kitaifa.

Mwanasiasa mwingine kutoka Nyanza aliyejipata katika njiapanda kama hiyo ni mbunge wa Kasipul-Kabondo Bw Samuel Onyango Ayodo. Alihudumu kama Waziri wa Serikali za Wilaya kati ya 1963 na 1969. Alishindwa ikiwa amuunge mkono Jaramogi ama Mzee Kenyatta.

Mnamo Juni 1963 Dkt Odero-Jowi alishinda ubunge katika eneo la Lambwe (likiitwa Ndhiwa kwa sasa) kwa tiketi ya chama cha Kanu. Alisomea masuala ya uchumi nchini India, ambapo baadaye alihudumu kama mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Masuala ya Leba jijini Kampala, Uganda.

Wakati huo, Kenya ilikuwa ikitumia Katiba iliyopata baada ya Mazungumzo ya Lancaster, nchini Uingereza. Chini ya Katiba hiyo, Kenya ilikuwa na mabunge matata, yakiwemo Bunge la Kitaifa, Seneti na mabunge ya kikanda. Seneti na mabunge ya kikanda yalifutiliwa mbali baadaye kufuatia mageuzi ya kikatiba.

Mnamo 1965, eneobunge la Mbita lilibuniwa upya kutoka eneo la Lambwe. Dkt Jowi alihamia eneobunge la Ndhiwa, huku Seneta Mbeo Onyango akichaguliwa kama mbunge wa Mbita.

Hata hivyo, alipoteza kiti hicho baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa 1969, alipohudumu kama Waziri wa Mipango ya Kitaifa na Maendeleo.

Kwenye uchaguzi huo, jamii ya Waluo ilikosa kuwachagua watu wote waliowania kwa tiketi ya Kanu. Dkt Jowi alishindwa na Bw Matthews Otieno Ogingo kwenye uchaguzi uliokumbwa na utata. Bw Ogingo alihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Bunge la Eneo la Nyanza.

Alienda mahakamani kupinga uchaguzi huo, ambapo aliibuka mshindi kwenye kesi. Hata hivyo, Bw Ogingo alimshinda tena kwa kiwango kikubwa cha kura. Mzee Kenyatta alimteua kama mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN) ambapo alichangia pakubwa katika kuiwezesha Kenya kuwa makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Mazingira (UNEP). Alihudumu kati ya 1972 na 1974.

Alirejea Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1974, ambapo alitwaa tena kiti hicho. Alimshinda Ogingo na wawaniaji wengine saba kwa tiketi ya Kanu. Hata hivyo hakumaliza kipindi chake.

Aliondoka na kujiunga na shirika moja la UN nchini Canada mnamo 1977. Kwa mara nyingine, uchaguzi mdogo uliandaliwa katika eneo hilo. Bw Zablon Olang’ ambaye alikuwa afisa wa polisi wa ngazi za juu aliibuka mshindi.

Baada ya kukaa kwa miongo mitatu bila kuonekana hadharani, Rais Mstaafu Mwai Kibaki alimpa tuzo ya kitaifa (EBS) kwa mchango wake kwa nchi. Alikabidhiwa tuzo hiyo na Bw Raphael Tuju, aliyehudumu kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke