Makala

MWANASIASA NGANGARI: Mzungu wa kwanza kuwa waziri baada ya uhuru

May 25th, 2019 4 min read

Na KEYB

ROY Bruce McKenzie alikuwa waziri wa pekee wa serikali ya ukoloni aliyehifadhi kiti chake Kenya ilipopata uhuru na alishikilia wadhifa huo hadi 1969 alipojiuzulu kwa sababu za kiafya.

Alikuwa Waziri wa Kilimo.

Mwanasiasa huyo mzaliwa wa Afrika Kusini anatambuliwa kwa kuongoza uchumi wa kilimo nchini Kenya wakati ulipokumbwa na hali ngumu huku mashamba yaliyomilikiwa na wazungu yakihamishiwa wamiliki Waafrika na kilimo cha mashamba makubwa kikawa cha mashamba madogo madogo.

Bruce aliyezaliwa 1919 na Roy Douglas McKenzie, alikamilisha masomo yake ya msingi katika Hilton College, shule ya mabweni iliyokuwa Midlands, Kwa Zulu-Natal.

McKenzie, alijiunga na jeshi la angani la Afrika Kusini (SAAF) mnamo 1939 wakati vita vya pili vya Dunia (WW11) vilipoanza na baadaye akapigana katika kikosi cha SAAF kilichotumwa kupigana vita vya Mussolini Afrika.

Kwa kushiriki vita hivyo, alipokea medali mbili- the Distinguished Flying Cross (DFC) na the Distinguished Service Order (DSO).

McKenzie alikuwa mmoja wa wanajeshi waliosimamishwa kazi baada ya vita kuisha 1946.

Alihamia Kenya na kuanza kuishi kwenye shamba la ekari 1,200 huko Solai, Nakuru ambako aliendesha ufugaji. Alilipachika shamba hilo jina Gingalili Farm.

Alifuga ng’ombe wazuri nchini kwa wakati huo na wakulima walowezi kwa miaka mingi walimchagua mwenyekiti wa chama kilichofahamika wakati huo kama Royal Agricultural Society of Kenya, kinachojulikana kwa wakati huu Agricultural Society of Kenya.

Akiwa mmoja wa wakulima wa kikoloni waliofaulu, McKenzie alijiunga na wakulima –wanasiasa wakiwemo Michael Blundell, Ferdinard Cavendish-Bentinck (CB) na Charles Makham, kuongoza siasa za walowezi Kenya. Mnamo 1957, McKenzie aliteuliwa katika Legislative Council (Legco).

Alikuwa katika Government House, Nairobi, wakati waziri wa Uingereza aliyehusika na koloni za nchi hiyo Allan Lennox-Boyd alipoambia Legco kwamba angezindua katiba Kenya ambayo ingedumu kwa miaka kumi.

Lakini McKenzie hakupendelea katiba ambayo ingechukua muda mrefu ambayo masetla wazungu waliotaka faida kutoka uwekezaji wao walipendelea.

Katiba ya Lennox-Boyd, iliyopatia Waafrika nafasi 14, wazungu nafasi 47, Waeshia nafasi 6 na Waarabu nafasi 2 katika Legco ilipata visiki bunge hilo lilipofunguliwa 1958.

Waafrika 14 waliochaguliwa waliondoka Gavana Evelyn Baring alipotangaza kuwa hakungekuwa na mabadiliko zaidi ya kikatiba.

Hii ilisababisha mzozo.

Musa Amalemba alikuwa Mwafrika wa pekee kukubali wadhifa wa uwaziri.

Ilikuwa ni wakati huo wa hasira ambapo Blundell alijiuzulu kama Waziri wa Kilimo, Masuala ya Wanyama na Maji kuunda chama cha New Kenya Party kuendeleza siasa za msimamo wa kadiri alizokumbatia.

Mshirika wake aliyeunga mabadiliko McKenzie alichukua nafasi yake 1959, hatua iliyonuiwa kuhakikishia walowezi kwamba hawakuwa na cha kuogopa.

Juhudi za Blundell mnamo Aprili 1959 za kutaka Waafrika kujiunga na chama chake cha New Kenya Party zilikataliwa na viongozi Waafrika walitaka kuzungumza na serikali kuhusu katiba na hawakutaka iliyozinduliwa na Lennox-Boyd.

McKenzie alijiunga na serikali wakati ambao Harold Mcmillan alichaguliwa Waziri Mkuu wa Uingereza na akatangaza kuwa wimbi la mageuzi lilikuwa likivuma katika koloni.

Zilikuwa pia nyakati ambazo siasa za Kenya zilikuwa zikibadilika: Ian MacLeod alikuwa amechukua nafasi ya Lennox-Boyd kama waziri wa masuala ya Koloni na akatangaza mwisho wa katiba ya Lennox-Boyd.

Kufuatia tangazo hilo, wawakilishi wa Waafrika walisitisha mgomo wao wa kutohudhuria vikao Legco.

McKenzie aliteuliwa waziri wa Kilimo wakati ambao masetla walikuwa wameingiwa na hofu ya kuwepo kwa serikali iliyoongozwa na Waafrika.

Ilikuwa ni kupitia McKenzie ambapo suala tata la ardhi lilitatuliwa. Huko London, wakati wa kongamano la Lancaster Conference, alitakiwa kutunga sera ambayo ingewaridhisha Waafrika na Wazungu.

Kupitia juhudi zake na mazungumzo na MacLeod, sera ya kuuzia waliotaka kununua kwa waliotaka kuuza bila kulazimishwa ilipendekezwa.

Akiwa Waziri wa Kilimo, Mckenzie alikuwa mmoja wa wakulima Wazungu wasiokuwa maarufu kama waliokuwa na misimamo mikali.

Miongoni mwao aliyekuwa Spika wa Legco Ferdinard Cavedish-Bentinck, ambaye aliendesha kampeni kali kutaka Uingereza kufidia wakulima kwa hasara yoyote.

Ni McKenzie aliyekuwa kwa kwanza kufahamisha masetla katika mkutano uliofanyika County Hall, Nairobi, 1960, kwamba serikali ingenunua mashamba makubwa na kuyagawia wakulima Waafrika na Wazungu wawe nyapara. Ukumbi huo ulilipuka kwa kicheko!

Ilikuwa ni kupitia juhudi zake ambapo iliamuliwa Waafrika wapatiwe mashamba katika maeneo ya nyanda za juu yaliyokaliwa na Wazungu.

McKenzie aliungwa mkono na Blundell, aliyechukua nafasi yake katika wizara hiyo. Katika Legco, alionya kuwa kama wakulima wazungu wangeondoka Kenya baada ya mashamba yao kununuliwa ingekuwa vigumu kwa uchumi kukua. Kwa sababu ya hofu hii, MacLeod alikutana na Gichuru na Mboya, mnamo Septemba, 1960.

Baadaye McKenzie alikutana na waziri wa serikali za wilaya Wilfrid Havelock na akawahakikishia wawili hao kwamba wakulima wazungu hawangefukuzwa na kwamba angeshinikiza serikali ya Uingereza kupatia serikali mpya ya Kenya pesa za kuwapa makao Waafrika ambao hawakuwa na ardhi hasa katika maeneo yaliyojulikana kama White Highlands.

McKenzie — na kwa kiwango fulani Havelock — walikuwa wameibuka kama mawaziri waliokuwa na misimamo ya kadiri wakiwakilisha chama cha Blundell cha New Kenya Group.

Kundi hilo lilikuwa karibu na Kanu kuliko watu walivyofikiri. Kuanzia mwanzo, kwa hivyo, McKenzie alikuwa katika kundi lililolenga Kenya ya watu wa ngozi za rangi tofauti.

Mnamo Oktoba 7, 1960, kamati kuu ya European Convention of Associations ilipiga kura kuunga uamuzi wa Cavendish-Bentick na muungano wake wa Kenya Coalition katika uchaguzi hatua iliyonuiwa kuzima chama cha McKenzie cha New Kenya Group. Kufuatia uamuzi huo alianza kuunga Kanu ambacho kilikuwa kimeibuka kama chama maarufu cha Waafrika.

Mara kwa mara McKenzie alikuwa akipeleka vita London na kulaumu muungano wa Kenya Coalition wa Cavendish-Bentick kwa kutaka wazungu wachache wapendelewe na hivyo kusababisha hofu iliyofanya Kenya kukosa pesa.

Akataa kujiunga na serikali

Kanu kiliposhinda uchaguzi wa 1961 lakini kikakataa kuunda serikali hadi Kenyatta aachiliwe, McKenzie pia alikataa kujiunga na serikali ya muungano akidai haingeweza kujali maslahi ya muda mrefu ya wazungu wachache.

Alijiunga na Kanu na kushirikiana na Gichuru na Gavana kwa mwisho Malcolm McDonald. McKenzie alipatia Kanu msaada kilichohitaji kilipokuwa kikipigania nchi iliyoungana na mfumo wake wa kuuza na kununua mashamba bila kushurutishwa.

Alikuwa akipinga mfumo wa utawala wa Majimbo uliopiganiwa na chama cha Kadu na sera za chama hicho kuhusu ardhi. Hivyo ndivyo McKenzie alivyoweza kukabiliana na siasa za mwisho za kikoloni.

Ilikuwa ni McKenzie aliyeshawishi Kanu kukubali katiba ya Majimbo ya 1963 ili kuokoa mazungumzo katika kongamano la Lancaster na kisha kuitupa kikiingia mamlakani.

Mnamo 1963, McKenzie alichaguliwa kama mwanachama maalumu wa Bunge la Wawakilishi na kujiunga na Baraza la kwanza la Mawaziri la Kenyatta na waziri wa kwanza wa Kilimo katika Kenya huru.

McKenzie alikabiliana na shida nyingi katika wizara hiyo.

Alitakiwa kushirikiana na wizara ya Ardhi na Makao kuafikia malengo yake lakini ukosefu wa mifugo ulimaanisha sekta ya maziwa haingestawi ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, aliongeza mashamba ya kahawa ya wakulima wadogo na Waafrika wapya 15,000 walipanda majanichai mwaka wa 1965.

Ni kupitia juhudi zake Kenya ilianza kuuza majanichai kwa wingi nje ya nchi. McKenzie alikufa akitoka shughuli za kibiashara nchini Uganda 1978.

Alikuwa ameenda Uganda kwa ndege kutia sahihi kandarasi ya kibiashara na Rais wa nchi hiyo Idi Amin, ambaye walinzi wake walimsumbua McKenzie, wakihofia angemkaribia Rais.

Alipokuwa akirudi, mshirika wa Amin aliwekea sanamu ya kichwa cha Simba kwenye ndege akidai ilikuwa zawadi kutoka kwa Rais.

Sanamu hiyo ilikuwa bomu lililolipua ndege ya McKenzie aina ya Piper Aztec 23 ikiwa Milima ya Ngong akijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi. Alikuwa na umri wa miaka 59.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke