Makala

MWANASIASA NGANGARI: Ngala alitamba katika siasa za Ukambani

June 29th, 2019 4 min read

Na KENYA YEAR BOOK (KYB)

ELIUD Ngala Mwendwa aliwahi kutawala siasa za iliyokuwa Wilaya ya Kitui (sasa kaunti ya Kitui), kama simba.

Aliteuliwa katika baraza la kwanza la mawaziri katika serikali ya Rais wa kwanza nchini Mzee Jomo Kenyatta ambapo alihudumu katika wizara mbalimbali.

Itakumbukwa kuwa alipohudumu kama Waziri wa Leba, Mwendwa ndiye aliasisi Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) na Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS).

Alizaliwa mnamo mwaka wa 1923 katika kijiji cha Kalia, tarafa ya Matinyani na babake, Mwendwa Kitavi, alikuwa Chifu Mkuu katika enzi ya ukoloni. Ni kakake aliyekuwa Jaji Mkuu wa kwanza Mwafrika nchini marehemu Kitili Mwendwa ambaye ni mumewe waziri wa zamani, Bi Nyiva Mwendwa.

Mwendwa alijiunga na Shule ya Msingi ya Matinyani, ambayo ilifadhiliwa na Kanisa la Africa Inland Church (AIC), mnamo 1935. Baadaye alijiunga na shule ya Kitui School ambako alifanya mtihani wa kitaifa wa Common Entrance Examination (CEE).

“Ni katika Kitui school ambako niliona mzungu kwa mara ya kwanza. Na baada ya kukamilisha masomo yangu katika shule hiyo nilifanya vizuri na kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance mnamo 1943,” alisema alipokuwa akihojiwa wakati mmoja.

Baada ya hapo Mwendwa alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kagumo kusomea kozi ya ualimu. Baada ya kuhitimu mnamo 1947 alitumwa katika Shule ya Msingi ya Kituo School alikosomea zamani. Baada ya muda alihamishwa hadi Shule ya Msingi ya Matinyani DEB ambako alifunza hadi 1957.

Mnamo 1958, Mwendwa aliajiriwa kama Mkufunzi katika Chuo cha Ualimu cha Mutune ambayo nyakati hizi ni Shule ya Upili ya Wasichana ya St Angela’s.

Lakini wakati huo, joto la kisiasa lilianza kupanda nchini kufuatia hatua ya serikali ya ukoloni kutangaza hali ya hatari ili kudhibiti shughuli za wafuasi wa kundi la wapiganiaji uhuru la Mau Mau.

Mwendwa hakuwa katika mstari wa mbele katika vita vya uhuru. Kwa hivyo hakukumbuka visa vyovyote vya mapambano ya ukombozi wa kwanza.

Lakini anasema machifu wengi na polisi katika enzi hizo walikuwa wakatili na waliwakamata watu kiholela na kwa sababu finyu.

Wakati mmoja alipokuwa akihudumu kama mwalimu katika Shule ya Kitui School, anakumbuka kwamba polisi walivamia taasisi hiyo na kujaribu kumkamata kwa tuhuma za kuwaunga mkono wapiganiaji uhuru.

Mwendwa anasema Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo alimtetea na akaonya polisi kwamba kumkamata kungechochea mgomo na fujo shuleni humo. Maafisa hao waliondoka.

Ngala, kama alivyofahamika nyakati hizo, alipiga mbizi kwa mara ya kwanza katika bahari ya siasa mapema mwaka wa 1960, wakati ambapo taifa hili lilikuwa likijiandaa kujinasua kutoka kwa minyororo ya ukoloni.

Mnamo 1961, Ngala alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kitui ya Kati baada ya kuwashinda Bw Nzau Muimi na Fred Mbiti Mati. Baadaye Bw Mati aliandikisha historia kwa kuchaguliwa Spika wa kwanza Mwafrika wa Bunge la Kitaifa.

Juhudi za Ngala za kutaka kuwa kigogo wa siasa katika eneo la Ukambani zilimgonganisha na Bw Paul Ngei. Ngei pia alihudumu kama Waziri katika serikali ya Mzee Kenyatta baada ya kuwekwa kizuizini kwa miaka sita katika eneo la Kapenguria pamoja na wanasiasa wengine watano.

Baada ya miaka kadha Ngala alifaidi kutokana na vita vya maneno kati ya Mzee Kenyatta na Ngei.

Wawili hao ambao walikuwa marafiki na wakafungwa pamoja kule Kapenguria.

Baadaye Ngei na Kenyatta walikosana hali iliyomfanya mbunge huyo wa zamani wa Kangundo, wakati huo, kuunda chama cha Akamba People’s Party (APP), ambacho kilivutia wanasiasa kadha kutoka Ukambani.

Mmoja wao alikuwa Fred Mati. Na hatua yake ya kugura KANU na kujiunga na APP ilimfanya Mzee Kenyatta kumfuta kazi kama Waziri wa Leba na mahala pake kuchukuliwa na Bw Ngala Mwendwa.

Ngala aliendelea kuwa mfuasi mwaminifu wa KANU na Mzee Kenyatta hatua ambayo ilimwezesha kuhudumu kama Waziri katika wizara za Afya, Kawi na Mawasiliano.

Lakini masaibu yake ya kisiasa yalianza mapema mwaka wa 1971, pale alipodinda kuunga mkono hoja ya kumkemea dhidi ya kakake wa kambo, Kitili Mwendwa.

Kitili, pamoja na viongozi wengi, hususan, kutoka Ukambani walikabiliwa na tuhuma za kujaribu kupindua Serikali kwa ushirikiano na maafisa fulani wa kijeshi wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wakati huo Jenerali Joseph Ndolo, aliyekuwa Mkamba.

Tuhuma hizo zilimfanya Mbunge wa Yatta, wakati huo, Gideon Mutiso kuwekwa kizuizini huku Ndolo na Kitili wakilazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao.

Hata hivyo, wawili hao hawakushtakiwa katika mahakama ya kawaida au ile ya kijeshi.

Washauri wa Mzee Kenyatta walifasiri uasi wa Ngala Mwendwa kama hatua yake ya kuunga mkono mapinduzi ya serikali, japo kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Na hapo ndipo nyota yake ya kisiasa ilianza kudidimia.

Wakati mmoja alipigana na mbunge mmoja kutoka Nakuru baada ya wao kulumbana kuhusu tuhuma zilizomkabili Kitili ambaye alikuwa Jaji Mkuu.

“Mbunge huyo alinikemea kwa kutokuwa mwaminifu kwa Serikali. Alikataa kusikiza utetezi wangu kuhusu suala hilo,” Ngala alinukuliwa kusema wakati huo.

Katika uchaguzi mkuu wa 1974, Ngala alishindwa na wakili Daniel Mutinda na akapoteza kiti kama Mbunge wa Kitui ya Kati. Lakini alidai kuwa kushindwa kulipangwa kwa sababu alikuwa mshirika wa Tom Mboya, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi jijini Nairobi mnamo 1969.

Ngala anasema familia ya Mutinda ilikataa kumuunga mkono hata baada ya kumshawishi Charles Njonjo kumsaidia kakake wakili huyo kwa jina John Mutinda kwenye kesi iliyomkabili mahakamani.

Waziri huyo wa zamani pia alikabiliwa na tuhuma kwamba alichangia kusambaratika kwa Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Mutune baada ya fedha ilizotengewa kuelekezwa katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Shanzu, kilichoko mjini Mombasa, eneo la Pwani.

Ngala anasema madai hayo yalibuniwa na kusambazwa na Paul Ngei kwa lengo la kuwakasirisha wapiga kura wake ili wamkatae. Alisema ukweli ni kwamba ni Waziri wa Elimu, wakati huo, Taaita Towett, ndiye alishusha hadhi chuo cha Mutune TTC hadi kuwa shule ya upili.

“Ningewezaje kuunga mkono kushushwa hadhi kwa taasisi ambayo nilihudumu kama mkufunzi,” Ngala akauliza alipohojiwa.

Lakini baadhi ya watu walidai kuwa alipoteza kiti chake cha ubunge kutokana na kauli yake kuhusu utajiri wake.

“Umaskini hauko kwangu kabisa. Mimi sio kama watu wengine waliozaliwa katika familia zilizopo katika lindi la ufukara,” Ngala akanukuliwa kusema.

Lakini alikana madai kuwa alijigamba kuhusu utajiri wake, akitaja madai hayo kama uvumi uliokuwa ukienezwa na mahasidi wake wa kisiasa

Mnamo 1984, baada ya kifo cha Mzee Kenyatta, Ngala alirejea katika utumishi wa umma baada ya Rais mstaafu Daniel Moi kumteua kuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Jiji la Nairobi. Hii ni baada ya Moi kuvunjilia mbali Baraza la Jiji la Nairobi mnamo 1983.

Lakini baadaye Ngala alifutwa kazi kupitia taarifa ya habari katika KBC redio baada kukosana na Rais Moi alipozuru Kitui.

Mahakama ya kutatua mizozo

Kando na Shirika la NYS na Hazina ya NSSF, Ngala pia ndiye aliyeanzisha Mahakama ya kutatua mizozo kati ya waajiri na wafanyakazi alipohudumu kama Waziru wa Leba.

“Hizi ni kesi maalum ambazo hazifai kusikizwa katika mahakama za kawaida, haswa katika hali ambapo Serikali ni mhusika,” Ngala akanukuliwa kusema alipoamuru kuanzishwa kwa mahakama ya Leba.

Mwanasiasa huyo wa zamani alijihusisha na kilimo biashara, haswa upanzi wa miti na aina mbalimbali za matunda. Ngala anamiliki ardhi kubwa katika maeneo ya Maliku, Inyuu na Mbusyani katika kaunti ya Kitui. Pia anamiliki kipande cha ardhi katika eneo la Githurai, kaunti ya Kiambu, karibu na Nairobi.

Yeye na mkewe wa kwanza, Agnes, walijaaliwa watoto wanane.

Mke huyo alifariki mnamo 1960 na akaoa mke mwingine kwa jina Priscilla Kavutha ambaye ana watoto sita. Alijaaliwa wajuu na vitukuu wengi.

Ngala alifariki mnamo Juni 2016.