Makala

MWANASIASA NGANGARI: Omamo: Mtaalamu wa kilimo, siasa

October 13th, 2019 5 min read

Na KEYB

SAWA na jina lake la msimbo, ‘Kaliech’ (linalomaanisha kama Ndovu kwa lugha ya Kijaluo), mchango wa Dkt William Odongo Omamo kwa siasa za Kenya ulikuwa mkubwa.

Alikuwa mmoja wa wanasiasa waliojaliwa ustadi wa kunena waliowahi kuhudumu Kenya.

Alikuwa mwanamune aliyekuwa na kipawa cha ucheshi na angehutubu kwa muda mrefu bila kuwachosha waliomsikiliza.

Wakati mmoja akiwa kwenye kampeni, aliulizwa na wakazi kuwaonyesha alichokuwa amewafanyia. Katika jibu lake aliwaacha wote wakiangua kicheko.

Omamo alikuwa na wake wawili, Joyce Acholla na Anne Audia na watoto 16. Mmoja wa watoto hao, Raychelle, alikuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wanasheria Kenya, alihudumu kama balozi wa Kenya Ufaransa na kwa wakati huu ni waziri wa ulinzi Kenya.

Omamo alikuwa mkulima mkubwa maeneo ya Bondo na Muhoroni na alihudumu kama chansela wa chuo kikuu cha Great Lakes mjini Kisumu.

Kenya ilipopata uhuru, aliteuliwa msimamizi wa kwanza mwafrika wa chuo cha Egerton College ambacho kwa sasa ni chuo kikuu.

Alijiunga na siasa 1969 na kushinda kiti cha eneobunge la Bondo. Kiti hicho kilikuwa kimeshikiliwa na Jaramogi Odinga lakini alitupwa kizuizini kabla ya uchaguzi.

Omamo alizaliwa Februari 27, 1928, huko Bondo katika familia ya watoto wanane, wavulana wawili na wasichana sita. Baba yake alioa wake wengine wanane na kupata watoto wengine.

Alijiunga na shule iliyojulikana kama Maranda Sector School, iliyokuwa umbali wa kilomita tano kutoka nyumbani kwao mwaka wa 1936.

Hivi ndivyo alivyoelezea siku yake ya kwanza shuleni ilivyokuwa: “Nilikuwa nusu uchi, nilikuwa na ngozi ya mbuzi iliyofunika sehemu zangu za siri pekee na makalio.”

Siku iliyofuata, wazazi wake walimtafutia mavazi bora kufuatia kanuni kali za shule zilizoidhinishwa na wakoloni.

Kuanzia siku ya kwanza, walimu wake na wanafunzi wenzake walimtambua kama kiongozi kwa sababu ya ustadi wake wa kuhutubu na uwezo wa kufahamu alichofunzwa.

Wanafunzi wenzake walimtaja kama mwanafunzi aliyekuwa mwerevu ambaye alipenda kuwinda, kupanda miti na maua.

Tofauti na wanafunzi wenzake ambao waliacha shule au kurudia madarasa kwa kukosa karo au kutofanya vyema, alikuwa na mteremko shuleni. Alipata alama za juu katika mitihani ya kitaifa na baadaye akajiunga na shule ya Maseno kwa elimu ya sekondari.

Ni akiwa Maseno ambako alipopenda somo la kilimo. Mwaka wa 1951, Omamo alipata ufadhili kwenda kusomea India. Ni wakati huo alipokutana na Odinga, aliyekuwa miongoni mwa waliowakagua wanafunzi wa Kenya walionufaika na ufadhili wa masomo kutoka serikali ya India.

Alikumbuka wakati huo kwa kusema: “Nilikuwa mmoja wa Wakenya wachache walionufaika na ufadhili wa masomo kutoka India. Nilienda chuo cha Punjab Agriculture College kwa miaka miwili na kisha nikahamia chuo cha Madras Agricultural College, ambapo nilihitimu na digrii ya sayansi ya kilimo mwaka wa 1955.”

Mkenya wa pekee aliyekutana naye India alikuwa Titus Mbathi, ambaye alikuwa Madras Christian College. Mbathi alipanda ngazi katika utumishi wa umma, akawa mwanasiasa na waziri. Alihudumu kama mwenyekiti wa kampuni ya Kenya Generating Company (Kengen).

Aliporudi Kenya, Omamo aliajiriwa kama afisa wa kilimo na kutumwa kufunza katika chuo cha walimu cha Siriba Teachers, mkoa wa Magharibi. Hata hivyo, alijiuzulu baada ya miaka miwili- 1957- na kujiunga na chuo kikuu cha Lahore nchini Pakistan kuendeleza masomo ya uchumi na kilimo.

Alirudi kutoka Pakistan 1959 akiwa na digrii ya uzamili na akatumwa wilaya ya Embu kama naibu afisa wa kilimo.

Mnamo 1960, Omamo alijiuzulu tena na kwenda ng’ambo kwa masomo ya juu. Alienda chuo kikuu cha Oregon State University, Amerika alikosomea digrii ya pili ya uzamili katika kilimo.

Aliporudi nyumbani Machi 1961, Omamo alipandishwa cheo na kutumwa Nyeri akiwa mkuu wa kilimo mkoa wa kati aliyesimamia usoroveya.

Mwaka wa 1962, alihamishwa hadi Homa Bay katika wadhifa huo lakini akaongezewa majukumu ya kusimamia masuala yote ya kilimo katika mkoa wa Nyanza.

Alikumbuka: “Nilisimamia kikamilifu na sijawahi kufanya kazi kwa bidii kama wakati huo katika maisha yangu!” Na ni wakati huo alipopachikwa jina la “Kaliech”.

Kati ya 1963 na 1965, Omamo alinawiri katika taaluma yake. Alihamishiwa Kisumu na kupandishwa cheo kuwa mkuu wa kilimo katika mkoa wote wa Nyanza.

Wakati nafasi ya naibu mwalimu mkuu wa Egerton College Njoro ilipotangazwa kuwa wazi, Omamo alituma maombi.

Alipata kazi hiyo na kuweka historia kuwa mwafrika wa kwanza kushikilia wadhifa huo. Mnamo 1966, alipandishwa cheo kuwa mwalimu mkuu na kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mike Baretti akiwa pia mwafrika wa kwanza kushikilia wadhifa huo. Chuo hicho kilikuwa na wanafunzi 300 wakati huo.

Lakini mnamo 1969, aliacha wadhifa huo kujiunga na siasa. “Niliamini nilikuwa nimeweka mpango wa chuo hicho na kwa hivyo ulikuwa wakati wangu wa kuondoka.” alisema.

Japo alikuwa ameridhika na kazi ya afisa wa serikali na awali hakuwa na mipango ya kujiunga na siasa, alibadilisha nia kwa kile alichotaja kuwa matukio ya kuhuzunisha yaliyoathiri nchi na hasa jamii ya Waluo.

Matukio hayo yalikuwa kifo cha kutatanisha cha C.M.G. Argwings-Kodhek jijini Nairobi, kuuawa kwa waziri wa mipango ya kiuchumi na katibu mkuu wa Kanu Tom Mboya na kupigwa marufuku kwa chama cha Bw Odinga cha KPU.

Omamo alisema: “Nilijiunga na siasa kwa sababu ya kile nilichoona kuwa hatari ya kuwa na pengo katika uongozi wa jamii yetu kufuatia matukio hayo ya kuhuzunisha.”

Wakati alipojiuzulu kutoka Egerton, Omamo alikuwa ameteuliwa mkuu wa kitengo cha rasilmali asilia katika tume ya uchumi ya Afrika yenye makao Addis Ababa.

Alikataa uteuzi huo na kurejea kijiji chao huko Bondo kugombea kiti cha ubunge kufuatia kutupwa kizuizini kwa Odinga na viongozi wengine wa KPU. Alishinda uchaguzi huo na Kenyatta akamteua waziri wa maliasili.

Bunge la pili la Kenya (1969-1974) lilikuwa changamfu hasa kwa viongozi kutoka Nyanza ambao hawakuwa wakiendeana kichinichini.

Omamo alisema kwa sababu ya muungano wao walituma ujumbe kwa Kenyatta kumuomba amwachilie Odinga na viongozi wengine wa KPU waliofungwa pamoja naye.

Lakini wapigakura wa Bondo hawakufurahishwa na Omamo na kwenye uchaguzi mkuu wa 1974 walichagua mshirika wa Odinga, Hezekiah Ougo. Alikubali kushindwa lakini hakuacha kusaidia wapigakura kupitia harambee na miradi mingine ya maendeleo.

Wakati Kenyatta alipomteua Omamo kuwa mwenyekiti wa Kampuni ya Sukari ya Mumias, alipanua shughuli za kampuni ya Mumias Outgrowers Company.

Lakini mwaka mmoja baada ya Omamo kupoteza kiti cha Bondo, Kenyatta alimteua mbunge maalamu bungeni kuchukua nafasi ya Walter Odede, aliyefariki. Kwenye uchaguzi mkuu wa 1979, wapigakura walimkataa Omamo tena na kumchagua Ougo.

Kenyatta alipofariki Agosti 22, 1978 akiwa Mombasa, Omamo alikumbuka kwamba alikuwa akihutubia ujumbe wa mabalozi katika kiwanda cha sukari cha Mumias.

Mkuu wa ujumbe huo alimuita chemba na kumfahamisha kuwa mzee alikuwa amekufa na mkutano ukakatizwa.

Mabalozi hao walikuwa wamekutana na Kenyatta Mombasa ambaye aliagiza kiongozi wao kuwapeleka Mumias kujionea ufanisi wa kiwanda hicho chini ya usimamizi wa Omamo.

Moi alipotwaa hatamu za uongozi, Omamo aliteuliwa mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha Nairobi na baadaye Agricultural Finance Corporation.

Hata hivyo, alijiuzulu 1980 kugombea kiti cha eneobunge la Bondo kwenye uchaguzi mdogo kufuatia kujiuzulu kwa Ougo aliyetaka kumuachia Odinga ambaye alikuwa ameteuliwa mwenyekiti wa Cotton Marketing Board.

Lakini chama cha Kanu, kilichokuwa cha pekee, kilimzuia Odinga kugombea kikisema hakuwa ametosha kuwa mwaminifu kwa Kanu. Hii ilikuwa baada ya kudai Kenyatta alikuwa mnyakuzi wa ardhi.

Omamo alishinda kiti hicho na Moi akamteua waziri wa mazingira na mali asili- hii ilikuwa siku kumi baada ya serikali kuzima jaribio la mapinduzi la Agosti 1.

Kwenye uchaguzi wa ghafla wa 1983, Omamo alishinda kiti hicho na akateuliwa waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo.

Mnamo 1987, alihamishiwa wizara ya Sayansi na Tekinolojia lakini hakudumu kwa muda mrefu katika wadhifa huo.

Wakati mmoja Omamo alidai kuwa mahasimu wake wa kisiasa walimpotosha Moi kwamba alikuwa amemsifu Odinga kwa kufanikisha ufadhili wake kwenda kusoma India kwenye sherehe ya shukrani, chuo alichosomea kilipomtunuku digrii ya uzamifu.

Baadaye Moi alimsamehe baada ya ukweli kubainika kwenye hafla hiyo.

Aligombea kiti cha Bondo 1988 na 1992 na kwenye uchaguzi mdogo wa 1994 lakini hakufaulu.

Mnamo 1997, alihama Kanu na kujiunga na chama cha National Development Party kilichokuwa cha Raila Odinga na akashinda kiti cha eneobunge la Muhoroni, Kisumu.

Alistaafu siasa 2002 akisema alikuwa kama baluni ambayo wakati hufika ikatolewa pumzi. Alikufa Aprili 27 2010 akiwa na umri wa miaka 82.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke