Makala

MWANASIASA NGANGARI: Waziri aliyekuwa na uaminifu wa kipekee kwa Jomo

December 8th, 2019 4 min read

Na KEYB

MATHEWS Joseph Ogutu alikuwa Waziri wa Utalii na Wanyamapori katika baraza la mawaziri la mwisho la Rais Jomo Kenyatta.

Ogutu alizaliwa katika kijiji cha Uyundo, Sega wilayani Siaya mwaka wa 1931 kwenye ukoo mkubwa wa Punyi unaoishi eneo la Ugenya.

Kumbukumbu kuhusu kijiji hicho zilififia na wakati hivi kwamba ni wachache wanaoweza kukumbuka tarehe halisi ambayo Mathews Joseph Ogutu alizaliwa

Ogutu alikuwa mvulana wa kawaida katika familia ya kawaida ambayo kiongozi wake Julius Oduor, baadaye aliteuliwa naibu wa chifu.

Hata alipotembea kwenda shule ya msingi ya Uyundo na baadaye shule ya sekondari ya Kasese, Uganda, ulimwengu ulipokuwa ukijiandaa kwa vita vya pili vya dunia, Ogutu hakufahamu kuwa angekuwa mashuhuri.

Ingawa kuna madai kwamba Ogutu alihudhuria shule ya St Mary’s, Yala, shule ya upili ambayo ilitoa watu mashuhuri eneo la Nyanza, mwanakijiji mwenzake, James Meso, ambaye alikuwa diwani wa Ugenya Magharibi, hakuweza kukumbuka.

Meso alimfahamu Ogutu binafsi na anakumbuka kuwa punde tu baada ya Ogutu kuondoka shule ya msingi ya Uyundo, alienda Uganda kuendelea na masomo ilivyokuwa ikifanyika wakati huo.

Hii inaweza kuwa sababu ya wakazi kukosa kufahamu mengi kuhusu maisha ya Ogutu katika ujana wake.

Baada ya kumaliza masomo, Ogutu alirudi Kenya na kuwa mwanakandarasi wa ujenzi maeneo tofauti ya Ugenya.

‘‘Baada ya kufanya kazi kama mwanakandarasi kwa miaka kadhaa, akijengea watu nyumba,” akumbuka Meso.

Ogutu alipata kazi kama mhandisi katika kampuni ya Uingereza Mowlem Construction Company na akatumwa kufanya kazi Uganda.

Ogutu alifanya kazi kama mhandisi katika migodi ya Kilembe nchini Uganda, hatua iliyoimarisha hadhi yake katika jamii nyumbani kwao Ugenya hasa baada ya kuoa mke wake wa kwanza, Josephine.

Akiwa mwanamume ambaye hakufanya mambo yake nusunusu, ‘woud lando’ (mwana wa mwanamke mweupe) Ogutu alivyofahamika, alifanya makuu kwa kujenga nyumba ya vyumba vitano mnamo 1964, katika kijiji cha Uyundo, na kumfanya awe gumzo la majirani.

Mnamo 1996 akihojiwa na gazeti la Daily Nation, Ogutu alisema alijenga nyumba hiyo kama sehemu ya kujiandaa kustaafu.

Hii ilikuwa kasri iliyovutia Ugenya kwa sababu ilikuwa ikikarabatiwa kila baada ya miaka mitatu na mwanamume ambaye wengi walimchukulia kuwa mwenye kiburi.

Ziara zake katika boma lake mashambani ziliongezeka Mowlem ilipohamishwa hadi Nairobi, na kumpatia nafasi ya kuimairisha ngome yake ya kisiasa.

Tofauti kati ya Rais Jomo Kenyatta na naibu wake Jaramogi Oginga Odinga mwaka wa 1969, zilimfungulia Ogutu mlango wa kujaribu bahati yake katika siasa za uchaguzi.

Mwaka huo, Ogutu alijiuzulu kama mhandisi katika kampuni ya Mowlem, kujiunga na siasa. Aligombea kiti cha eneobunge la Ugenya mkoa wa Nyanza. Haikuwa rahisi kwake kwa sababu ni mwaka huo ambao chama cha pekee cha upinzani, KPU cha Odinga, kilipigwa marufuku na viongozi wake kuzuiwa.

Viongozi wa KPU, wengi wao kutoka Nyanza, walikamatwa na kuzuiliwa kufuatia makabiliano kati ya viongozi wa Kanu na KPU mjini Kisumu.

Ogutu wa Ugenya, William Odongo Omamo wa Bondo (lililokuwa eneobunge la Odinga) walijaza pengo la kisiasa lilililoachwa wazi.

Kenyatta alimteua Ogutu waziri msaidizi katika wizara ya serikali za wilaya. Alihudumu kwa miaka mitano kabla ya kupandishwa cheo kuwa waziri wa Utalii na Wanyamapori. Ogutu aliunga serikali kikamilifu.Michango yake bungeni ilidhihirisha alikuwa mwaminifu kabisa. Akichangia mjadala kuhusu hotuba ya rais ya kufungua bunge mnamo Februari 6, 1970, alisema: “Bw Naibu Spika, ninaungana na waheshimiwa wenzangu kumshukuru Mtukufu Rais kwa maelezo yake kuhusu sera ya umma alipohutubia bunge hili.

“Ningetaka kuzungumzia kidogo kuhusu sekta ya utalii. Tunakaribisha tamko la rais katika hotuba yake kuhusu kupanuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kisumu. Tunaomba serikali kuharakisha upanuzi huo na kuhusisha mji wa Kisumu na maeneo mengine ya Nyanza katika soko la kitalii ili tuweze kunufaika kwa utalii kama maeneo mengine ya nchi hii.

“Kuhusu barabara, Bw Naibu Spika, tunafurahishwa na maandalizi yanayofanywa ya kuweka lami barabara ya Yala kwenda Busia. Barabara hii inapitia inapitia eneo lililo na watu wengi na inatumiwa na magari makubwa. Tunaomba serikali iimarishe kiwango cha barabara hii.”

Akichangia kuhusu mpango wa kuwapa Wakenya ajira, Ogutu akisema mengi yalihitajika kufanywa ili uweze kufaulu. Waziri huyo msaidizi alisema: “Tuko na vijana na wasichana wengi waliomaliza shule ambao hawana kazi. Ninaamini kwamba mpango huu ulivyo kwa sasa unatumiwa kusajili wanaotafuta kazi na sifikirii serikali inafanya ya kutosha.”

Alifurahishwa na mpango wa rais wa kuanzisha kodi ya viwanda akisema italeta enzi mpya ya kutoa mafunzo ya lazima na ushirikiano wa serikali ambao ungetoa mafunzo.

Alisema kodi hiyo iliyopendekezwa ingebadilisha mfumo wa kutoa mafunzo. Alipendekeza kuwa kampuni na viwanda zipokonywe utoaji wa mafunzo na liwe jukumu la ushirikiano kati ya serikali na viwanda huku kila kampuni ikilazimishwa kulipia mafunzo hayo.

Kwa hakika, mojawapo ya mafanikio makubwa yakiwa katika wizara ya Utalii ilikuwa ni kushawishi serikali kwamba Kenya ilinufaika pakubwa kwa kuchoma pembe za ndovu.

Kenyatta alitoa tangazo hilo sikukuu ya Madaraka Dei mwaka wa 1977 na kuagiza litekelezwe katika muda wa miezi mitatu.

Mnamo 1996, waziri huyo wa zamani alisema alijivunia kuhudumia Kenya na Kenyatta kwa uaminifu na kwa uwezo wake wote.

“Ninaamini nilitimiza matarajio ya wapigakura wa Ugenya na Mzee Mzee Kenyatta. Hautegemei wapigakura kuishi, wanakudai huduma wakikuchagua,” alisema na kuongeza kuwa utumishi wa umma ni jukumu na sio kujitajirisha.

Akichangia hotuba ya bajeti mwaka wa 1971 iliyowasilishwa na waziri wa fedha Mwai Kibaki, Ogutu alisema ilikuwa nzuri na iliyoshughulikia kodi.

Alisema: “ Mimi ninaamini katika ukuaji wa uchumi wa Kenya. Hapa Kenya, tunafahamika kwa kutegemea kilimo. Kinachosikitisha ni kuwa hatujashughulikia uchumi wetu wa kilimo,” alisema.

Alikumbuka kuwa mnamo 1970, Wakenya walilazimika kula mahindi ya majano na uhaba mwingine wa mahindi ulitarajiwa 1971. Alisema wateja waliruhusiwa kununua pakiti mbili pekee za unga madukani.

Ogutu aliwahimiza wenzake kupanga uchumi wa kilimo iwapo nchi hii ingejitosheleza kwa chakula.

Kwa ufupi, Ogutu alilaumu ukoloni kwa uhaba wa chakula akitoa mfano wa sera ya serikali iliyoruhusu mazao ya kibiashara katika mkoa wa Rift Valley na sehemu za mkoa wa Kati.

Na kuhusu hali mbaya ya barabara za humu nchini, Ogutu alilaumu wahandisi wa kigeni kwa kutofahamu hali ya hewa ya humu nchini.

Nyota ya kisiasa ya Ogutu ilianza kufifia Juni 30, 1980, Mahakama Kuu ilipobatilisha ushindi wake kama mbunge wa Ugenya kufuatia kesi iliyowasilishwa na mpinzani wake Askofu Mkuu Stephen Ondiek.

Kwa Ogutu, hiyo ilikuwa siku ya huzuni zaidi katika maisha yake ya kisiasa majaji walipoagiza spika wa bunge la kitaifa kutangaza kiti chake kuwa wazi na kuitisha uchaguzi mdogo.

Kwenye uchaguzi mdogo, Ondieki alimshinda Ogutu kwa kura nyingi. Na huo ulikuwa mwisho wa maisha yake ya kisiasa.

Baada ya kifo cha Kenyatta, Moi alimteua Ogutu mwenyekiti wa bodi ya Pamba kuchukua nafasi ya Odinga. Hata hivyo, hakukaa sana- alijiuzulu 1983 kugombea kiti cha eneobunge la Ugenya lakini akashindwa na wakili James Orengo ambaye alikuwa amehitimu kutoka chuo kikuu cha Nairobi.

Ogutu alisema alifurahia na kuridhishwa na siku zake akiwa waziri kwa sababu Kenyatta aliwapatia mawaziri uhuru wa kutumia maarifa yao kikamilifu. Alimsifu sana Kenyatta: “Kenyatta alikuwa mwanzilishi wa taifa na alifahamu siasa na alituunganisha. Kila wakati tulishirikiana katika baraza la mawaziri. Alikuwa kiongozi mkakamavu niliyewahi kukutana naye. Pia alitufunza kuwa jamii moja na nchi moja.”

Ogutu alikuwa na wake wanne na watoto 14.

Alifariki Oktoba 4, 1997, akiwa na umri wa miaka 66.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook

Editorial Board; kenyayearbook.co.ke