Makala

MWANASIASA NGANGARI: Waziri aliyewatimua wafanyabiashara wa Kihindi mashambani

November 10th, 2019 5 min read

Na KYEB

ELIUD Timothy Mwamunga alikuwa mwanasiasa mtajika kutoka Pwani kabla na baada ya Kenya kupata uhuru ambaye pia alihudumu kwa miaka mingi kama Mbunge na Waziri.

Aliwahi kushikilia nyadhifa kadha za uwaziri katika serikali za Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Rais mstaafu Daniel Moi.

Baadaye mapema miaka ya 1990 Bw Mwamunga alishirikiana na Rais mstaafu Mwai Kibaki kuunda chama cha kisiasa cha Democratic Party (DP) ambacho kilimwandaa Kibaki kuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya.

Katika eneo linalojulikana kama kaunti ya Taita Taveta kwa ujumla Bw Mwamunga ndiye anashikilia rekodi ya mwanasiasa aliyewahi kuhudumu kama mbunge kwa miaka 20 mfululizo. Hamna wanaasiasa waliomtangulia au wale walichipuka baada yake waliwahi kuhudumu kama wabunge kwa mihula miwili.

Wanasiasa hao ni Basil Mwakiringo, Darius Mbela, Boniface Mganga na Adiel Kachila.

Weledi wa Bw Mwamunga katika ulingo wa siasa ulimwezesha kunawiri katika serikali za Kenyatta na Moi nyakati ambapo wanasiasa waliokuwa wakiendeleza siasa za makabiliano walizimwa kwa kutupwa gerezani, kupokonywa nyadhifa zao za uwaziri au kuondolewa bungeni kupitia wizi wa kura.

Yamkini, ni sifa hiyo iliyomwezesha kunawiri kuliko wanasiasa wengine katika eneo la Taita na Pwani kwa ujumla. Kando hayo Bw Mwamunga alikuwa tajiri aliyemiliki vipande kadhaa vya ardhi katika Taita Taveta yenye mali asili kama vile madini, mimea ya kuuzwa (kama vile mkonge) na wanyamapori.

Mwamunga alizaliwa mnamo Julai 21, 1935 katika kijiji cha Ishamba kando la Milima ya Taita. Alilelewa katika eneo hilo ambalo lina utajiri mkubwa wa mali asili, kama vile madini ya ruby, mimea ya mikonge, matunda (maembe) na wanyamapori kwa sababu Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo iko karibu.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Ishamba, kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Shimo la Tewa kwa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne. Baadaye aliitwa katika Shule ya Upili ya Alliance kusome kiwango cha A’ level (vidato vya tano na sita).

Aliendelea na elimu ya juu katika chuo kikuu cha Makerere kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salam ambako alisomea shahada ya Uanasheria.

Baada ya kuhitimu kwa shahada ya Uanasheria, Mwamunga alifanyakazi kama mwalimu nyakati za enzi ya mapambano ya ukombozi wa uhuru hadi mwaka wa 1952 wakati hali hatari ilitangazwa nchini. Ni wakati huo ambapo wanasiasa walianza kuunda vyama vya kisiasa kwa ajili ya kupigania uchumi.

Baadaye aliachana na kazi ya ualimu na kuajiriwa kama Karani katika Baraza la Miji la Taita Taveta. Katika wadhifa huo, Bw Mwamunga alitangamana na madiwani pamoja na wabunge. Vilevile, alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali katika Taita Taveta ambapo alipata nafasi ya kung’amua kuwa watu wa eneo hilo walikuwa na mahitaji na shida nyingi. Ndipo akajitwika wajibu wa kutoa mchango wake katika juhudi za kushughulikia changamoto zao.

Mnamo 1969, Bw Mwamunga, akiwa na umri wa miaka 34, alijitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti iliyokuwa eneobunge la Taita Taveta. Alisema kuwa alipata hamasa kutoka kwa aliyekuwa mpiganiaji uhuru kutoka Pwani, Ronald Ngala ambaye alikuwa mstari wa mbele kupambana dhidi ya unyanyasaji wa watu wa pwani.

Baada ya kushinda kiti cha ubunge, Mwamunga alitekeleza miradi kadhaa ya maendeleo, alijenga urafiki na wataalamu wa kilimo, wahifadhi wa wanyamapori, wachimba madini wa asili ya Kenya na mataifa ya kigeni ambao walichimba rasilimali katika wilaya hiyo.

Vilevile, Bw Mwamunga alijenga uhusiano wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa. Mkakati huu ulimfaidi kwani ulimwezesha kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa 1974.

Ni baada ya kushinda kiti cha ubunge kwa mara ya pili ambapo Hayati Mzee Jomo Kenyatta alimteua katika baraza lake la mawaziri kuwa Waziri wa Ustawi wa Maji.

Katika kipindi cha miaka miwili alipohudumu katika wizara hiyo Mwamunga alianzisha miradi kadhaa katika iliyokuwa Wilaya ya Taita Taveta. Miongoni mwa miradi hiyo ilikuwa uchimbaji mabwawa, usambazaji wa maji katika maeneo ya miji na miradi ya unyunyiziaji mashamba maji kupiga jeki sekta ya kilimo.

Kwa sababu kilimo kilikuwa (na kingali) nguzo kuu ya uchumi wa Kenya, Wizara ya Maji ilikuwa muhimu katika kuisaidia serikali kuanzisha miradi ya unyunyiziaji mashambaji kukuza chakula kulisha watu wake na kuuza katika mataifa ya ng’ambo.

Mnamo 1976, Rais Kenyatta alimhamisha Bw Mwamunga hadi Wizara ya Biashara na Viwanda na nafasi yake ikapewa Dkt Gikonyo Kiano,

Katika Wizara hii mpya Mwamunga alisaidia katika utayarishaji wa sera nyingi ambazo ziliunda mazingira mazuri kwa watu kutoka ng’ambo kuwekeza nchini katika nyanja ya biashara na viwanda.

Na huku akifuata nyayo za Makamu wa Rais na Waziri wa Masauala ya Ndani wakati huo Daniel Moi na Kiano (aliyekuwa waziri wa Biashara na Viwanda), Mwamunga aliendesha sera ya kuhakikisha kuwa biashara za humu nchini zinamilikiwa na kuendeshwa na wenyeji.

Hii ni kwa sababu sekta hiyo ilitawaliwa na Wazungu pamoja na Wahindi ambao walipiga kambi jijini Nairobi na miji mingine mikubwa nchini, huku wanyabiashara wa asili ya Kenya wakikoosa nafasi ya kunawiri.

Kupitia uungwaji mkono kutoka kwa Rais Kenyatta, Mwamunga alitoa ilani kwa Wahindi waliokuwa wakiendesha biashara katika maeneo ya mashambani kuhama. Walitakiwa kujikita jijini Nairobi na miji mingine mikuu nchini.

Baadaye serikali kupitia Shirika la Ustawi wa Kibiashara na Kiviwanda (ICDC) ilitoa mikopo kwa wenye kusudi waweze kuanzisha biashara katika maeneo ya mashambani ili kujaza nafasi zilizosalia baada ya Wahindi kuondoka.

Ni katika mwaka huo, 1976, ambapo Kenya ilitunukiwa nafasi ya kuandaa Kikao cha Nne (4) cha Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) lililofunguliwa rasmi na Rais Kenyatta.

Kongamano hilo lilikuwa la kwanza la aina yake kuandaliwa barani Afrika na lilihudhuriwa na viongozi wa viwango vya kimataifa kama vile aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Henry Kissinger, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Kurt Waldheim na Rais wa Ufilipino nyakati hizo Ferdinand Marcos.

Katika hotuba yake, Mwamunga alitoa wito kwa mataifa ya ulimwengu kutatua mizozo ya kibiashara, haswa kati ya mataifa tajiri na masikini. Alipendekeza kuanzishwa kwa mikataba ya kuongoza utoaji wa mikopo na mashirika ya kimataifa ya kifedha na uimarishaji wa bei ya bidhaa kutoka mataifa masikini katika masoko ya kimataifa.

Mawimbi ya kisiasa yalianza kumgonga Mwamunga mwishoni mwa 1977 wakati wa uchaguzi wa iliyokuwa chama tawala, Kanu. Alitofautiana na Katibu Mkuu wa chama hicho wakati huo Robert Matano alipokuwa akisimamia uchaguzi wa tawi la Mombasa ambapo John Mambo alichaguliwa kama mwenyekiti. Alikatalia mbali ushauri wa Matano kwamba uchaguzi huo urudiwe kutokana na udanganyifu uliogunduliwa.

Lakini hatimaye alisalimu amri baada ya msajili wa vyama vya kisiasa kuingilia kati na uchaguzi mwingine ukafanyika ambapo marehemu Shariff Nassir alichaguliwa. Hatimaye, Nassir aligeuka kwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa mkubwa zaidi katika eneo la zima la pwani katika enzi ya utawala wa Mzee Moi.

Lakini licha ya Mwamunga kukosana Katibu Mkuu wa Kanu, alifaulu kuhifadhi kiti chake cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa 1979 baada ya eneobunge hilo kubadilishwa jina na kuitwa, Voi. Katika uchaguzi huo, wa kwanza baada ya kifo cha Kenyatta, Mwamunga alizoa kura 8, 364 na kumshinda mpinzani wake wa karibu Kwaya Mwatibo aliyepata kura 2,699 pekee.

Na baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali ya Rais Moi mnamo 1982, Bw Mwamunga kwa mara nyingine alielekezewa lawama kwamba alikuwa mmoja wa wanasiasa walioegemea kambi ya aliyekuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo aliyedaiwa kupanga mapinduzi hayo. Alipinga madai hayo.

Wakati huo alikuwa akihudumu kama Waziri wa Habari na Utangazaji. Masaibu ya Mwamunga yaliendelea kutokota hadi mwaka wa 1988 alipopokonywa cheo cha uwaziri miezi michache kabla ya uchaguzi wa mwaka huo. Hatimaye alishindwa na Darius Mbela katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Voi. Baadaye Mbela aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi.

Hatimaye mnamo Januari 1992 Mwamunga alishirikiana na Kibaki kuunda chama cha DP baada ya Katiba kufanyiwa mabadiliko kurejesha utawala wa vyama vingi mnamo Desemba 1991. Mwamunga aliteuliwa kwa mwakilishi wa chama hicho eneo la Pwani.

Lakini kwa mara nyingine alishindwa katika uchaguzi wa ubunge wa Voi mnamo 1992. Baada ya hapo aliamua kustaafu kutoka siasa na kuamua kujihusisha na shughuli za biashara na kilimo nyumbani kwake kijijini Ishamba.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke