Makala

MWANASIASA NGANGARI: Zacharia Onyonka alifariki kabla ya kuwa Waziri wa Fedha, jambo alilotamani sana

October 6th, 2019 4 min read

Na KEYB

MAREHEMU Dkt Zacharia Theodore Onyonka alipata umaarufu mkubwa katika jamii ya Wakisii kwa misingi kwamba ni mmoja wa wanasiasa walioshindania nafasi ya kuwa wasemaji wa jamii hiyo kuanzia miaka ya 1960s hadi 1990s.

Wengine walikuwa ni aliyekuwa mbunge wa Kitutu Magharibi katika miaka ya mapema miaka ya sitini (‘60s) na Waziri wa kwanza kutoka eneo la Kisii, Lawrence Sagini Ndemo na aliyekuwa Mbunge wa Nyaribari Chache na Waziri, Bw Simon Nyachae.

Aliingia bungeni, kwa mara ya kwanza, baada ya kumshinda marehemu Sagini katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka wa 1969. Alikuwa na umri mdogo wa miaka 25 pekee.

Sagini, ambaye pia ni marehemu, ndiyo mtu wa kwanza kutoka jamii ya Wakisii kuteuliwa katika baraza la mawaziri tangu Kenya ilipopata uhuru. Alihudumu kama Waziri wa Serikali za Wilaya kati ya 1964 hadi 1969.

Kando na kuhudumu kama mbunge, Onyonka aliwahi kushikilia nyadhifa za Uwaziri katika wizara za Elimu, Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo, Biashara na Masuala ya Kigeni katika serikali za rais wa kwanza nchini Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Rais Mstaafu Daniel Moi.

Onyonka alizaliwa mnamo Juni 28, 1939 katika wilaya ya Meru (sasa kaunti ya Meru) ambako babake, Godrico Oeri Mairura, alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi. Alikuwa mtoto wa pili katika familia ya Oeri na Mama Kerobina Kebati.

Familia hiyo ilirejea Kisii baada ya babake Onyonka kujiuzulu kazi ya polisi na kujiunga na Utawala wa Mkoa kama naibu chifu.

Shuleni, Onyonka alikuwa mwanafunzi mwerevu na mwenye mienendo mizuri. Alisomea shule zilizodhaminiwa na Kanisa Katoliki. Nazo ni; Shule ya Msingi ya St Mary’s Nyabururu na kisha akajiunga na Shule ya Upili ya St Marys Yala, hadi mwaka wa 1958.

Miongoni mwa wanafunzi wenzake katika shule hiyo ya upili alikuwa Peter Oloo Aringo ambaye baadaye walihudumu pamoja katika baraza la mawaziri wakati wa utawala wa Mzee Moi.

Baada ya kukamilisha masomo katika shule ya upili, Onyonka aliajiriwa na lililokuwa Baraza la Wilaya ya Gusii hadi 1960 alipopata udhamini wa kimasomo uliomwezesha kujiunga na Chuo Kikuu cha Puerto Rico jijini San Juan nchini Amerika.

Alihitimu kwa shahada ya digrii katika taaluma ya uchumi na mnamo 1966 alijiunga na Chuo Kikuu cha Syacuse, jijini New York kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya benki. Baada ya kuhitimu alianza kusomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu hicho hicho cha Syracuse. Ni wakati huo ambapo Onyonka alijunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama mhadhiri msaidizi huku akiendelea na utafiti kwa ajili ya shahada yake ya uzamifu. Alihitimu mnamo 1969.

Onyonka alifanya kazi kwa karibu na Profesa Terry Ryan wa Idara ya Takwimu ambaye alimsaidia pakubwa hadi akahitimu. Baadaye, Chuo Kikuu Cha Nairobi kilimwajiri kama Mhadhiri katika Idara ya Masomo ya Kiuchumi.

Lakini alivutiwa na siasa. Na kwa kuwa Wakisii waliamini kuwa mwanamume ambaye hajaoa hafai kupewa wadhifa wa uongozi, aliamua kuoa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Beatrice Mughamba kutoka Moshi, Tanzania. Nyakati hizo Beatrice alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Cha Nairobi.

Wenzake chuoni wakati huo walikuwa Chris Obure (sasa Waziri Msaidizi katika Wizara ya Uchukuzi, mbunge wa zamani wa Webuye Musikari Kombo na aliyekuwa Katibu wa Wizara Sospeter Arasa.

Onyonka na Beatrice walioana rasmi mnamo Agosti 1969. Walijaaliwa watoto sita: Elizabeth Kwamboka (aliyezaliwa 1970), Tolia Nakadori (1972), Kiki Christopher Robert (1975), David Wilfred (1976), Timmy Eric (1977) na Naanjela Anna (1980).

Lakini, awali wakati Onyonka alikuwa akifanyakazi katika Baraza la Wilaya ya Kisii, kabla ya kuelekea Amerika kwa masomo ya juu, alikuwa amemuoa Bi Teresia Nyakarita. Walijaaliwa mwana wa kiume, Richard Momoima Onyonka, mbunge wa sasa wa Kitutu Chache Kusini kwa tiketi ya Ford Kenya. Bw Momoima pia aliwahi kuhudumu kama Waziri Msaidizi wa Masuala ya Kigeni katika serikali ya muungano ulioongozwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Onyonka alipokuwa Amerika kwa masomo, Teresia aliolewa na mtu mwingine. Momoima aliungana na babake alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Upili ya Kisii. Beatrice alimkubali kama mwanawe.

Momoima alipenda kushirikiana na babake katika kampeni za kisiasa na hivyo ndivyo alivyopata tajriba zilizomwezesha kushinda kiti cha ubunge cha Kitutu Chache Kusini mara tatu.

Baada ya kumshinda Bw Sagini katika uchaguzi mkuu wa 1969, Rais Kenyatta (Hayati) alimteua kuwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi kuchukua mahala pa Tom Mboya ambaye alikuwa ameuawa Julai 9 mwaka huo jijini Nairobi.

Baadaye Onyonka alihudumu Waziri katika wizara za Afya, Nyumba na Huduma za Kijamii, Habari na Utangazaji, Elimu, Sayansi na Teknolojia na hatimaye Wizara ya Masuala ya Kigeni aliyoshilikia kwa miaka miwili na kuacha kumbukumbu kuu.

Alitamani sana kuhudumu kama Waziri wa Fedha kwa sababu ya utaalamu aliyokuwa nayo katika masuala ya benki na fedha, lakini alifariki 1996 kabla ya kutimiza ndoto hiyo.

Kama mbunge alianzisha miradi ya kuwasaidia wananchi kama vile barabara na shule. Alikuwa akisafiri kuelekea eneo bunge lake kila Ijumaa kukagua miradi ya ujenzi, uteuzi wa wanachama wa bodi za usimamizi wa shule, uajiri wa walimu kati ya masuala mengine.

Alikuwa ni mtu aliyependa kufanyakazi pamoja na viongozi wenzake, bungeni, serikali na katika wilaya nzima ya Kisii. Tofauti na wanasiasa wengine Onyonka aliheshimu utawala wa sheria na haki ya kila mtu.

Isitoshe, tofauti na wanasiasa katika enzi za tawala wa Hayati Kenyatta na Mzee Moi, Onyonka alichelea tabia ya kujitajirisha kwa mali ya umma. Hii ndio maana wakati mmoja alipopewa ardhi ya ukubwa wa ekari 50 katika eneo la Kitale alikataa na badala yake akapendekeza ipewe wakati wa eneo bunge lake.

Wakati ambapo siasa za urithi wa Mzee Kenyatta zilipamba moto kati ya 1976 na 1978 na jaribio la mapinduzi ya serikali ya Moi mnamo 1982, na mivutano iliyofuata ndani ya iliyokuwa chama tawala, KANU, Onyonka alipenda kuchukua msimamo usioegemea upande wowote. Badala yake alijaribu kupatanisha pande hasimu na kuhubiri maridhiano.

Onyonka alipata hadhi na tuzo nyingi katika maisha yake kama msomi na kama mwanasiasa. Mzee Kenyatta alimpa hadhi kuu nchini almaarufu, “Elder of the Golden Heart (EGH). Chuo Kikuu cha Syracuse alikosomea nacho kilimtuza Shahada ya taadhima ijulikanayo kama, “Doctor of Letters” kwa huduma yake ya kipekee kwa jamii.

Kando na nyadhifa za ubunge na uwaziri, Onyonka aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Kanu, tawi la Kisii, mwanachama wa Baraza la Mawaziri wa ACP/EEC na Shirika la Maendeleo la Nchini za Kanda hii (IGAD) na mwanachama wa Kamati ya Mazungumzo kuhusu Upatanishi Nchini Sudan Kusini. Vile vile, Onyonka alikuwa mwanachama wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Ustawi Afrika Mashariki.

Mnamo 1988, aliugua ugonjwa wa kiharusi na afya yake ikaanza kudhoofika. Licha ya tatizo hilo aliendelea kuchapa kazi kama Waziri wa Utafiti na Mafunzo ya Kiteknolojia hadi afya yake ilipozorota zaidi na akafariki mnamo Oktoba 22, 1996.