Habari Mseto

Mwanasiasa wa ODM azimwa kuwania viti vya kisiasa

May 1st, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

MWANASIASA wa ODM wa Kaunti ya Lamu, Rishad Amana, amepata pigo kubwa baada ya mahakama ya Lamu kumpiga marufuku ya kugombea kiti chochote cha kisiasa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amana ambaye aligombea kiti cha eneobunge la Lamu Magharibi na kuibuka wa pili kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, alikuwa ameshtakiwa kwa makosa mawili, ikiwemo kumpiga mtu na kusababisha vurugu kwenye kituo cha kuhesabia kura cha Mokowe mnamo Agosti 9, 2017.

Akitoa uamuzi wake Jumatatu, Jaji Mkazi wa Mahakama ya Lamu, Bi Njeri Thuku, alisema Bw Amana ana hatia kwa makosa yote.

Mahakama ilimpiga faini ya Sh 10,000 au miezi mitatu gerezani kwa kosa la kwanza la kumpiga mtu ilhali kosa la kusababisha fujo kituoni  akipigwa faini ya Sh 100,000 au kifungo  cha miezi mitatu gerezani.

Mahakama pia iliamua kumpiga marufuku Bw Amana ya kutosimama kiti chochote cha kisiasa eneo hilo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Baada ya uchunguzi, imebainika kuwa una hatia na unatakikana kulipa faini ya Sh 10,000 kwa kosa la kwanza la kumpiga mtu na Sh 100,000 kwa kosa la pili la kusababisha fujo kituoni au miezi mitatu gerezani kwa kila kosa. Pia huruhusiwi kuwania kiti chochote cha kisiasa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” akasema Bi Thuku.

Mapema Machi mwaka huu, Bw Amana alikuwa ameshinda kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama, kwenye Mahakama Kuu ya Malindi, hatua ambayo ilipelekea kutupiliwa mbali kwa ushindi wa mbunge huyo.

Uamuzi wa Jumatatu wa mahakama huenda ukamzuia Bw Amana kushiriki uchaguzi mdogo wa eneobunge la Lamu Magharibbi iwapo utaandaliwa mwaka huu.

Kufikia sasa tarehe ya uchaguzi huo mdogo bado haijatangazwa hasa baada ya Bw Muthama kuwasilisha kesi ya kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu katika Mahakama ya Rufaa mjini Malindi.

Kesi hiyo itaanza kusikizwa Mwezi huu.