Makala

Mwanateknolojia na mwalimu stadi

March 24th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

KUHUSISHA wanafunzi moja kwa moja katika masomo yanayohitaji ubunifu wa kiteknolojia, kunawapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini zaidi.

Mawanda ya fikira zao hupanuka upesi, uelewa wao huimarika na hatimaye huamshiwa hamu ya kuwa wavumbuzi baada ya kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida.

“Nashirikisha ubunifu mwingi wa kiteknolojia katika ufundishaji wangu. Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo huwasisimua sana wanafunzi, matumizi ya michoro, video na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya masomo kuvutia,” anasema mwalimu John Isaac Ochieng.

Kwa mtazamo wake, wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi iwezekanavyo ili wajiamini zaidi katika usomaji na ujifunzaji wa dhana mpya ndani na nje ya mazingira ya shuleni.

“Njia rahisi ya kukuza wanafunzi katika safari ya elimu ni kuwapa majukwaa yatakayowawezesha kuhusisha wanachokisoma darasani na matukio ya kawaida katika jamii. Matumizi ya vifaa vya kidijitali huchochea zaidi ubongo wa mwanafunzi kufanya kazi,” anaelezea.

Ochieng alizaliwa katika kijiji cha Rageng’ni, Rarieda, Kaunti ya Siaya.

Ndiye wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa Bw Saul Achila na Bi Salome Anyango.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Nyangera, Siaya (2003-2010) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Ukwala Boys, Siaya (2011-2012) kisha Bondo Township, Siaya (2013-2014).

Japo matamanio yake yalikuwa kujitosa katika taaluma ya udaktari, alihiari kusomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Bondo, Siaya (2015-2017).

Aliyemchochea kujibwaga katika ulingo wa ualimu ni Bw McDonald Odongo ambaye alimfundisha somo la Hisabati na kumpokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika shule ya upili.

Ochieng alishiriki mafunzo ya nyanjani katika Shule ya Msingi ya Usenge, Siaya, mnamo 2017 na akaajiriwa katika Shule ya Msingi ya Pristine Academy mjini Bondo mnamo 2018.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia Upright Academy, Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu (2019-2020).

Amekuwa mwalimu wa Hisabati na somo la Sayansi na Teknolojia katika Shule ya Kingsmead Junior Academy iliyoko Ruaka, Kaunti ya Kiambu, tangu mwaka wa 2021.

Anaamini kwamba mwalimu bora anastahili kuwa kielelezo chema kwa wanafunzi wake huku akiwahimiza kujitahidi masomoni ili wazifikie ndoto zao za kiakademia.

“Anatakiwa pia kuwa karibu na wanafunzi wake, atambue changamoto wanazozipitia, aelewe kiwango cha mahitaji ya kila mmoja wao, awashauri ipasavyo na awaamshie hamu ya kuthamini stadi za kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika.”

“Mwalimu anayejali maslahi ya wanafunzi wake anastahili kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya somo lake. Apende kufanya utafiti, awe mchangamfu na ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote,” anasisitiza.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Ochieng ni kujitosa katika fani ya uandishi wa vitabu vya kiada anavyohisi vitabadilisha sura ya ufunzaji wa somo la Hisabati nchini Kenya.

Anapania pia kujiendeleza kitaaluma kwa kusomea shahada ya ualimu.