Habari Mseto

Mwanaume afariki baada ya kuburudika kingono na mjane

August 14th, 2019 1 min read

NA WYCLIFFE KIPSANG

WAKAZI wa Lokesheni ya Ngeria, Kaunti ya Uasin Gishu mnamo Jumatatu waliamkia habari za kushangaza ya mwanaume aliyefariki katika hali ya kutatanisha.

Habari zilisema kuwa mwanamume huyo alifariki baada ya kushiriki ngono na mjane mwenye umri wa miaka 50.

Bw James Kiptoo, 35 yadaiwa alikuwa akinywa pombe kwenye baa moja eneo la Sachangwan karibu na uwanja wa ndege wa Eldoret Jumapili usiku, alipokutana na mwanamke huyo ambaye jina lake bado halijabainika.

Wakazi walikuwa wakiendelea kumiminika katika shamba la mahindi kutazama mwili wa Bw Kiptoo ambaye mauti yalimpata akila uroda na mwanamke huyo shambani humo.

Mwanamke huyo aliwasimulia polisi jinsi Bw Kiptoo alizidiwa na mahanjam baada ya kumeza vidonge vya kusisimua mwili kimapenzi.

Chifu wa kata ya Ngeria Mathew Arusei aliwatahadharisha vijana dhidi ya kujihusisha na masuala yasiyo ya kimaadili kama kushiriki ngono na kunywa pombe kiholela ambayo yanahatarisha maisha yao.

Polisi kutoka kituo cha Kiambaa waliowasili kwenye eneo la tukio walichukua mwili wa mwendazake na kuupeleka katika mochari ya hospitali ya Moi (MTRH).