Kimataifa

Mwanaume ahadaa majirani anazika paka, kumbe ni mwanawe!

January 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAUME mmoja kutoka Mexico aliwahadaa majirani kumpa mahali pa kuzika paka wake aliyefariki, lakini watu wakashangaa baadaye walipobaini kuwa alimzika mwanawe.

Mtoto huyo wa mwaka mmoja anahofiwa kuwa alizama katika maji bafuni, ndipo jamaa huyo akaamua kumzika bila kuwafahamisha watu.

Wakazi wa eneo hilo la Albuquerque walishangaa baadaye wakati polisi walifika na kuufukua mwili wa mtoto.

Wakazi walimpa jamaa sehemu ya kumzika ‘paka’ wake mahali wamekuwa wakizika wanyama wao wanaokufa kwani alikuwa mfanyakazi wa nyumbani.

Wakazi hao, hata hivyo, walisema kuwa jamaa huyo siku za majuzi amekuwa akionyesha tabia zisizo za kawaida, na kuongeza “tulianza kubaini hivyo kabla ya Krismasi.”

Walisema kuwa jamaa huyo kwa jina David Zuber alitegea wakati majirani wameenda kusherehekea krismasi ndipo akawapigia simu kuwapa ombi hilo.

“Alisema ni mmoja kati yap aka wake ambaye alikuwa amekufa,” akasema jirani ambaye mtoto alizikwa kwake.

“Hapa ndipo tumekuwa tukizika mbwa wetu wote ambao wamekufa,” akaongeza.

Lakini waliporejea kutoka likizo, walisema polisi walifika na kuanza kukagua, ndipo wakafukua mwili.

“Alikuwa amezikwa chini ya mzoga wa mbwa huko nyuma ya nyumba,” akasema jirani huyo.