Habari Mseto

Mwanaume ajuta kumuua mwanawe na kusulubisha mwili kama Yesu

March 14th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MWANAMUME alishtakiwa Jumanne katika mahakama ya Nakuru kwa kumuua mwanawe mwenye umri miaka minne na kisha kuusulubisha mwili wake kama alivyofanyiwa Yesu Kristo..

Bw Ezekiel Kagiri Njue aliyefikishwa mbele ya Jaji Maureen Odero na kushtakiwa kwa kutenda kitendo hicho Machi 11, 2018 nyumbani kwake karibu na kanisa la Prayer Centre, eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru.

Inadaiwa Bw Kagiri alimnyonga mtoto huyo kwa kutumia mshipi na kisha akapigilia mikono yake kwa misumari nyumbani kwake.

Baada ya kutekeleza kitendo hicho cha kinyama, inasemekana alitoroka na kuacha mwili wa mtoto ndani ya nyumba.

Alikamatwa Jumatatu baada ya kujisalimisha katika kambi ya askari wa utawala iliyoko Lanet na kukiri kwamba alitekeleza kitendo hicho cha kikatili.

Baada ya kuhojiwa na polisi ilibainika kwamba alitumia nyundo na misumari kuunganisha mikono ya mtoto huyo kabla ya kutoroka.

Mnamo Jumapili, maafisa wa polisi kutoka kituo cha Bahati walipata mwili wa mtoto huyo ndani ya nyumba ya baba yake na kuupeleka mochari.

Wakazi walisema mshukiwa alikuwa ametengana na mkewe ambaye alimuacha na mtoto huyo.

Alipofikishwa mahakamani jana, Bw Kagiri hakujibu mashtaka baada ya mahakama kuagiza akachunguzwe kubaini iwapo ana akili timamu.

Jaji Odero aliagiza azuiliwe katika gereza la Nakuru akisubiri kufanyiwa uchunguzi huo. Atarejeshwa kortini April 5.

Katika kisa tofauti, mwanamume mwenye umri wa 29 anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Rangwe, Kaunti ya Homabay kwa kushukiwa kumuua mkewe.