Habari Mseto

Mwanaume ang'atwa nyeti kwa kutolipia uroda lojing'i

October 23rd, 2018 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

POLISI katika Kaunti ya Taita Taveta wanamsaka mwanamke aliyetoroka baada ya kuuma sehemu nyeti za mwanamume waliyekosana kuhusu bei ya huduma za mapenzi wakiwa ndani ya lojing’i.

Ingawa kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo, Bw Francis Warui hakupatikana ili kutoa maelezo zaidi, maafisa walio chini yake walisema kisa hicho kilitokea katika eneo la Njukini, mjini Taveta usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mwanaume huyo anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja nchini Tanzania ambako alipelekwa na wasamaria wema waliommokoa baada ya kung’atwa.

Wakazi walioshuhudia kisa hicho walieleza kuwa wawili hao walianza ugomvi kuhusu malipo na kupelekea mwanamke huyo kuuma uume wa mteja wake kisha akatoroka.

Duru za kuaminika zilieleza kwamba wawili hao walikuwa walevi na walisikika wakizozana chumbani humo kabla ya mwanamume huyo kuomba msaada.

Wenyeji walilaumu kukithiri kwa pombe haramu katika eneo hilo kama chanzo cha visa kama hivyo.

“Vilevile kuna pombe haramu kutoka nchi jirani ya Tanzania ambayo inaingizwa humu nchini kisiri,” akasema mwenyeji mmoja.

Alisema kuwa wenye mabaa katika eneo hilo wamekuwa wakivunja sheria za uuzaji wa vileo kwa kuuza pombe kabla ya masaa yaliyowekwa kisheria, almaarufu ‘Sheria za Mututho’.

“Pombe inauzwa kila wakati. Wenye mabaa hawajali sheria ya nchi,” akasema.

Alidai kuwa maafisa wa polisi wa eneo hilo wanapewa rushwa na wenye biashara za pombe ili kukwepa mkono wa sheria.