Habari Mseto

Mwanaume azuiliwa rumande kwa madai ya kuambukiza mwanamke ukimwi kimakusudi

February 21st, 2024 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameomba mahakama kuu iamuru mwanaume anayeshtakiwa kuambukiza mwanamke ukimwi (HIV/AIDS) atolewe sampuli za damu apimwe ikiwa anaugua ugonjwa huo usio na tiba.

Hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi, wa mahakama ya Milimani alielezwa shtaka linalomkabili mwanaume huyo ni baya kwa sababu adhabu yake ni kifungo cha maisha akipatikana na hatia.

“Naomba hii mahakama iamuru mshtakiwa atolewe sampuli za damu kupimwa hali yake ndipo afunguliwe mashtaka mengine,” kiongozi wa mashtaka James Gachoka alimsihi hakimu.

Bw Gachoka alieleza mahakama kwamba mshtakiwa anakabiliwa na shtaka kwamba akijua ni mhasiriwa wa ukimwi alifanya tendo la ndoa na mwanamke bila kondomu kwa lengo la kumwambukiza maradhi hayo yasiyo na tiba.

Mshtakiwa amekana kati ya Oktoba 5, 2022 na Juni 30, 2023 akijua anafanya makosa alishiriki tendo la ndoa na mwanamke bila kondomu ilhali anajua ni mhasiriwa wa ukimwi.

Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba ripoti kutoka Mwanakemia wa Serikali ni muhimu kubaini ikiwa mshtakiwa yuko na ukimwi au la.

Bw Ochoi alielezwa endapo mshtakiwa atakutwa yuko na ukimwi basi mashtaka yatabadilishwa.

Mahakama ilielezwa adhabu ya makosa hayo ya kuambukiza wanawake ukimwi kwa hiari ni kali kwa mujibu wa sheria.

Mmoja akipatikana na hatia anaweza kufungwa maisha gerezani.

Bw Gachoka alieleza mahakama huenda afisi ya DPP ikamfungulia mshtakiwa makosa mengine kulingana na ripoti ya Mwanakemia wa Serikali.

Awali Bw Gachoka aliomba kesi hiyo isikizwe faraghani mlalamishi asitambulikane kwa umma.

Bw Ochoi alikubaliana na matamshi ya kiongozi wa mashtaka, wakili wa mhasiriwa na wakili anayemwakilisha mwanaume huyo “kwamba haki za mlalamishi zapasa kuzingatiwa ili asifedheheke.”

Mahakama iliamuru mshtakiwa azuiliwe katika gereza la Viwandani hadi Feburuari 26, 2024.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Kachero Eunice Nyaga aliomba mshtakiwa anyimwe dhamana kwa vile imekuwa vigumu kumpata.

Bi Nyaga aliomba mahakama iamuru mshtakiwa azuiliwe gerezani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.