Habari

Mwanavitimbi Nyasuguta asimulia alivyotwangwa na kuvuliwa nguo

August 16th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWIGIZAJI katika kipindi cha maarufu cha televisheni cha Vitimbi, Bi Eunice Wambui almaarufu Nyasuguta Alhamisi alisimulia katika mahakama ya Nairobi jinsi alishambuliwa na wanaume wawili waliompiga na kumjeruhi mbali na kumwibia pesa Sh16,000 na mikufu ya dhahabu na kumtoa nguo

Bali na kumtandika, wavamizi hao walirarua nguo zake na kumuumiza.

Akiwatambua washambulizi wake mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Elector Riany kama Bw John Ngigi Kabogo, Joseph Karanja na Bi Dorica Wambuga, Nyasuguta alisema  alishambuliwa kwa kuuliza bili ya maankuli waliyokuwa wameongezewa katika kilabu maarufu cha Oleng Sidai, kilichoko kwenye barabara ya Kiambu Road kaunti ya Nairobi.

Washukiwa John Ngigi Kabogo (kulia), Joseph Karanja na Dorica Wambuga walipofikishwa kortini Agosti 16, 2018 kujibu mashtaka ya kumshmbulia Bi Eunice Wambui (Nyasuguta). Picha/ Richard Munguti

Nyasuguta alisema walikuwa wameenda kwenye kilabu hicho kula chakula cha mchana wakiandamana na mwaniaji kiti cha Embakasi Kaskazini aliyeshindwa Bw Harrison Wangoro Mwangi na mfanyabiashara mwingine Bw George Maina.

Mwigizaji hiyo anayepeperusha matangazo ya Safaricom katika runinga alimweleza Bi Riany walikuwa wamemaliza kula na Bw Mwangi akalipa bili ya Sh14,500 walipoongezewa bili nyingine ya Sh1,650.

Alisema Bw Maina alisema atalipa bili hiyo kisha akapeana kadi mbili za benki zitumike kulipa pesa hizo.

Mlalamishi huyo alisema mwuzaji aliyewapa bili hizo alienda na kadi hizo za Bw Maina na kupoteza moja.

“Bw Maina alimpa mwuzaji kadi moja na kumweleza aitumie kulipia bili hiyo,” alisema Nyasuguta.

Nyasuguta aliyekuwa akitoa usahidi katika kesi ya wizi wa mabavu dhidi ya Mabw Kabogo na Karanja pamoja na Bi Wambuga alisema alishambuliwa hata nguo zake za ndani na sidiria ikararuriwa.

“Nilipigwa nikaanguka chini. Nilimwita Bw Mwangi nikamwambia achukue video jinsi ninapigwa,” alisema Nyasuguta.

Bi Bi Eunice Wambui (Nyasuguta) alieleza mahakama kuwa hangeendesha gari akiwa ameraruriwa nguo na kuvuliwa sidiria. Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilielezwa wavamizi hao waliwashambulia Nyasuguta hata akatoroka na kuacha gari lake karika egesho la kilabu hicho.

Alienda hospitali kutibiwa majeraha aliyopata na kuwaeleza polisi waliompa Fomu ya P-3.

“Nilienda hospitali nikatoa nguo nikakaguliwa kwa vile nilikuwa nimeumizwa. Ilibidi niache gari langu kwenye kilabu hicho,” alisema.

Alikanusha madai ya wakili anayewatetea washtakiwa kwamba walikuwa walevi na walikuwa wameshindwa kulipa bili ya vinywaji na chakula walichokuwa wamelipa.

“Bili ilikuwa imelipwa ya Sh14,500. Niliuliza kadi ya benki iliyopotezwa na mwuzaji aliyepewa. Vita vilitokana na kutoweka kwa kadi ya benki ya Bw Maina,” alisema Nyasuguta akijibu maswali ya wakili.

Akieleza sababu ya kuacha gari, Bi Nyasuguta alisema hangeendesha gari akiwa ameraruriwa nguo na kuvuliwa sidiria.

“Uliacha gari kwenye kilabu ukachukua Machi 21, 2018 kwa vile ulikuwa mlevi wa kupindukia. Ulishindwa kulipa gharama ya Sh2,000?” Nyasuguta aliulizwa na wakili wa washtakiwa.

Nyasuguta baada ya kutoa ushahidi dhidi ya washukiwa watatu Agosti 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

“Hapana nilikuwa nimeumia. Nilikuwa sina nguo za ndani. Singeweza kuendesha gari na pia nilikuwa nimeumizwa. Nilihisi aibu kuendesha gari jinsi nilivyokuwa. Sikuwa mlevi kama inavyodaiwa,” alijibu mshtakiwa.

Mabw Maina na Mwangi walitoa ushahidi jinsi walivamiwa na washtakiwa kwa vito vya chuma na kuporwa pesa na simu aina yas Tecno na Samsung.

Washtakiwa walikanusha shtaka hilo la wizi wa mabavu na wameachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000.