Habari Mseto

Mwandamanaji ashtakiwa kuvunja Bunge na kuiba CCTV za Sh2.2 milioni


MWANDAMANAJI ameshtakiwa kwa kuvunja jengo la Bunge la Kitaifa na kuiba kutoka mle ndani vifaa vya kielektroniki vya thamani ya Sh2.2 milioni.

Kevin Mwamiri Mang’are alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi wa mahakama ya Milimani Bw Gilbert Shikwe.

Mang’are alikana mashtaka matatu ya kuvunja na kuingia katika jengo la bunge mnamo Aprili, Mei na Juni 2024.

Kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech alieleza mahakama Mang’are alivunja na kuingia Basement No.2 ya Bunge mnamo Aprili 23, 2024.

Akiwa mle ndani mshtakiwa alikana kuiba vifaa vya kamera za CCTV vya thamani ya Sh890,000 mali ya kampuni ya ulinzi ya Magal Security Solutions Company (MSSC).

Kamera ambazo mshtakiwa alidaiwa kuiba ni muundo wa CISCO.

Shtaka la pili dhidi ya Mang’are lilisema mnamo Mei 20, 2024 aliiba vifaa vya kamera za CCTV vya thamani ya Sh890,000 mali ya MSSC.

Shtaka la tatu lilisema mnamo Juni 25, 2024 mshtakiwa huyo vunja Bunge na kuiba kifaa cha kamera ya CCTV chama thamani ya Sh445,000 mali ya MSSC.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “hana pesa ila anawategemea wahisani.”

Alitiwa nguvuni Julai 8, 2024 na kufikishwa mahakamani Julai 10, 2024.

Bi Koech hakupinga ombi hilo la mshtakiwa kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Akitoa uamuzi, hakimu alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa.

Bw Shikwe aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili upande wa mashtaka ueleze ikiwa umemkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.

[email protected]