Habari Mseto

Mwandani mwingine wa Ruto amulikwa

July 2nd, 2020 1 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta sasa wanataka Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany apokonywe wadhifa huo kwa kudai fedha za chama hicho zimeibwa.

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu na mwenzake wa Cherangany Joshua Kutuny, wamesema Alhamisi kwamba Bw Kositany hafai kuendelea kuhudumu katika wadhifa huo huku akiendelea “kuharibu” jina la chama.

Bw Ngunjiri ameshangaa ni kwa nini mbunge huyo wa Soy anatoa madai hayo wakati huu, ilhali amekuwa akishikilia wadhifa wa Katibu Mkuu wa Jubilee tangu kilipoanzishwa.

“Bila shaka madai kama haya yanalenga kumharibia jina Rais Kenyatta ambaye ndiye kiongozi wa Jubilee,” akasema Bw Ngunjiri.

Akaongeza: “Kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama, Kositany alipaswa kufuata taratibu zifaazo ndani ya chama kutoa madai yake badala ya kufanya hivyo kupitia vyombo vya habari.”

Mbunge huyo alimsuta Bw Kositany kwa madai ya kuendeleza ajenda ya kundi la ‘Tangatanga’ ya kuiharibia Jubilee jina kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Naye Bw Kutuny amesema Bw Kositany hafai kuruhusiwa kuendelea kuhudumu katika wadhifa huo kwa kukiuka sera na maadili ya Jubilee.

“Ipo haja ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kuitishwa kumpiga kalamu Bw Kositany kwa kuendeleza ajenda ya vuguvugu pinzani,” akasema.

Baada ya kuondolewa kwa Aden Duale kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Kositany ndiye mshirika pekee wa Naibu Rais William Ruto aliyesalia katika nafasi ya uongozi ndani ya Jubilee.

Wengine waliovuliwa nyadhifa za uongozi ni Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, mwenzake wa Nakuru Susan Kihika na Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki.

Mapema wiki hii, Bw Kositany aliibua madai ya wizi na ufujaji wa fedha za chama katika makao makuu ya Jubilee.

Alidai Sh7 milioni hutumiwa kugharamia chai na vitafunio kila mwezi.