Habari

Mwandishi mashuhuri Binyavanga Wainaina afariki

May 22nd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWANDISHI mashuhuri Binyavanga Wainaina amefariki akiwa na umri wa miaka 48.

Iliripotiwa kuwa Bw Wainaina ambaye alishinda tuzo ya The 2002 Caine kwa Waandishi wa Afrika alifariki mwendo wa saa nne za usiku Jumanne baada ya kuugua kiharusi.

Mnamo Januari 2019 Binyavanga, anavyofahamika na wengi, aliibua msisimko miongoni mwa Wakenya mitandaoni pale alipotangaza hadharani kwamba yeye ni shoga.

Huku akipinga sheria kadhaa zinazopinga ushoga zilizopitishwa katika mataifa kadhaa barani Afrika, Binyavanga aliandika hivi: “Hakuna mtu ambaye amesikia hili maishani mwangu. Mimi ni shoga Mama,”. Alifichua ukweli huu katika aya kwa jina “A Lost Chapter” katika kitabu, “One Day I will Write About This Place.”

Baadaye alituma ujumbe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter: “Kwa mtu yeyote ambaye amechanganyikiwa au ana tashwishi, mimi ni Shoga na ninafurahi.”

Hadithi fupi aliyoandika kwa jina “Discovering Home” ilipata tuzo ya 2002 Caine Prize for African Writing. Na mnamo 2003 alipewa tuzo na Chama cha Wachapishaji Nchini (Kenya Publishers Association) kwa njia ya kutambua mchango wake katika fasihi ya Kenya.

Kwa mara ya kwanza Bw Binyavanga aliugua kiharusi nyumbani kwake karibu na Bomas of Kenya mnamo Oktoba 31, 2015, na akapelekwa India kwa matibabu.