Makala

MWANGI: Vijana wanafahamu ulevi huahirisha matatizo yao tu!

September 11th, 2020 2 min read

Na DAISY MWANGI

TANGU ugonjwa wa Covid-19 utue nchini mnamo Machi, vijana wengi wamezama kwenye ulevi kupindukia.

Ingawa vilabu vya usiku vimefungwa, maaduka ya vileo na mvinyo bado huwa wazi mchana.Imekuwa ni kawaida kwa vijana kununua pombe na kuipeleka makwao. Vijana wengi wamegeukia ulevi mchana kutwa baada ya kupoteza kazi msimu huu wa Corona.

Asilimia sabini ya watu waliopoteza kazi kwa sababu ya janga la Corona nchini ni vijana. Inamaanisha vijana hao hawana jingine la kufanya isipokuwa kuchapa mtindi tu. Kupoteza kazi pia kumewafanya vijana wengi kutamauka maishani.

Vijana hawana budi kuelewa ya kuwa pombe ya kila siku haitatatua shida zao. Vile vile, wafahamu kuwa pombe ni hatari kwa afya zao. Wanapobugia pombe kila uchao wakumbuke ndoto zao za usoni. Wakumbuke maisha yao ya kesho. Wengi wao wangetaka kuwa na familia kamili, watoto wazuri na hata kuwa viongozi wa kesho. Wasipotahadhari, ulevi utawaangamiza. Vijana hawana budi kijichunga.

Inanikeketa maini kwamba, hata wasichana siku hizi wanabugia vileo. Ni vyema waangalie maslahi yao ya kiafya. Na wanapobugia pombe kila uchao, wajue wanahatarisha maisha yao na yale ya watoto wao siku za usoni.

Serikali haina budi kuhakikisha vijana wanapata kazi. Wengi kwa sasa wanateseka.

Vijana waliosoma na kuhitimu vyema walikuwa wa kwanza kutimuliwa kutoka mahali pao pa kazi pindi tu janga la Corona lilipoanza kuenea nchini. Wengine wamekata tamaa.Hawana la kufanya ila tu vileo na mihadarati.

Ni vyema serikali ishughulikie vijana hao. Vijana wote wakijiharibu, kesho itasalia mahame.

Wazazi pia na viongozi wa kidini wana jukumu la kuzungumza na vijana hao na kuwaeleza kuwa kukatika kwa mwiko sio mwisho wa upishi. Waeleze kesho watakuwa sawa na wala wasikate tamaa.

Na pia wawaonyeshe upendo. Familia na marafiki waache kuwaonyesha kuwadhalilisha vijana waliopoteza kazi. Angalau wapende na kuwasaidia wawezavyo. Hivyo hawatajitoma kwenye pombe au hata kujichukia.

Vijana pia wenyewe kwa wenyewe wanafaa kupeana motisha. Wasilaze mtaani huku wakihurumiana ama kulewa tu bali wapeane motisha na kujaribu kufikiria pamoja kuhusu njia tofauti za kujipatia riziki.

Wasiwe watu wa kukata tamaa kwa haraka. Wakumbuke ya kuwa, panda shuka za dunia ni za kawaida kwa kila mtu.

Leo maisha yanaweza kuwa magumu lakini kesho yakabadilika na kuwa mazuri. Na pia wakumbuke kumwomba Mwenyezi Mungu awakumbuke anapogawa baraka zake.