Habari

Mwangi wa Iria kukamatwa na kuwasilishwa kwa seneti

August 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamemwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kumkamata na kumwasilisha Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria mbele yao Septemba 10, 2020, ajibu maswali kuhusu matumizi ya Sh24 bilioni katika kaunti hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC) Sam Ongeri ametoa amri hiyo Ijumaa baada ya Bw Wa Iria kukaidi agizo la kufika mbele ya kamati hiyo ili awajibikie hitilafu za matumizi kwa miaka mitatu iliyopita.

Hitilafu hizo ziliibuliwa kwenye ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tangu mwaka wa kifedha wa 2015/2016 hadi 2017/2018.

“Hatuwezi kufumba macho yetu kwa hali kama hii ambayo ni kinyume cha Katiba. Kaunti ya Murang’a imepokea zaidi ya Sh24 bilioni kwa miaka mitatu ya kifedha. Sharti gavana Mwangi wa Iria awajibikie makosa katika matumizi ya fedha hizo yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali,” Profesa Ongeri akasema.

“Kwa hivyo ninaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi amsake na amwasilishe kwa nguvu mbele ya kamati hii mnamo Septemba 10, 2020, saa tatu na nusu za asubuhi ili atoe ufafanuzi kuhusu hitilafu katika matumizi ya fedha hizo,” akasema mwenyekiti huyo ambaye ni Seneta wa Kisii.

Kwenye barua aliyotuma kwa kamati hiyo, Bw Wa Iria alisema hangeweza kufika mbele ya kamati ya CPAIC kwa sababu Idara ya Afya imeamuru shughuli zote zisitishwe katika afisi za serikali ya Kaunti ya Murang’a baada ya wafanyakazi wawili kupatikana na virusi vya corona.

Hata hivyo, Profesa Ongeri na maseneta Ochilo Ayacko (Migori) na Samson Cherargei (Nandi) walipuzilia mbali sababu hiyo wakisema kamati hiyo ilimwalika Bw Wa Iria tangu Juni 11, 2020.

“Alifaa kujiandaa mapema kufika mbele ya kamati hii, siku au wiki jana baada ya ripoti ya maambukzii ya virusi vya corona kuchipuza katika afisi za kaunti hiyo,” akasema Bw Ayacko.