Makala

MWANGI: Waajiri waheshimu haki za wafanyikazi wa nyumbani

August 14th, 2020 2 min read

Na DAISY MWANGI

WAJAKAZI ni watu wa maana mno na wanaofaa kuheshimiwa.

Wafanyikazi hawa wa nyumbani huweza kutekeleza majukumu ambayo bila wao, familia nyingi zingekuwa na matatizo ya kulea watoto na kutunza nyumba.

Tunaishi katika nyakati ambazo wengi hawana budi kufanya kazi ili kutosheleza mahitaji ya kifedha ya familia zao. Hivyo basi, familia nyingi hasa mijini hazina budi kuajiri mfanyikazi wa nyumbani.

Kwa kawaida, majukumu ya wajakazi huwa ni kufanya kazi za usafi, kupika na kutunza watoto.

Wengi hurauka asubuhi na mapema ili kuanza kazi ya kuandalia familia kiamsha kinywa, kufanya usafi na kuwatayarisha watoto kwenda shuleni ama hata kuwapeleka.

Licha ya wajakazi kufanya kazi hizi zenye umuhimu sana, waajiri wengi huwanyanyasa.

Wapo wengi wa waajiri ambao huwalipa mishahara duni licha ya serikali kuweka kanuni ya kudhibiti malipo ya wafanyikazi wa nyumba nchini. Kwa mfano, jijini Nairobi hakuna mfanyakazi wa nyumbani ambaye anapaswa kulipwa mshahara wa chini ya Sh10,000.

Wajakazi pia hawafai kufanya kazi kwa zaidi ya saa 52 kwa wiki. Isitoshe, wana haki ya kupewa ruhusa ya kupumzika siku moja kila wiki.

Hata kama waajiri wengi wanajua kuwa wajakazi wao wana haki hizi, huwa wanazipuuza hasa kuhusu malipo, muda wa kupumzika na hata wengine hudhulumu kwa matusi na hata kuwapiga.

Tatizo kubwa la ukiukaji wa haki za wajakazi ni kuwa wengi wao huwa hawazijui. Wengi wao huwa wanachukuliwa mashambani na kupelekwa mijini kufanya kazi za nyumbani na idadi yao kubwa hawana elimu hata ya darasa la nane, mbali na kuwa wanatoka familia maskini zisizo na uwezo wa kusimama kutetea haki zao.

Kutokana na mazingira ya familia zao, wajakazi wengi huwa hawana budi kuvumilia mateso wanayotendewa na waajiri kutokana na shinikizo za kifedha zinazowakumba wao na familia zao.

Serikali na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu hasa haki za wanawake wana jukumu la kuhakikisha kuwa wajakazi wanazielewa haki zao, na pia waajiri wanaowanyima haki na kuwanyanyasa wamechukuliwa hatua kali za kisheria.

Nao waajiri hawana budi kuwaheshimu na kuwatendea haki wajakazi kwa kukumbuka kuwa hawa ni watu ambao unategemea kulinda na kutunza watoto wako, wanafanya maisha yako kuwa nafuu kwa kufanya kazi za nyumbani ambazo zingekutatiza kutokana na shughuli zako za kikazi, na pia hawa ni binadamu wanaostahili kutendewa haki kama wengine.

Unapomnyanyasa na kutomtendea haki mjakazi, fahamu kuwa anaweza akaamua kulipiza kisasi kwa kumtendea mtoto wako mchanga mabaya wakati haupo.