Mwanzo mpya

Mwanzo mpya

LEONARD ONYANGO na WACHIRA MWANGI

UHUSIANO kati ya Mahakama na Serikali Kuu unatarajiwa kuimarika kufuatia kuapishwa kwa Martha Karambu Koome kuwa Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kenya.

Macho yote yameelekezwa kwake kuona ikiwa atafaulu kurejesha uhusiano mwema baina ya Idara ya Mahakama na Rais Uhuru Kenyatta.

Jaji Mkuu Koome na Jaji wa Mahakama ya Juu William Ouko, waliapishwa Ijumaa saa saba mchana katika Ikulu ya Nairobi kwenye hafla fupi iliyohudhuriwa na Rais Kenyatta.

Uhusiano baina ya Idara ya Mahakama na Serikali Kuu ulidorora kwa kiasi kikubwa wakati wa kipindi cha mtangulizi wake Jaji Mstaafu David Maraga.

Hali hii ilisababishwa na msimamo mkali wa Bw Maraga wa kutetea uhuru wa Mahakama na majaji.

Miongoni mwa mambo yaliyozua mvutano kati ya Maraga na serikali kuu ni kupunguzwa kwa bajeti ya Idara ya Mahakama, Jaji Mkuu kudhalilishwa katika hafla za kitaifa, Rais Kenyatta kukataa kuteua rasmi majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) na serikali kupuuza maagizo ya mahakama.

Jaji Koome aliambia jopo la JSC lililomhoji kuwa, atakuwa akiwasiliana kwa simu na Rais Kenyatta mara kwa mara ili kukuza uhusiano mwema.

Alisema anaamini ataweza kumshawishi Rais Kenyatta kuwateua majaji hao ambao sasa wamebaki 40 baada ya mmoja kufariki.

Jaji Koome pia aliambia jopo la JSC kuwa, iwapo kutakuwa na tofauti miongoni mwa majaji wa Mahakama ya Juu, atakuwa anapanga ziara ambapo watapata fursa ya kujadili masuala tata huku wakipata mlo.

“Chakula kinasaidia watu kuzungumza pamoja, hivyo tutakuwa na ziara ambapo tutakutana na kula pamoja ili kutatua shida iliyopo,” Jaji Koome aliambia JSC.

Ijumaa, Rais Kenyatta alihimiza Jaji Mkuu Koome na Jaji Ouko kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao bila upendeleo au misukumo ya kisiasa.

“Tunawaombea na tuko tayari kufanya kazi pamoja nanyi. Fanyeni kazi kwa haki na hatutakuwa na shida nanyi,” akasema Rais Kenyatta.

Serikali pia imeshutumiwa kwa kukiuka na kupuuza maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na mahakama..

Akizungumza katika Mahakama ya Juu dakika chache baada ya kuapishwa, Jaji Mkuu Koome alisema kuwa atatetea uhuru wa Idara ya Mahakama.

Alishauri Wakenya kutumia njia mbadala za kutatua mizozo ili kupunguza msongamano wa kesi mahakamani.

“Tunafaa kutatua migogoro kati yetu hata kabla ya kwenda mahakamani. Tuishi kwa kuzingatia maadili mema na kuepuka migogoro kwani sisi sote ni watoto wa Mungu,” akasema.

Mashirika ya kutetea haki za umma katika ukanda wa Pwani yamemrai Jaji Mkuu Koome, kulinda uhuru wa Idara ya Mahakama.

Kulingana na Afisa wa Mipango ya Dharura katika Shirika la Kiislamu la Kutetea Haki za Binadamu (MUHURI), Bw Francis Auma, serikali imekuwa ikiingilia idara hiyo kwa kuipunguzia bajeti na vitisho vinavyoelekezewa majaji na baadhi ya maafisa wake wakuu.

Kasisi Gabriel Dolan kutoka shirika la Haki Yetu alisema, wana imani kuwa atalinda Mahakama .”Tuna imani naye kwamba atakuwa mwenye msimamo thabiti kwa kuitetea Katiba kama mtangulizi wake, David Maraga,” akasema kasisi huyo.

You can share this post!

Arsenal yakataa wazo la Newscastle United kutaka kumsajili...

Kila bandari Kenya kuwa na mkurugenzi wake mkuu