Habari

Mwanzoni vijana wengi walikuwa na mtazamo potovu na hawakutishika na Covid-19, yasema ripoti

November 5th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

ASILIMIA kubwa ya vijana walikuwa na mtazamo kuwa hawangeambukizwa na maradhi ya Covid-19, ripoti moja imesema.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la Y-Act ambalo ni tawi katika shirika la Amref, asilimia 39 ya vijana walikuwa na mtazamo kuwa uwezekano wao wa kuambukizwa virusi vya corona ulikuwa wa wastani au mchache mno, huku asilimia 26 wakiwa na hofu kuwa wangeambukizwa maradhi hayo iwapo hawangejikinga.

“Asilimia 29 walikuwa na mtazamo kuwa kiwango cha maambukizi ya corona miongoni mwa vijana kilikuwa cha chini mno, nao wengine ikiwa ni asilimia tatu (3) walidhani hawawezi kuambukizwa virusi hivyo kabisa na asilimia nyingine tatu (3) hawakujua wangeathirika na kiwango kipi cha maambukizi,” inasema ripoti hiyo.

Matokeo ya ripoti hii yanatokana na utafiti kupitia njia ya mtandao, pamoja na mahojiano kwa simu yaliyofanywa kati ya Aprili 30 na Mei 5, 2020, na shirika hilo. Utafiti wenyewe ulihusisha sampuli ya vijana 2,153 kutoka kaunti zote 47 nchini.

Utafiti huo ulifanyika wiki chache baada ya kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 kutangazwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Ripoti hiyo inasema kuwa walioshiriki ni vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 35, huku asilimia 49.8 wakiwa wa kike na asilimia 49.3 wakiwa wa kiume.

Kulingana na ripoti hiyo, vijana hao walitoa sababu ya kusema hawakuwa katika hatari ya maambukizi ya corona huku asilimia 43 wakijitetea kuwa hawakuwa wamesafiri sana, asilimia 24 waliripoti kuwa Mungu anawalinda na asilimia tisa (9) wakisema ni wachanga bado.

Wengi wa waliotoa maoni hayo walikuwa vijana wa kiume, kwa ailimia 12 na wa kike kwa asilimia saba.

Asilimia 49.7 walikuwa hawana kazi huku asilimia 19.3 wakiwa wameajiriwa na asilimia 28.4 walikuwa wamejiajiri wenyewe. Asilimia 2.6 hawakupeana majibu kuhusu hali yao kikazi.

Hata hivyo, ripoti inasema kuwa asilimia 98 ya vijana walikiri Covid-19 ni ugonjwa hatari na wakipata maambukizi basi wanakuwa na wasiwasi kwa sababu kufikia sasa hauna tiba.

Zaidi, takwimu zingine za ripoti hiyo zilithibitisha kuwa asilimia 30 ya vijana walipoteza kazi zao au kipato chao kilipungua pakubwa huku asilimia 30 wakisongwa na mawazo.

Pia, utafiti huo ulitambua kuwa asilimia 50 ya kundi hili la watu hawakuwa na uwezo wa kujitenga na kugharimia karantini ya nyumbani iwapo wangepata maradhi ya Covid-19, na hivyo wengi walichagua kufuata maagizo yaliyowekwa na Wizara ya Afya kama vile kubakia nyumbani, kuvalia barakoa, kunawa mikono, kutumia sabuni na maji safi ili kujikinga na maambukizi ya corona.

“Vijana wengi pia walihofia kuwa iwapo wangelazimishwa kusalia nyumbani, mahitaji yao ya chakula ingekuwa asilimia 93, maji asilimia 62 na pesa asilimia 54,” ikasema ripoti.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa wakati ambapo visa vya Covid-19 vinazidi kuongezeka sambamba na vifo nchini.

Idadi ya walioangamia kwa sababu ya Covid-19 kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe imefika jumla ya wagonjwa 1,072 baada ya watu 21 kufariki katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Waziri Kagwe amesema watu 1,008 wamethibitishwa kuugua Covid-19 kutokana na sampuli 6,038 ambapo idadi hii inafikisha jumla ya visa 59,595 tangu kisa cha kwanza kithibitishwe nchini Kenya Machi 13, 2020.

Waziri amesema Alhamisi kwamba watu 802 wamepona ambapo 679 ni wale waliokuwa chini ya uangalizi wa nyumbani huku 123 wakiwa ni wale waliokuwa wanapokea matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

Idadi jumla ya waliopona sasa ni 39,193.