Mwashetani aachia Achani tikiti ya ugavana

Mwashetani aachia Achani tikiti ya ugavana

Na SIAGO CECE

AZIMIO la Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, kuwania ugavana mwaka 2022 limepigwa jeki baada ya Mbunge wa Lungalunga, Bw Khatib Mwashetani, kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wawili hao walitarajiwa kuwa washindani wa karibu kati ya wanasiasa wanaotaka kurithi kiti cha Gavana Salim Mvurya, atakayekamilisha kipindi chake cha pili 2022.

Bw Mwashetani alitangaza majuzi kwamba ameamua kutowania ugavana kwa vile angependa kuendelea kuwakilisha eneobunge la Lungalunga.

Wachanganuzi wa siasa wanasema wawili hao walitarajiwa kuwa washindani wa karibu kwa vile wote wamepata umaarufu katika kipindi ambapo wamekuwa mamlakani, na pia wameonekana kuegemea upande mmoja wa Naibu Rais William Ruto kisiasa katika miaka ya hivi majuzi.

Hata hivyo, Bi Achani hajatangaza rasmi chama anachopanga kutumia kuwania ugavana mwaka 2022 wala muungano wa kisiasa atakaoegemea.

Bw Mvurya, ambaye humpigia debe naibu wake, alishinda kiti hicho kupitia Chama cha Jubilee mwaka wa 2017.

Wanasiasa wengine wanaotarajiwa kuwania wadhifa huo ni Katibu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga, aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Chirau Mwakwere, mhandisi katika Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), Bw Lung’anzi Chai na Bw Daniel Dena.

Mhadhiri wa chuo kikuu ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa, Prof Halim Shauri asema ijapokuwa sasa Bi Achani amevuka daraja moja, bado anakumbwa na changamoto ya kuamua haraka chama au muungano atakaotumia kutetea kiti hicho.

“Suala kuhusu vyama vya kisiasa siku hizi ni muhimu kuzingatiwa. Ijapokuwa (Bw Mvurya na Bi Achani) wanapiga kampeni, ukweli kwamba hajatangaza chama chake huenda ukamweka taabani,” akasema.

Wakati Dkt Ruto alipozuru Lungalunga mnamo Julai, baadhi ya wanasiasa akiwemo Bw Lung’anzi waliandamana naye.

Mwanasiasa huyo baadaye alivaa kofia iliyo na nembo ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kuashiria amejiunga na mrengo wa naibu rais.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, Prof Hassan Mwakimao hata hivyo asema Bi Achani atalazimika kupanga mikakati ipasavyo hata kama kuna baadhi ya watu wanaoona ana nafasi nzuri baada ya Bw Mwashetani kujiondoa.

Kulingana naye, kuna masuala mengi ambayo wapigakura wataangalia katika uchaguzi ikiwemo kutaka uongozi mpya.

“Naamini kuna mambo mengi ambayo yatajitokeza kumkosoa wakati wa kampeni, ikiwemo watu ambao watakosoa utawala aliokuwemo kwa miaka kumi,” akasema.

Prof Boga ambaye huegemea upande wa Chama cha ODM anatarajiwa kumchagua Katibu wa Wizara ya Utalii, Bi Safina Kwekwe kuwa mgombea mwenza wake.

Kwa upande mwingine, Bw Dena ambaye itakuwa mara yake ya tatu kuwania ugavana Kwale anaungwa mkono na Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chama cha KANU.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba kuna uwezekano Bi Achani hataki kutangaza chama atakachotumia 2022 kwa sababu pia huwa ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta, kando na jinsi alivyokuwa karibu na naibu rais awali.

You can share this post!

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru aagizwa kufika Kortini

Pande zote zakubaliana kumsukuma Bashir ICC