Makala

Mwasisi wa Ekeza afafanua maswala kadha

March 2nd, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

HUENDA ujipate ukimsaidia Kasisi David Kariuki Ngare na Sh2 bilioni kufufua kampuni yake ya Ekeza Sacco ambayo iliripotiwa na serikali kuwa inaanguka kupitia wizi wa pesa za wateja wake.

Zimeenea habari kwamba kasisi huyu alijinufaisha kwa kujipa Sh1.5 bilioni za wateja wake kwa njia ya magendo.

Hata hivyo, Kasisi Ngare ambaye pia ni mwanzilishi na Mhubiri mkuu wa Kanisa la Chosen Calvary centre lililoko katika mtaa wa Kiandutu Mjini Thika sasa anaitaka serikali impe mkopo wa Sh2 bilioni ili afufue Ekeza Sacco.

Anasema kuwa kampuni hiyo ina umuhimu mkuu katika kuafikia ajenda nne kuu za Rais ambazo ni utoshelevu wa chakula, afya kwa wote, uimarishaji wa viwanda na pia kuafikia manyumba ya makazi kwa wote.

Anasema kuwa ana wateja 45,000 ambao kwa sasa hawana uwezo wa kupata pesa zao kutoka akaunti za Ekeza.

“Serikali ilisimamisha leseni yetu ya kufanya kazi kwa muda, ikatangaza hadharani kuwa tulikuwa tunafilisika na ikatutwika mzigo mkuu wa kuyumba kufuatia kutupotezea imani ya wateja,” anadai Kasisi Ngare.

Kasisi Ngare anashikilia kuwa ikiwa serikali ilitekeleza wajibu wake kwa ueledi na ustaarabu wa kimaadili, kampuni ya Ekeza haingeporomoka “kiasi cha kujumuika miongoni mwa matapeli wa utajiri wa Wakenya.”

Akiwa pia ni mshauri mkuu wa kiuchumi katika serikali ya Kaunti ya Kiambu, Bw Ngare anasema kuwa sasa serikali imetangaza kuwa itauza mali yake katika mnada wa hadhara.

“Sikatai, lakini ni lazima nihusishwe kikamilifu. Sitaki utokee ukora wa baadhi ya maafisa wa serikali kung’ang’ania mali yangu kwa msingi kuwa inasaka pesa za kuwalipa wanaotudai,” asema.

Kasisi Ngare anateta kuwa masuala ya Ekeza hayakuwa na hatari kubwa kwa wateja wake bali serikali ndiyo “iliingilia katika biashara yetu na bila kuzingatia upande wetu wa kujitetea” ilikimbia hadharani “kutuangazia kama matapeli”.

Anasema kuwa pesa ambazo ripoti ya serikali ilimwangazia kama aliyepora ni Sh1.5 bilioni za wawekezaji.

“Hawa walioandaa ripoti hiyo walikosa kuwafahamisha Wakenya kuwa mimi nilikopa kama mwanachama wa Sacco hii. Walisema kuwa mimi nilijipa pesa za Ekeza lakini hawakuwaambia Wakenya kuwa ndio nilijipa mkopo huo, lakini kabla ya kutuanza kutuhangaisha, nilikuwa nimelipa Sh400 milioni za mkopo huo na sikuwa na deni katika mkataba wa maelewano
katika masharti ya mkopo huo,” akasema.

Alisema kuwa Ekeza na kampuni ya Gakuyo Real Estate zina uhusiano wa moja kwa moja ambapo wateja wa Gakuyo ndio wateja wa Ekeza na ambao wakiweka akiba, walikuwa aidha wakinunuliwa mashamba au
rasilimali zingine.

Mnamo Desemba 17, 2018 Kamishna wa vyama vya ushirika, Bi Mary Mungai aliunda kamati ya kuchunguza muundo wa kibiashara wa Ekeza kwa nia ya kuafikia maamuzi ya kurejeshewa au kunyimwa leseni.

Kwa mujibu wa Bi Mungai, shida kuu ya Ekeza ilikuwa katika upanuzi wake ambapo licha ya kuwa na leseni ya kuhudumu katika eneo la Starehe jijini Nairobi, kampuni hiyo ilipanua harakati zake hadi katika zaidi ya Kaunti 10 hapa nchini.

Pia, Ekeza ikawa na kampuni ya kando na ambayo ni ile ya ununuzi na uuzaji wa vipande vya ardhi ya Gakuyo Real Estate na ambapo hakuna rekodi za utendakazi zilikuwa zikiandaliwa kwa serikali kwa mujibu wa mwongozo wa vyama vya ushirika, hali ambayo ilizua changamoto kuu ya kupokonywa leseni kwa muda.

Kupokonywa leseni kulizindua misururu ya washirika wa uwekezaji kuanza kutoa pesa zao kwa akaunti na ambapo shida za kifedha ziliandama Ekeza kwa kasi kiasi cha kuzama.

“Lakini hali bado inaweza ikalainishwa. Katika Ekeza, tulikuwa na hifadhi ya Sh2.5 Bilioni za wateja lakini katika misukosuko iliyojiri, wanachama wengine wakatoa Sh500 milioni kutoka akaunti zao na hivyo basi tukajipata bila uthabiti wa uwekezaji,” akasema Kasisi Ngare.

Huku wanachama wengine wakizidi kusukuma warejeshewe pesa zao, Ekeza imelipa Sh116 milioni lakini katika Kampuni ya Gakuyo Real Estate kukiwa na mikataba ya mikopo ya Sh1.3 bilioni.

“Hali hii inakuonyesha waziwazi kuwa tuko na changamoto ndio, lakini pia tuko na uthabiti wa kimsingi…Changamoto kuu ni kuwa majina ya Kampuni zetu yameharibiwa sifa mitandaoni kiasi kwamba hata kupata mwekezaji wa kushirikiana naye kumekuwa na ugumu,” akasema Kasisi huyo.

Hata hivyo, alisema kuwa ako na matumaini kuwa mambo yatalainika baada ya kuonyesha wateja wake kuwa hakuna nia yoyote ya kuzamisha akiba zao.

Tegemeo lake kuu katika harakati hizo ni serikali impe ufadhili wa pesa hizo ili azime kilio cha wanaodhania watapokonywa pesa zao na awe na uthabiti wa kuendelea kuokota pesa za mikopo kutoka kwake na wateja wengine ambayo kwa ujumla ni ya Sh1.3 bilioni.

“Tukiwa katika biashara, tutaweza kujinyanyua. Lakini katika hali hii ambapo serikali ndiyo inachochea mambo, itakuwa ngumu sana kuwajibikia shida hizi zetu. Lakini cha maana kuelewa ni kuwa, hakuna nia yoyote ya kuwapokonya wateja wetu pesa zao,” akasema.