Mwatate United yaendelea kuimarika

Mwatate United yaendelea kuimarika

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

MWATATE United FC iliendelea kuwika na kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kuibuka washindi wa Supaligi ya Taifa ilipoilaza Fortune Sacco FC kwa bao 1-0 kwenye mechi kali iliyotitigwa uga wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi, Jumatano.

Mwatate ilijipatia bao la ushindi dakika ya tatu ya majeruhi kupitia kwa Cornelius Juma. Katika mechi hiyo, wageni hao wa Fortune walibidi wacheze mchezaji mmoja mpungufu kutoka dakika ya 22 wakati Brian Mandela alipooyeshwa kadi nyekundu alipopewa kadi ya pili ya njano.

Timu hiyo ya Mwatate ambayo inashiriki kwenye ligi hiyo kwa mara ya kwanza sasa imezipiku timu nyingine mbili za jimbo la Pwani, Coast Stima na Modern Coast Rangers FC kwani iko nafasi ya tano ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 16.

Stima iko kwenye nafasi ya 10 ikiwa na pointi 22 kutokana na mechi 15 hali nayo Rangers kwenye nafsi ya 13 ikiwa na pointi 19.

Katika mchezo uliochezwa Jumatano, Coast Stima ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Kenya Police kutoka Nairobi uliofanyika uwanja wa Mbaraki Sports Club. Stima ilistahili kushinda pambano hilo lakini Police ilijipatia bao la kusawazisha dakika mbili za majeruhi.

Mabao ya Stima yalifungwa na Clinton Ochieng dakika ya 30 na Khamis Abudu dakika ya 65 hali wafungaji wa mabao ya Police walikuwa Clinton Kinanga dakika ya 37 na Eliakim Nyang’a dakika ya 92.

You can share this post!

BIG 3 COAST LADIES TOURNAMENT: MTG United yajiondoa dimba...

Corona ilivyomsaidia kuvuta wateja wa nyama