Habari

Mwathethe ateuliwa mwenyekiti wa KenGen

November 5th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali (Mstaafu) Samson Mwathethe ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa kampuni ya kuzalisha umeme nchini, KenGen.

Mwathethe anachukua pahala pa Joshua Choge ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Choge alivuliwa wadhifa huo katika Mkutano Mkuu wa 67 wa Kila Mwaka (AGM) wa Bodi ya KenGen uliofanyika Jumanne.

Kwenye taarifa, bodi ya kampuni hiyo ya uzalishaji umeme ilisema Jenerali anailetea tajriba kubwa ya uongozi ambayo ameipata kwa miaka mingi akihudumu jeshini.

“Chini ya uongozi wa Jenerali Mwathethe, KenGen imejitolea kuimarisha uhusiano wake na wadau huku tukiendelea kushughulikia mahitaji mapya ya kibiashara yanayoendana na ukuaji wa kiteknolojia na kijamii,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa KenGen Rebecca Miano.

Mwathethe alistaafu kutoka jeshini mnamo Mei 2020 na Rais Uhuru Kenyatta akamteua Jenerali Robert Kibochi kuchukua nafasi hiyo.

Akiwa jeshini Mwathethe amewahi kushikilia nyadhifa kama vile Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji miongoni mwa vyeo vingine.