Mwaura arejea rasmi kama Seneta Maalum

Mwaura arejea rasmi kama Seneta Maalum

Na CHARLES WASONGA

BW Isaac Mwaura Jumatano alipokelewa tena rasmi katika Seneti kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kufutilia mbali hatua ya chama cha Jubilee kumfurusha.

Spika wa Seneti Ken Lusaka alitaja uamuzi huo wa mahakama alipomkaribisha Bw Mwaura na kumruhusu kushiriki shughuli za bunge hilo.

“Mahakama Kuu ilifutilia mbali Notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali nambari 4597 ya Spika wa Seneti ambaye alitangaza kuwa wazi kwa nafasi ya seneta maalum na hivyo kumpokonya Isaac Mwaura nafasi yake kama Seneta Maalum,” akasema Bw Lusaka.

“Vile vile, uamuzi huo wa mahakama kuu uliondoa Notisi ya Gazeti Rasmi nambari 4598 ya Mei 11, 2021 ya mwenyekiti wa IEBC iliyomteua Bw Sammy Prisa Leshore kuchukua mahala pa Isaac Mwaura kama Seneta Maalum anayewakilisha watu wanaoishi na ulemavu (PWDs). Kwa hivyo, naamuru kwamba Isaac Mwaura Maiga asalie kuwa Seneta Maalum kulingana na Katiba ya Kenya na Sheria za Seneti,” akaongeza Spika Lusaka.

Bw Mwaura alisindikizwa katika ukumbi wa Seneti na wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Wao ni maseneta maalum Naomi Waqo na Falhada Iman Waqo na Seneta wa Bomet Christopher Langat.

Bw Mwaura alipoteza kiti chake mapema mwaka huu 2021 alipofurushwa na chama cha Jubilee.

Jopo la kutatua mizozo katika vyama vya kisiasa lilidumisha uamuzi huo, hatua ambayo ilipelekea Bw Mwaura kusaka usaidizi katika Mahakama Kuu.

Chama cha Jubilee kilimteua aliyekuwa Seneta wa Samburu Sammy Leshore kujaza nafasi ya Bw Mwaura.

Hapo ndipo mwanasiasa huyo aliwasilisha kesi mahakamani kutaka uamuzi huo ubatilishwe.

You can share this post!

Wanaotaka kumrithi Uhuru wafuatilia hotuba yake bungeni

Donnarumma atawazwa Kipa Bora Duniani

T L