Habari za Kitaifa

Mwekezaji katika eneo la mlipuko wa gesi azungumza kupitia mawakili wake

February 3rd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MWEKEZAJI Derrick Kimathi anayehusishwa na mlipuko wa gesi uliotokea Mradi, Embakasi, Kaunti ya Nairobi mnamo Alhamisi na ukasababisha vifo vya watu watatu huku mamia ya wengine wakijeruhiwa, sasa anadai hakuhusika na janga hilo.

Amesema kwamba licha ya kumiliki sehemu ambapo mlipuko huo ulitokea na kusababisha hasara ya watu kupoteza maisha, mali haikuwa yake.

Kupitia taarifa ya mawakili wake wawili–Bw Wandugi Karathe na Bi Nancy Mukabana– mwekezaji huyp alisema kwamba kinyume na dhana ambayo imeundwa kupitia vyombo vya habari na pia matamshi ya wanasiasa, yeye ni mwathiriwa sawa na wengine.

Mawakili Bw Wandugi Karathe (kulia) na Bi Nancy Mukabana. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alisema kwamba hana biashara ya gesi na iliyolipuka ilikuwa imebebwa na lori ambalo “dereva alipitia kwangu bila idhini na hadi sasa ninashirikiana na polisi kumtia mbaroni”.

Aliongeza kuwa kinyume na taswira ambayo imeundwa kwamba yeye huwa na uwekezaji wa kuuza gesi ya mitungi ya kutumika kwa kutoa kawi ya upishi, hadi wakati wa mlipuko huo kutokea, alikuwa akiendesha biashara ya karakana ya kuunda magari.

“Ni kweli kwamba mimi nilikuwa kwa wakati mmoja nimeomba leseni ya kushiriki mauzo ya gesi ya kujaza mitungi lakini serikali ikakataa kunipa. Niliachana na mambo hayo na hadi sasa, nimekuwa katika biashara ya uchukuzi na kuunda magari,” akasema Bw Kimathi.

Alisema kwamba hata yeye anaomboleza hasara iliyotokana na mkasa huo wa moto.

“Aidha, hata hayo mauti yaliyozuka pamoja na majeruhi yamenisononesha si haba. Pia, mimi nimeumizwa na kusambazwa kwa dhana kwamba mimi ni mhalifu wa kusababisha mauti. Ningependa nieleweke kwamba mimi ni mtiifu wa sheria na habari zozote za kuniangazia kama mkora zinanipa huzuni,” akasema.

Bw Kimathi aliwataka wote wazipee taasisi za serikali muda na nafasi ya kutekeleza uchunguzi ambao utaweka ukweli wazi.

[email protected]