Habari Mseto

Mwende Mwinzi asilazimishwe kutupa uraia wa Amerika – mahakama

November 14th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imeamua kwamba balozi mteule wa Kenya nchini Korea Kusini, Mwende Mwinzi hawezi kulazimishwa kutupa uraia wa Amerika alioupata kwa kuzaliwa.

Imefikia uamuzi huo huku ikipinga wasilisho la Mwinzi alilowasilisha Februari kutaka asasi ya bunge isitishwe kumshurutisha atupe uraia wa Amerika kabla ya kupata kazi hiyo.

Jaji James Makau wa Kitengo cha Masuala ya Kikatiba na Haki za Kibinadamu amesema wasilisho lake linakuja mapema kwa sababu mchakato wa uteuzi ulikuwa haujakamilika.

“Uteuzi ni wajibu wa ofisi ya Rais na asasi ya bunge kuamua,” amesema Jaji Makau.

Hata hivyo, Jaji amesema balozi si afisa wa serikali na hivyo halazimishwi kutupa uraia mwingine.

“Katika hitaji la uraia wa mataifa mawili , ofisi ya balozi haijaorodhrshwa kama ya serikali,” Jaji ameamua.

Hata hivyo, amesema ikiwa ni ya serikali, bado kifungu 78(3)b cha Katiba kinamlinda mtu.

Mwinzi aliwakilishwa na wakili Prof Tom Ojienda.