Mwendwa aahidi kuongea na FIFA kuondoa marufuku

Mwendwa aahidi kuongea na FIFA kuondoa marufuku

NA RUTH AREGE

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kenya Nick Mwendwa amefichua kuwa, wakati wowote kutoka sasa Kenya itaachiliwa huru kushiriki mechi za kimataifa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya kurejea ofisini rasmi hapo jana Jumanne.

Mwendwa aliongoza Makamu wa Rais wa FKF Doris Petra, Katibu Mkuu Barry Otieno Mkuu wa Uadilifu wa FKF Michael Kamure miongoni mwa viongozi wengine ambao waliongoza ufunguzi wa jumba hilo.

Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya jengo la Goal Project, Mwendwa ameahidi kufufua soka ya Kenya.

“Baada ya kurejea ofisini siku zijazo tutafanya mambo haraka turudi uwanjani tucheze soka yetu. Soka ya kimataifa ambayo inatambulika na FIFA itarejea kawaida. Wakati wowote wiki hii tutawandikia FIFA barua ya kuwaeleza kuwa tumetii maagizo yao,” alisema Mwendwa.

“Hii leo tutakuwa na kikao na viongozi wa vilabu. Ijumaa tutakuwa na kikao kingine na Kamati Kuu ya Kitaifa ya Wanachama wa FKF (NEC) kuzungumza kuhusiana na msimu ujao. Tunataka soka yetu irejelee ukawaida wake,” aliongezea Mwendwa.

Kuhusiana na kuanza msimu mpya wa 2022/23 wa ligi kuu wikendi ijayo, Mwendwa amewasuta viongozi waliokuwa wanaendesha soka tangia kutimuliwa kwake.

“Soka ambayo inatambulika na FIFA ni soka ambayo inaendeshwa na FKF halali. Vijana warejee uwanjani na mwezi mmoja kutoka sasa ligi itaanza rasmi. Ninaomba viongozi wa klabu kuanzia ligi kuu hadi klabu za mashinani kujiandaa vilivyo,” aliongezea Mwendwa.

“Ninataka kumshukuru kwa dhati rais William Ruto kwa kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha soka inarejea katika hali yake ya kawaida. Soka yetu imeharibiwa na watu waliokuwa wakisimamia soka msimu uliopita,” aliongezea Mwendwa.

Jumba la Goal Project, Kandanda House huko Kasarani, lilifungwa zaidi ya miezi 10 baada ya Katibu wa Baraza la Mawaziri la Michezo Balozi Amina Mohamed kuwatimua viongozi wa FKF ofisini.

Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kenya Nick Mwendwa (kati) akizungumza na wanahabari alipoingia katika Kandanda House jijini Nairobi mnamo Septemba 20, 2022. PICHA| RUTH AREGE

Pamoja na Wanachama wengine Mwendwa alifukuzwa ofisini mnamo Novemba 11, 2021 na Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohamed baada ya ukaguzi wa hesabu za pesa za shirikisho zilizodaiwa kutumika vibaya.

Akiwa ameshtakiwa kortini kwa makosa manne ya ulaghai, Mwendwa – katika barua ya Novemba 29 iliyotumwa kwa NEC ya FKF – alisema alihamisha majukumu yake kwa naibu wake Petra huku akitaka kusafisha jina lake.

Mohamed aliteua Kamati ya kuendesha Soka nchini kwa kipindi cha awali cha miezi sita kabla ya kubadilika na kuwa Kamati ya Mpito.

Amina aliongeza muda wa Kamati ya Mpito kwa miezi miwili mnamo Agosti 16, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Kiambiu-Salem: Timu ya mashabiki wa Ingwe tawi mojawapo la...

Ukraine yashtumu Urusi kwa kulenga kituo cha nyuklia

T L