Mwendwa aponea ila hatarejea afisini FKF

Mwendwa aponea ila hatarejea afisini FKF

RICHARD MUNGUTI na JOHN ASHIHUNDU

MKURUGENZI wa mashtaka ya umma (DPP) hakumfungulia mashtaka rais wa shirikisho la kandanda nchini (FKF) Nick Mwendwa ya ubadhirifu wa pesa jana kama alivyoagizwa na mahakama wiki iliyopita.

Sasa Mwendwa yuko huru lakini haimaanishi atarudi kuendeleza shughuli za FKF ambazo sasa zinasimamiwa na kamati iliyoteuliwa na waziri wa michezo Amina Mohamed.Kamati hiyo inaongozwa na Jaji (mstaafu) Aaron Ringera.

Hakimu mwandamizi Wandia Nyamu alielezwa polisi wanaendelea na uchunguzi na hatma ya Mwendwa itategemea ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka.Hakimu aliamuru dhamana ya pesa tasilimu ya Sh4 milioni arudishiwe Mwendwa.

Kesi hiyo ilipotajwa jana DPP kupitia wakili wa Serikali Everlyne Onunga aliomba kesi aliyowasilisha kortini dhidi ya Mwendwa ifungwe kwa kwanza ili polisi waendelee na uchunguzi.“Sijawasilisha mashtaka dhidi ya Mwendwa kama nilivyoagizwa wiki iliyopita.

Naomba mahakama ifunge kesi niliyowasilisha nikiomba polisi wapewe muda wa siku 14 kukamilisha uchunguzii wa matumizi ya pesa dhidi ya Mwendwa,” Onunga alieleza korti.Nyamu aliamuru DPP wiki iliyopita amshtaki Mwendwa katika muda wa siku saba la sivyo aachiliwe huru.

Onunga alieleza mahakama polisi wataendelea kumchunguza Mwendwa na wakipata ushahidi watamfungulia mashtaka.Nyamu alifunga kesi hiyo lakini haimaanishi kwamba “Mwendwa atarudi katika afisi za FKF kuendeleza masuala ya kandanda nchini.

”Kamati ya Ringera inataka klabu zote nchini zitimize sheria ya Michezo kulingana na Katiba ya 2013.Ringera alisema timu zitaanza kuona jinsi michezo ilivyo maarufu duniani, mbali na kuwa biashara kubwa sana duniani.

Katika kuzingatia sheria hiyo, timu zitahakikisha kuwa wale wanaowekeza pesa zao wanaona thamani ya uwewekezaji wao na kujipatia fedha au faida kusaidia wahusika, wakiwemo wachezaji kama ilivyo katika mataifa mengine yanayozingatia sheria kama hiyo.

Sheria hii kadhalika itawafahamisha wanachama muda wa viongozi kukaa madarakani na namna ya mapato na matumizi ya fedha na rasilimani za shirika na jinsi ya kutatua mizozo ya mara kwa mara, ikizingatiwa kwamba viongozi ndio nguzo imara ya maendeleo na mafanikio ya shirika lolote.

Kadhalika kulingana na sheria hiyo, wanachama watakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu shirika lao, kinyume na ilivyo sasa kwa mashirika mengi ya michezo nchini.Katika hali hii, shirika litatambulika kuwepo na kufanya shughuli zake katika sehemu husika.

Sheria ya Michezo (2013) zinakubalia tu mashirika ya michezo kujiandikisha kama klabu ya michezo, shirika la michezo kwenye kaunti au shirika la kitaifa la michezo.Kadhalika kamati hiyo ya Aaron Ringera inazitaka klabu hizo kuchagua viongozi ambao ni raia wa Kenya.

Agizo ambalo linalenga kuzuia raia wa kigeni kupenya mashirika ya michezo nchini, kama Elly Kalekwa ambaye ndiye mmiliki wa klabu ya Sofapaka.Klabu 17 kati ya 18 zilizohudhuria mkutano huo katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo Jumatano pia zikubaliana na kamati hiyo ya muda pendekezo la kurejelewa kwa ratiba ya mechi za ligi kuu hapo Disemba 4.

Klabu hizo zilikubali kushirikiana na kamati ya Ringera huku zikiunga kono hatua ya Waziri wa Michezo Amina Mohamed kuvunjilia mbali afisi kuu ya Nick Mwendwa kufuatia madai ya ufisadi.Mwanachama wa kamati hiyo, Ali Amour alisema mkutano huo ulijadili kwa kirefu mbinu za kuboresha kandanda nchini kuanzia mashinani.

Ringera alikubaliana na klabu ligi kuu irejelewe Disemba 4 ili kuwe na uwazi katika usimamizi wao.Amour alisema klabu zitakazofuata ushauri wa kama hiyo zitanufaika kwa kuvutia wadhamini ambao wanapenda uwazi.Kamati ya Ringera kadhalika imepanga kukutana na wadhamini wanaofadhili ligi mbali mbali nchini pamoja na marifarii wanaendesha mechi za ligi.

Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi- Amina Mohamed aliteua kamati ya muda kusimamia shughuli za kandanda kwa miezi sita, lakini Fifa imesisitiza kwamba Kenya itapigwa marufuku kushiriki katika mashindano yoyote ya kimataifa iwapo Serikali haitarejesha ofisini Mwendwa na kamati yake.

You can share this post!

Afueni Rudisha akifanyiwa upasuaji na kutangaza atarejea...

Shujaa mawindoni kulipiza kisasi Dubai 7s msimu mpya...

F M