Michezo

Mwendwa kikaangioni kuhusu mamilioni ya Afcon 2019

May 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa alishinda katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) mnamo Alhamisi ya Mei 21, 2020, akihojiwa kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya fedha.

Mwendwa aliwasili katika afisi za DCI zilizopo kwenye Barabara ya Kiambu mnamo saa tatu asubuhi akiwa ameandamana na naibu wake Doris Petra na Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

Mwenda alihojiwa kuhusu namna FKF ilivyotumia Sh244 milioni ambazo zilitolewa na serikali mwaka uliopita kwa minajili ya kuiandaa timu ya taifa ya Harambee Stars kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Misri.

Matokeo ya uchungizi wa DCI yatawasilishwa baadaye kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atakayetathmini iwapo Mwendwa na FKF wana kesi ya kujibu au la.

Mwishoni mwa mwaka jana, gazeti la Nation Sport lilifichua jinsi ambavyo Mwendwa, Petra, aliyekuwa Katibu Mkuu wa FKF Robert Muthomi na baadhi ya maafisa wa Kamati Kuu ya FKF walijipa marupurupu ya hadi Sh50,000 kwa siku wakati wa kampeni za AFCON nchini Misri.

Katibu wa zamani wa Wizara ya Michezo, Kirimi Kaberia aliwahi kujitokeza na kutaka FKF kuwajibikia matumizi ya fedha hizo.

Bonasi

Kuhojiwa kwa Mwendwa kunafanyika siku chache baada ya nahodha wa Stars, Victor Wanyama kuthibitisha kwamba wanasoka wa timu ya taifa ya Kenya bado hawajapata bonasi walizoahidiwa kwa ushindi wa 3-2 waliousajili dhidi ya Tanzania katika mechi ya awamu ya makundi AFCON 2019.

Mwendwa ambaye alichaguliwa Rais wa FKF mnamo 2016, anamulikwa pia kutokana na ombi la Sh4 milioni lililowasilishwa na FKF kwa Wizara ya Michezo wakati Stars walipokuwa wakijiandaa kwa mechi dhidi ya Misri katika juhudi za kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 zitakazoandaliwa nchini Cameroon.

Mechi hiyo ya ufunguzi ya Kundi G kati ya Kenya na Misri ilichezewa mjini Alexandria mnamo Novemba 2019 na kumalizikia kwa sare ya 1-1.

Jingine ambalo Mwendwa alihojiwa kwalo ni kuhusu hatima ya basi la Sh125 milioni ambalo lilinunuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa minajili ya kuchangia maendeleo ya soka ya Kenya kupitia matangazo ya nje (OB). Basi hilo bado halijawasilishwa kufikia sasa.

Matukio yanayomzingira Mwendwa na FKF yanafichuka wakati ambapo ulingo wa soka unakabiliwa na suitafahamu tele baada ya uchaguzi wa FKF katika ngazi ya kaunti na kitaifa kufutiliwa mbali mara mbili na Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT).

FKF inachunguzwa pia kwa kushindwa kuwalipa makocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouche, Bobby Williamson na Sebastien Migne ambao kwa pamoja, wanadai kima cha Sh170 milioni.

Baada ya FKF kushindwa kulipa deni la Amrouche mwezi wa Aprili, Mwendwa shirikisho liko tayari kwa adhabu kali itakayotolewa na FIFA dhidi ya Kenya.

FKF iliamrishwa na FIFA kumlipa Amrouche ambaye ni raia wa Algeria na Ubelgiji kima cha Sh109 milioni kwa kosa la kukiuka masharti ya mkataba wake alipotimuliwa mnamo Agosti 2014.

“Tumetalii njia na mbinu zote za kupata fedha hizo bila mafanikio. Tumejaribu pia kuhusisha serikali lakini kwa sasa inaelekeza juhudi zote katika vita vya kukabiliana na janga la corona. Haitawezekana kwa Amrouche kulipwa,” akatanguliza Mwendwa.

“Tunasalia sasa kusubiri maamuzi ya mwisho ya FIFA. Iwapo watatupiga marufuku ya kushiriki mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022, basi ni sawa. Haitakuwa mwisho wa dunia au maisha. Tutasubiri wakati mwingine, labda 2026 sasa,” akaongeza Mwendwa.