Habari Mseto

Mwenye gari lililomuua mhariri wa NTV ajitetea

March 30th, 2020 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa gari lililomgonga na kumuua mhariri wa video katika kituo cha televisheni cha NTV Raphael Mutuku Nzioki alishtakiwa Jumatatu katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Stephen Kirumba Njoroge (aliye kati ya maafisa wa polisi pichani) alishtakiwa mbele ya hakimu mkazi Bi Martha Nanzushi katika mahakama ya trafiki.

Alikanusha mashtaka matatu ya kuruhusu gari kuhudumu kama haijalipiwa bima. Alikabiliwa na shtaka lingine la kuruhusu gari mbovu kubeba abiria na kutoweka na rekodi ya dereva wake.

Dereva wa gari hilo la Njoroge alitoroka baada ya kusababisha ajali hiyo mnamo Machi 7, 2020.

Wakili Kinyua Machina anayemwakilisha Njoroge. Picha/ Richard Munguti

 

Kupitia kwa wakili Kinyua Machina mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana. “Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana,” Bw Machina akasema.

Bw Machina alinweleza hakimu amwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu kwa vile uchumi umeathiriwa na ugonjwa wa Covid-19.

“Hii nahakama inafahamu jinsi biashara zilivyoathiriwa na maradhi ya Corona virus. Wakenya wanakaa kwa nyumba. Gari la mshtakiwa lilitwaliwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central baada ya dereva kutoroka.m,” Machina alimweleza hakimu Nanzushi.

Hakimu mkazi Martha Nanzushi. Picha/ Richard Munguti

Pia wakili huyo alieleza korti mshtakiwa atasaidia polisi kumtafuta dereva huyo aliyetoroka ashtakiwe.

Akitoa uamuzi aa dhamana, Bi Nanzushi alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh100,000 pesa tasilmu.

Pia alimwamuru mshtakiwa amfikishe mahakami mdhamini mmoja atakayeapa kwamba atahakikisha mshtakiwa amefika kortini kila wakati anapohitajika.

Kesi itatajwa Aprili 30 kwa maagizo zaidi.