Mwenye kilabu alikofia mbunge wa zamani George Thuo kuanza kujitetea ‘Siku ya Wapendanao’

Mwenye kilabu alikofia mbunge wa zamani George Thuo kuanza kujitetea ‘Siku ya Wapendanao’

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kilabu cha Porkies pamoja na wafanyakazi wake watano wanaoshtakiwa kwa mauaji ya aliyekuwa Mbunge wa Juja George Thuo miaka 10 iliyopita wako na kesi ya kujibu.

Akitoa uamuzi huo Jaji Roselyne Korir alisema baada ya kuchambua ushahidi wote amefikia uamuzi “kuna ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuwaweka kizimbani washtakiwa wote kujitetea.”

Jaji Korir alisema mwenye kilabu cha Porkies Paul Wainaina Boiyo almaarufu Sheki na wafanyakazi Christine Lumbazio Andika almaarufu Lumba, Andrew Karanja Wainaina, Samwel Kuria almaarufu Visi, Esther Ndinda Mulinge na Ruth Watahi Irungu almaarufu Atlanta wataanza kujitetea Februari 14, 2023.

Uamuzi huo uliwashtua mawakili wenye tajriba ya juu Dkt John Khaminwa na Cliff Ombeta, Pareno Solonka na Gedion Solonka.

“Hatukutarajia uamuzi wa hii mahakama utakuwa hivi. Umetushtua kabisa,” Dkt Khaminwa anayemwakilisha Boiyo alimweleza Jaji Korir.

Sita hao wanakabiliwa na shtaka la kumuua Thuo mnamo Novemba 17, 2013 katika kilabu cha Porkies kilichoko mjini Thika.

Viongozi wa mashtaka Gikui Gichuhi na Tabitha Ouya waliita mashahidi 30 katika kesi hiyo ya mauaji ya Thuo, aliyekuwa kiranja wa Bunge.

Mawakili Cliff Ombeta na Dkt John Khaminwa walieleza mahakama kwamba washtakiwa wote watajitetea wakiwa upande wa mashahidi ili wahojiwe na kiongozi wa mashtaka.

Sita hao walikanusha kumuua Thuo wakisema alikuwa mteja wao mashuhuri.

Ushahidi uliowasilishwa kortini ulisema Thuo aliwekewa sumu kwa kinywaji na hata hakukaa muda mrefu kabla ya kufariki.

Jaji Korir aliwaamuru washtakiwa watakaojitetea wakiwa upande wa mashahidi wawakabidhi viongozi wa mashtaka nakala za ushahidi wao ujiandae kuwahoji kwa undani.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana.

Mashahidi waliofika kortini walieleza jaji siku ile Thuo aliaga dunia, alikuwa amefika katika kilabu cha Porkies akitoka nyumbani kwake.

Baada ya kukaa muda mfupi alianza kulalamika anahisi joto kisha akazirai na alipofikishwa hospitalini, tayari alikuwa amefariki.

Awali walikuwa na mkewe na Kasisi Dominic Wamuguda akijaribu kuwapatanisha baada ya mzozo baina yao.

Thuo na mkewe walikuwa wametembelea eneo la Kitengela na aliporudi nyumbani alipewa kinywaji kisha akaondoka kwenda Porkies ambapo alifariki baada ya muda mfupi.

Washtakiwa walikataa madai kwamba walimtilia sumu Thuo kwenye kinywaji.

Dkt Andrew Gachii aliyemfanyia upasuaji Thuo alisema alifariki kutokana na sumu iliyowekwa kwenye chakula au kinywaji.

  • Tags

You can share this post!

Spika Wetang’ula aharamisha kanuni ya CBK ya...

Newcastle pua na mdomo kuingia fainali ya Carabao Cup baada...

T L