Habari za Kitaifa

Mmiliki wa lori la gesi iliyosababisha vifo vya watu 10 Embakasi, azuiliwa siku 14

February 15th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa lori la kubeba gesi lililolipuka katika eneo la Mradi, Embakasi, Nairobi na kusababisha vifo vya watu 10 na kuwajeruhi 600 atazuiliwa kwa siku 14.

Mahakama imeagiza Bw Abraham Mwangi Nguyo kukaa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill kwa siku hizo 14.

Bw Nguyo atarudishwa tena kortini Februari 28, 2024, wakati mmiliki wa kiwanda hicho cha gesi cha Maxxis Energy Nairobi Limited Derrick Kimathi na washukiwa wengine watatu watakapofikishwa kortini.

Kufikia sasa, watu watano wamekamatwa kufuatia mkasa huo uliotamausha wengi.

Mbali na Bw Nguyo na Bw Kimathi, washukiwa wengine waliokamatwa ni maafisa katika Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira Nchini (Nema) Mabw Joseph Makau, David Warunya On’gare, na Bi Marrian Mutete Kioko.

Akiomba Bw Nguyo azuiliwe kwa siku 14 kiongozi wa mashtaka James Gachoka alimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Nanzushi kwamba wachunguzi watasafiri hadi nchini Tanzania kuhoji mamlaka ya nchi hiyo kuhusu usafi wa gesi iliyonunuliwa na Bw Nguyo kutoka nchini humo.

Bw Gachoka alieleza Bi Nanzushi kwamba mshukiwa ndiye mmiliki wa lori lililolipuka na kusababisha maafa hayo.

“Tangu usiku wa Februari 1 na mapambazuko ya Februari 2, 2024, mshukiwa huyu alitoroka na kujificha,” akasema Bw Gachoka.

Alidokeza kwamba polisi walimtia nguvuni Bw Nguyo mnamo Februari 12, 2024, na kumzuilia kumhoji.

Mahakama ilielezwa uchunguzi wa kina unahitajika kufanywa kubaini kilichosababisha mlipuko huo.

Akiwa mafichoni, hakimu Nanzushi alielezwa, mshukiwa huyo aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu kuomba aachiliwe kwa dhamana na kuagiza polisi wasimzuilie akijisalamisha.

Wakili anayemwakilisha Bw Nguyo alifichua kwamba alimpeleka mshukiwa huyo na kumsalimisha kwa afisi za Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) katika eneo la Embakasi.

Mahakama ilielezwa polisi wanachunguza kuona ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki washukiwa hao watano kwa mauaji.

Bw Nguyo ndiye mmiliki wa lori la kubeba gesi–Liquefied Petroleum Gas (LPG)–lenye nambari za usajili KBJ 185X na ZD2234 muundo wa Mercedes Benz.

Lori hili ndilo lililolipuka katika kiwanda cha Maxxis Energy Nairobi Limited cha kujaza mitungi na gesi ya kupikia.

Mahakama ilielezwa mlipuko huo ulisababisha maafa makubwa.

Inspekta Isaac Kariuki anayechunguza kesi hiyo amedokeza kuwa watu waliochomeka katika mkasa huo hawajafanyiwa upasuaji utakaoshirikisha uchunguzi wa vinasaba vya DNA.

Baadhi ya miili ilichomeka na kuungua kabisa, Bi Nanzushi alielezwa.

Pia Bw Kariuki alisema huenda kuna miili zaidi katika eneo la mkasa huo.