Mwenye nguvu nipishe Juve na Atletico wakivaana UEFA

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

UWANJA maarufu wa Wanda Metroplitano jijini hapa unatazamiwa leo Jumatano kujaa hadi pomoni wakati Atletico Madrid watavaana na miamba wa soka ya Italia, Juventus katika pambano la Kundi D la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Timu zote zina historia tofauti katika mapambano haya.

Ingawa hivyo, itakumbukwa kwamba majuzi zaidi Juventus waliwabandua nje Atletico Madrid katika raundi ya 16-bora ya michuano hii kutokana na mabao ya fowadi wao matata Cristiano Ronaldo aliyetokea Real Madrid.

Mbali na mashabiki wao kusubiri kwa hamu kuonja ushindi baada ya kushindwa na Real Sociedad mwishoni mwa wiki, kadhalika Atletico wanatarajiwa kulipiza kisasi cha UEFA dhidi ya vigogo hawa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Juventus kwa upande wao walitoka bila ya kufungana na Fiorentina mwishoni mwa wiki iliyopita na sasa wako nyuma ya Inter Milan ambao wameanza kampeni zao kwa matao ya juu baada ya kusajili ushindi mara tatu hadi kufikia sasa msimu huu.

Wenyeji watakuwa na lengo la kufufua ubabe wao katika michuano hii ya Ulaya baada ya kubanduliwa mapema katika mechi za hatua ya mwondoano katika miaka ya karibuni.

Klabu kutoka Italia zimekuwa zikiandikisha ushindi dhidi ya wapinzani wao wa Uhispania, matokeo yakiwa ushindi mara nne pekee katika jumla ya mechi 27 zilizopita.

Messi ataka kumuona Neymar akirudi Barcelona 

Wakati uo huo, staa Lionel Messi anasema “angependa sana nyota Neymar arudi Barcelona kwani kuwasili kwake kutawaongezea nafasi na tumaini la kuyafikia malengo yao.”

Neymar, 27, alijiunga na Paris St-Germain (PSG) kutoka Barcelona mnamo 2017 kwa ada ya rekodi ya dunia ya Sh25.8 bilioni.

“Alitamani sana kurudi,” Messi aliliambia gazeti moja la spoti nchini Uhispania. “Sijui kama klabu ilijaribu kweli kumsajili au la.”

Neymar alifunga jumla ya mabao 105 katika mechi 186 akivalia jezi za Barcelona kati ya 2013-2017, na ana mabao 51 katika jumla ya michuano 58 aliyoichezea PSG. Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil alihusishwa mara kwa mara na taarifa za kurudi Barcelona au kutua Real Madrid wakati wa muhula uliopita wa usajili, ingawa imedaiwa kwamba hakuna klabu yoyote ambayo ilishawishika kumsajili.

“Ningependa Neymar arudi,” alisema kiungo na nahodha wa Barcelona Messi, 32. “Ninaelewa watu hao ambao wanapinga kurudi kwake na inaeleweka kwa kile kilichotokea kwa ‘Ney’ na namna ambavyo aliondoka uwanjani Camp Nou.

“Lakini nikifikiria kuhusu kiwango cha mchezo wake, mimi binafsi nadhani Neymar ni mmoja wa wachezaji bora ulimwenguni,” akasema. Messi.

Habari zinazohusiana na hii