Michezo

Mwenyekiti wa Arsenal Sir Chips Keswick astaafu

May 29th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SIR Chips Keswick amestaafu kwenye uenyekiti wa Arsenal baada kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka saba.

Kinara huyo mwenye umri wa miaka 80 ambaye pia ni shabiki sugu wa tangu zamani wa Arsenal, amekuwa kwenye bodi ya usimamizi wa Arsenal tangu 2005 na akateuliwa kuwa Mwenyekiti mnamo 2013 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Peter Hill-Wood.

Arsenal wamesema hawawazii kwa sasa kujaza pengo la Keswick hasa ikizingatiwa ukubwa wa uwezo unaojivuniwa na wanachama wao wa sasa kwenye bodi ya usimamizi wakiwemo Stan na Josh Kroenke, Lord Harris na Ken Friar.

“Imekuwa tija na fahari tele kuwa mwenyekiti wa kikosi hiki cha haiba kubwa. Arsenal imekuwa sehemu muhimu sana ya maisha yangu na itasalia kudumu katika moyo wangu katika kipindi kizima cha uhai wangu,” akatanguliza Keswick.

“Nilifichua maazimio ya kustaafu kwangu kambini mwa Arsenal mwishoni mwa msimu huu. Hili ni jambo lililojulikana kwa wanachama wote wa bodi hata kabla ya ujio wa mlipuko wa virusi hatari vya homa ya corona,” akasema kwa kusisitiza kwamba anaacha Arsenal ikiwa salama mikononi mwa wamiliki wakuu – Stan na Josh, vinara wengine wa bodi na maafisa wakuu wa klabu.

“Najua kwamba Arsenal wataibuka na kurejelea ubora wao wa zamani. Si ajabu kwamba ufufuo huo hautachukua kipindi cha zaidi ya miaka miwili ijayo. Hilo ndilo tamanio la kila mmoja. Tuna wachezaji wenye kiu ya kusajili ushindi na kocha anaelewa falsafa ya Arsenal tangu zamani,” akaongeza.

Kwa upande wao, Stan na Josh Kroenke walisema: “Tunatoa shukran zetu kwa Keswick ambaye amejitolea kwa hali na mali kukitumikia kikosi cha Arsenal kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita akiwa mwanachama wa bodi kisha mwenyekiti. Uzoefu mpana alionao katika mawanda ya biashara na tajriba yake pevu katika masuala ya usimamizi yamemfanya kuwa miongoni mwa wenyeviti bora zaidi kuwahi kuhudumia Arsenal. Imekuwa tunu kubwa kufanya kazi naye.”

Chini ya uenyekiti wa Keswick, Arsenal walitia kapuni mataji matatu ya Kombe la FA na hawakuwahi kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) nje ya mduara wa vikosi sita-bora kileleni mwa jedwali.