Habari Mseto

Mwenyekiti wa MWA akejeli majigambo ya Matiang'i eti faini zimeizolea serikali mamilioni

November 22nd, 2018 2 min read

NA CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Muungano unaotetea Maslahi ya wenye Matatu (MWA) Dickson Mbugua amemkashifu vikali Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kwa kujigamba kuhusu kiasi cha faini serikali ilijizolea kwa kuwatoza wahudumu wa matatu waliokosa kuzingatia sheria za Michuki.

Bw Mbugua amemtaka Bw Matiang’I kutafakari kuhusu namna maafisa wake wanavyoendelea kuwanyanyasa wahudumu barabarani kwa kuwakamata na kuwashtaki kwa makosa madogo madogo ambayo hayaambatani na hitaji la sheria hizo za barabarani.

“Kabla Bw Matiangi hajajipiga kifua kuhusu kiasi kikubwa cha faini na idadi ya waliokamatwa na kuadhibiwa mahakamani, anafaa kutuambia amewafuta au kuwasimamisha maafisa wangapi wa polisi wanaoendelea kuhangaisha wahudumu wetu,” akasema Bw Mbugua katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Vile vile Mwenyekiti huyo veterani alimtaka Bw Matiang’i kuamuru magari yote yanayoendelea kuzuiliwa katika vituo vya polisi yaachiliwe ili yaweze kupelekwa katika vituo vya ukaguzi badala ya kuwahangaisha wamiliki wao na waziri kutisha kwamba serikali itayachukua na kuyatoa kwa kaunti mbalimbali.

Wakati uo huo Bw Mbugua aliwashtumu wamiliki wa magari na wenyeviti wa vyama vinavyosimamia magari hayo(saccos) kwa hatua yao ya kujiondoa kutoka Muungano wa Kitaifa wa Wamiliki wa Matatu akitaja hatua hiyo kama ya kibinafsi isiyowafaidi kivyovyote.

“Ingawa hawataki kusema kisasi chao ni kukosa kuteuliwa katika Chama cha Uchukuzi katika Sekta ya Umma (Federation of Public Transport Sector) ambacho kila muungano ulitakiwa uwakilishwe na watu wawili na wanaolalamika walikosa kuteuliwa kwenye nafasi hizo,”

“Kwa kuwa tuna miungano sita si kila mwanachama wa kila sacco angepata nafasi ya kuteuliwa ila wanafaa kuzua ushirikiano na waliopata nafasi ili kuboresha sekta ya uchukuzi wa umma,” akasema Bw Mbugua.

Hata hivyo aliwaondolea hofu wamiliki wa matatu yanayobeba abiria 25 na 33 akisema kwamba serikali inalenga kuyaondoa kabisa matatu yanayobeba abiria 14 na kuna sera inayoundwa ili watakaoathiriwa waweze kulipwa fidia.

“Ni kweli kwamba magari yanayobeba abiria 14 yataondolewa kwasababu zimepitwa na wakati na hakuna faida. Ila wote watakaoathiriwa watalipwa fidia baada ya magari yao kufanyiwa ukaguzi na thamani ya kuridhisha kuafikiwa,” akasisitiza Bw Mbugua.

Kulinagana naye mabasi mapya yatakayoletwa barabarani maarufu kama ‘BRT Buses’ yatafanya kazi katika barabara zitakazoorodheshwa na serikali wala hayataathiri usafiri wa magari mengine ya umma.