Makala

Mwihoko: Wakati mmoja ilikuwa sehemu ya msitu, sasa ni kivutio cha uwekezaji

February 15th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ZAIDI ya miaka 20 iliyopita, eneo la Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, lilikuwa kichaka na msitu.

Kwa baadhi, picha haikuwahi kuwajia kwamba wangeshawishika wanunue kipande cha ardhi sehemu hiyo kwa sababu ya hali yake.

“Wakati huo halikuwa na thamani, ploti zilikuwa zikiuzwa kwa bei ya chini mno,” anaeleza mmiliki wa ploti na mkazi eneo hilo Mama Patrick, ambaye amejenga nyumba za watu kuishi kwa kulipia kodi.

Mwihoko kwa sasa ni miongoni mwa maeneo ambayo bei ya ploti haikamatiki hapa nchini. Limekua kwa kasi.

Ni chini ya utawala wa Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki, eneo hilo lilianza kuwa kitamanio cha wengi.

Kuzinduliwa kwa serikali za ugatuzi, chini ya katiba ya sasa na iliyozinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013, Mwihoko imekuwa mojawapo ya maeneo yanayolengwa kwa maendeleo.

Miundomsingi inaendelea kuimarishwa kila uchao, mojawapo ikiwa ujenzi wa barabara ya Mwihoko-Githurai, ambayo imeunganishwa na ya Ruiru-Embakasi, maarufu kama Eastern Bypass.

Sehemu ya barabara ya Mwihoko-Githurai. Picha/ Sammy Waweru

Mbunge wa Ruiru Simon King’ara amekuwa akisimamia mradi huo na ambao unaendeshwa na serikali ya kitaifa. “Itasaidia kupunguza msongamano katika barabara ya Ruiru – Embakasi,” anasema Bw King’ara.

Kulingana na John Karira, ambaye alinunua kipande cha ploti miaka kadha iliyopita, Mwihoko inaendelea kuvutia wawekezaji tofauti. Mosi, ni sekta ya biashara na ambayo imenoga.

“Kwa kuwa ni eneo linalokua, biashara ya vifaa vya ujenzi imeshika kasi. Watu wanahamia humu, wanahitaji bidhaa za kula na ni biashara nyingine inayoridhisha,” Karira akaambia ‘Taifa Leo’ wakati wa mahojiano.

Alinunua ploti yake, yenye kimo cha futi 50 kwa 100 Sh450,000.

Anasema kipande hicho sasa thamani yake ni zaidi ya Sh1.5 milioni. Hiyo ikidhihirisha wazi ni eneo linalokua kwa kasi na kuvutia wawekezaji wengi.

Mengi ni majumba ya kifahari, hasa ya wamiliki binafsi yanayoendelea kujengwa, hata ingawa kuna kadha ya kupangisha ili kusitiri wenye mapato ya chini na ya kadri.

Isitoshe, barabara za kuingia maeneo ya ndani, yaani mashinani zinaboreshwa.

Kuna taasisi kadha za elimu, mojawapo ikiwa Chuo Kikuu cha Kiriri Women’s na Chuo cha Kiufundi cha St Kizito, miongoni mwa zingine. Shule za msingi na upili pia zipo.

Hata ingawa visa vya utovu wa usalama havikosi kushuhudiwa, eneo hilo lina kituo cha kijeshi. Mamlaka ya Kitaifa ya Mawasiliano, ndiyo CA, pia ina tawi la ofisi yake humo lenye mitambo ya mawasiliano na kupeperusha mawimbi.

Shughuli za usafiri na uchukuzi humo si hoja.

Barabara ya Mwihoko-Githurai na ambayo ni ya lami, imerahisisha shughuli hiyo. Vijigari vidogo aina ya tuktuk pamoja na matatu, vyote vimesheheni humo.

“Nauli ni kati ya Sh30 – 50 kulingana na saa,” anasema mhudumu wa tuktuk Joseph Mwangi.

Kimsingi, ni eneo ambalo gharama ya maisha ni nafuu, ikizingatiwa kodi ya nyumba pia ni nafuu.

La kutia moyo, kuna baadhi ya wanaolima hivyo basi mazao ya kilimo humo ni tele. “Ninafanya ufugaji wa kuku wa mayai na nyanya, pamoja na ndege wa umaridadi. Mbolea yao huitumia kuzalisha mazao shambani,” asema Margaret Maina, mkazi ambaye pia hulima mahindi na maharagwe.

Maji husambaziwa na Kampuni ya Usambazaji wa Maji jijini Nairobi, ndiyo Nairobi Water & Sewerage Company.

Mbali na hayo, kuna maji ya mradi.

Aidha, kuna waliochimba mashimo ya maji katika makazi yao, ingawa yana uchachu kiasi.