Habari Mseto

Mwili bila kichwa waibua hofu tele

May 27th, 2019 1 min read

Na HAMISI NGOWA

TAHARUKI ilitanda katika kijiji cha Vijiweni Mtongwe, Kaunti ya Mombasa baada ya mwili wa mwanaume anayekisiwa kuwa na miaka 30 kupatikana kwenye gofu la nyumba ukiwa bila kichwa.

Mwili huo ambao haukuweza kutambuliwa, ulipatikana majira ya jioni Jumamosi na watu waliokuwa wakipita karibu na nyumba hiyo ambayo bado haijakamilika kujengwa.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo, Bw Benjamen Rotich alisema mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti katika Hospitali Kuu ya Rufaa kanda ya Pwani.

Bw Rotich alisema haijabainika ikiwa marehemu aliuawa katika sehemu nyengine tofauti na kisha mwili wake kutupwa kwenye nyumba hiyo.

Aliwataka wakazi wenye habari kuwasaidia ili kutegua kitandawali hicho alichokitaja kama kisa cha kwanza cha aina hiyo kuwahi kutokea eneo hilo.

“Hatujawahi kushuhudia tukio kama hilo, kwa hivyo nawaomba wakazi walio na habari waweze kujitokeza na kutusaidia ili waliotekeleza kitendo hicho wakamatwe,’’ akasema.

Inadaiwa wapita njia hao walikuwa katika shughuli zao wakati walipogundua mwili huo kutokana na harufu kali.

Mmoja wa watu waliofika katika eneo la tukio alisema mwili huo ulikuwa katika sehemu mbili. Sehemu ya chini ya mwili ilikuwa imebakishwa na kinyasa huku kichwa kikiwa kando hatua chache kutoka ulipokuwa mwili huo.

“Nilikuwa miongoni mwa watu waliofika katika eneo la tukio lakini nilishindwa kukaa hata dakaka tatu kutokana na kitendo hicho cha kinyama kilichofanyiwa marehemu,’’ akasema.